Social Icons

Alhamisi, 15 Mei 2014

Wizara ya Maliasili inaongozwa kwa ubabaishaji


Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Naibu wake Mahmoud Mgimwa wakimsikiliza kwa makini Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani wa wizara hiyo, Mchungaji Peter Msigwa alipokuwa akitoa CD bungeni aliyodai inaonyesha moja ya kampuni inayofanya uwindaji haramu kwenye baadhi ya mbuga za wanyama nchini. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema Wizara ya Maliasili na Utalii inaongozwa kwa ubabaishaji na ‘mvutano wa kimasilahi’ baina ya waziri na katibu mkuu, hivyo kukwamisha shughuli za kuendeleza utalii.
Msemaji wa kambi hiyo (Maliasili na Utalii), Mchungaji Peter Msigwa alitoa kauli hiyo juzi wakati akisoma maoni kuhusu hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa wizara hiyo kwa mwaka 2014/15.
Alisema kambi ya upinzani inasikitishwa na mvutano baina ya Waziri Lazaro Nyalandu na Katibu Mkuu wake, Maimuna Tarishi ambao unaonyesha udhaifu wa Serikali.
“Hii inathibitisha kuwa Serikali ni dhaifu kwa kuwa, waziri na katibu mkuu wa wizara moja wanafanya kazi bila kushirikiana na kila mmoja anaonekana kumvizia mwenzake hadharani badala ya kukaa kwa pamoja kutekeleza maazimio ya Bunge,” alisema Msigwa.
Alisema kitendo cha Waziri Nyalandu kuwasimamisha kazi wakurugenzi wawili, lakini wakarudishwa na katibu mkuu huku akisema taratibu za kuwafukuza hazikufuatwa na hii ni dalili kuwa hata yeye (Nyalandu) siyo msafi kwa kuwa anashindwa hata kujua mipaka yake ya kazi.
Mbali na mvutano huo, Msigwa alisema maazimio ya Bunge kuhusu matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangili yanaendelea kupuuzwa na watumishi wenye tuhuma wakihamishwa vitengo.
“Ngoma ikivuma sana hupasuka, tena Mungu siku zote hamfichi mnafiki na debe tupu haliachi kutika (siyo maneno yangu, bali ya wahenga). Siyo mara ya kwanza kambi ya upinzani kuhoji juu ya usafi wa Lazaro Nyalandu,” alisema.
Alisema Waziri Nyalandu alipozungumza katika kikao cha wadau wa ulinzi wa maliasili Juni mwaka jana mkoani Iringa, aliahidi kuwa majina ya majangili yakiwamo ya vigogo yangetangazwa hadharani, lakini hadi sasa hakuna majina yoyote yaliyotangazwa hadharani.
Uteuzi wa Sarakikya
Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) alizungumzia kitendo cha Waziri Nyalandu kumteua Paul Sarakikya kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori, jambo alilosema ni kinyume na haki za binadamu.
Msemaji huyo alibainisha kuwa, wakati wote Watanzania wanajiuliza maswali ambayo hayajapata majibu kuhusu vigezo vilivyotumika kumteua Sarakikya.
“Katika Operesheni Tokomeza, mtu huyu alikuwa kiongozi wa utekelezaji wa moja kwa moja na kinachodaiwa ni uvunjifu wa haki za binadamu, inashangaza kuona mtu huyu tena ndiye ana nafasi ya kukaimu ukurugenzi, lini kawa msafi?” alihoji Msigwa.
Msigwa pia alizungumzia shehena ya meno ya tembo ambayo alisema Serikali inatafuta soko lake badala ya kuyateketeza kwa kuwa kuuza ni kuchochea ujangili nchini.
Kudharau Mahakama
Msigwa alisema Mkurugenzi wa Wanyamapori alipuuza uamuzi wa Mahakama ulioizuia Kampuni ya Uwindaji ya Green Miles Safaris Limited kuwinda baada ya kubainika inavunja sheria.
Msigwa alisema kuna taarifa kuwa kampuni hiyo ilishapewa zuio na mahakama la kufanya uwindaji kutokana na kutozingatia sheria, lakini ilipitia mlango wa nyuma na kuomba kibali cha uwindaji na kupewa.
Ajibu hoja
Akijibu hoja mbalimbali za wabunge jana jioni, Nyalandu alisema Serikali itachukua vielelezo vyote vya Msigwa kuhusu Kampuni ya Green Miles Safaris Limited kufanya shughuli zake kinyume cha sheria na kuvifanyia kazi.
Kwa upande wa wakurugenzi wizarani, alisema kuna upotoshaji wa baadhi ya vyombo vya habari kwa kuwa hakuna mfanyakazi aliyefukuzwa kazi. .. “Siyo Mkurugenzi Bwana Songorwa (Alexander) wala mtumishi mwingine.”
Alisema hatua aliyochukua ni kuwahamisha vituo vya kazi, Profesa Songorwa alipelekwa Chuo cha Mwika kuwa mwalimu wakati Profesa Jaffar Kidegesho alihamishiwa Hifadhi ya Selous.
“Sheria ya utumishi wa umma haikuvunjwa wala kanuni zake, naomba nilithibitishie Bunge lako kuwa habari hizi nyingi za kwenye magazeti hazikuwa na usahihi wowote,” alisema.
Akizungumzia shutuma za Kambi Rasmi ya Upinzani juu ya kuteuliwa kwa Sarakikya kuwa Kaimu Mkurugenzi Wanyamapori, Nyalandu alisema hakuna anayeweza kuyaelewa yote yaliyotokea katika Operesheni Tokomeza ila hadi hapo Tume ya Kimahakama itakapokamilisha kazi yake.
“Ndugu Sarakikya ni mmoja watumishi waandamizi na waliobobea katika kazi walizofanya… Kwa hali yoyote ile Serikali haitamwonea mtu haya endapo atabainika na tume hii kwamba alivunja maadili yake,” alisema.
Ingawa Nyalandu hakujibu kuhusu uhusiano wake kikazi na Katibu Mkuu Tarishi, baada ya bajeti yake kupitishwa Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema yamezungumzwa mambo mengi kuhusu suala hilo, hivyo inaonyesha kuna tatizo.
Makinda alishauri waziri kuyo na katibu mkuu wake washirikiane ili kutimiza malengo ya Serikali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates