Meneja Biashara wa Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) amekutwa amekufa hotelini katika mazingira ya kutatanisha muda mfupi baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam akitoka Dodoma ambako alihojiwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Meneja huyo, Julius Gashaza, ambaye alikuwa na jukumu la kupanga bei za mafuta za kila mwezi, alihudhuria kikao hicho mjini Dodoma kwa siku mbili; Ijumaa na Jumamosi iliyopita kuhusu mambo mbalimbali, yakiwamo kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini, mgawo wa fedha unaotolewa na Ewura kwenda kuhudumia umeme vijijini (Rea) na fedha za mfuko wa barabara.
Jeshi la Polisi, Mkoa wa Temeke limethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa meneja huyo alikutwa amejinyonga kwa kutumia tai kwenye hoteli ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo Vituka wilayani Temeke.
Nyumbani kwa meneja huyo wa Ewura, kulikuwa na waombolezaji waliokuwa kwenye vikundi na kikao cha maandalizi ya mazishi kilifanyika ndani ya nyumba ya marehemu iliyopo Yombo Vituka na baadaye kuhamia nyumba ya jirani.
Kamati ya Bunge ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ilikutana na maofisa wa Ewura, akiwamo Gashaza na wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kugundua kuwapo kwa tofauti katika takwimu za kiwango cha mafuta kilichostahili kutozwa kodi.
Gashaza alikwenda Dodoma kutoa ripoti ya Ewura kwenye kamati hiyo ya Bunge akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kamati hiyo, takwimu za Ewura ziliashiria kuwa fedha zilizopatikana ni nyingi zaidi ya zile zilizoelezwa na TRA, lakini Wizara ya Fedha ilisisitiza zifuatwe takwimu za mamlaka ya mapato.
Habari hizo, zinasema baada ya kurejea Dar es Salaam juzi majira ya saa tatu usiku, Gashaza hakwenda nyumbani kwake na badala yake alikwenda kwenye hoteli iliyo karibu na nyumbani ambako mkewe na ndugu yake mmoja walimfuata na akawaeleza kuwa anahisi kutishiwa maisha yake.
Baadaye walifanya maombi maalumu kabla ya kuachana naye.
Inadaiwa kuwa marehemu aliomba akalale hotelini kwa sababu hakuona kama ana amani kulala nyumbani kwake na ilipofika asubuhi alikutwa ‘amejinyonga’ ndani ya chumba alicholala hotelini humo.
Nyumbani kwa marehemu waombolezaji walikusanyika katika makundi, lakini baada ya kukaa katika kikao cha familia walitoka na kauli moja kuwa hawatasema chochote na kwamba jukumu hilo libaki mikononi kwa polisi.
Polisi wathibitisha
Kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Seleiman Kova hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo akidai kuwa anayetakiwa kulizungumzia ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engbert Kiondo.
Alipotafutwa, Kamanda Kiondo alisema kulingana na taarifa zilizopo Gashaza aliitwa bungeni Mei 14 na akarejea Dar es Salaam Mei 17. Alisema aliporejea, Gashaza aliaga nyumbani kwake kuwa hajisikii vizuri na kuelekea Hoteli ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo ambako alichukua chumba Namba 113.
Kamanda Kiondo alisema akiwa hotelini, Gashaza alimpigia simu rafiki yake mmoja anayejulikana kwa moja la Silipwango akimweleza kuwa yupo hotelini hapo kujipumzisha kwa sababu bungeni aliulizwa mambo ambayo hayakumpendeza na kwamba alihitaji kupumzika.
Rafiki huyo, kwa mujibu wa Kiondo, alimpigia simu mkewe anayeitwa Judith akamweleza alivyoelezwa na mumewe na baadaye kwa pamoja wakamfuata hotelini ambako baada ya kuzungumza nao kwa muda mfupi, aliwaomba wamuache apumzike na ndipo walipoondoka.
Asubuhi, Silipwango alipigiwa simu na mkewe kumueleza kuwa Gashaza hakurudi nyumbani na akaamua kupitia kwenye hoteli waliyomuacha na alipofika akakuta watu wamejaa. Alipouliza akaelezwa kuwa kuna mtu amejinyonga chumbani.
Kamanda Kiondo alisema Gashaza alijinyonga kwa kutumia tai aliyoifunga kwenye bomba la maji ambalo pia lilikatika na hivyo kuukuta mwili wake ukiwa sakafuni.
Kilichojiri kamati ya bajeti
“Kisheria kodi ya mafuta ni Sh263 kwa lita inakwenda mfuko mkuu Hazina na Sh50 inakwenda kwa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), lakini takwimu za mafuta yaliyouzwa inayostahili kutozwa kodi kati ya TRA na Ewura zinatofautiana,” alisema mmoja wa wajumbe.
“Kwa hiyo Kamati ya Bajeti iliwaita wote (Ewura na TRA) na kwa kweli wajumbe wa kamati tulikuwa wakali sana, hatutaki mchezo tulitaka kujua nani anasema ukweli,” alidokeza mjumbe huyo.
“Uko ugomvi mkubwa tu kati ya TRA na Ewura kuhusu nani hasa mwenye takwimu halisi,” alisema mjumbe huyo na kudokeza kuwa meneja huyo alisema kila kitu kwa uwazi.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa baada ya vuta nikuvute ndani ya kamati hiyo, iliamuliwa watendaji wa vyombo hivyo viwili wakafanye ulinganisho na kupeleka jibu kwa kamati hiyo. Ewura waliwasilisha takwimu zao Jumamosi.
“Tension (mvutano) ni kubwa kwa sababu kuna watu wizarani hawazitaki takwimu za Ewura na wanataka za TRA ambazo sisi kama wajumbe tunaziona hazina uhalisia kunaweza kukawa na ufisadi,” alisisitiza mjumbe mwingine.
Chenge azungumza
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge alipoulizwa jana, alikiri kufanyika kwa kikao kilichomuhusisha meneja huyo na kwamba taarifa alizotoa zilionekana tofauti na zile za TRA.
“TRA ni chombo cha Serikali na Ewura ni chombo cha Serikali, kwanini wawe na takwimu zinazotofautiana? Hilo tu ndio tumewaagiza wakae pamoja watuambie zipi ni takwimu halisi,” alisema Chenge.
Alipoelezwa kuwa mmoja kati ya maofisa wa Ewura waliofika mbele ya kamati yake amejinyonga, Chenge alionyesha kushtushwa na kuhoji kama taarifa hizo zina ukweli.
“Una uhakika kwamba amejinyonga? lini? Kama ni kweli basi ni jambo la kusikitisha sana, lakini hiyo sasa ni kazi ya polisi. Mimi nisingependa sana kuzungumza, tuwaachie wao wachunguze sababu za kifo chake,” alisema Chenge.
Serikali inaelezwa kuwa katika hali mbaya kifedha na kamati hiyo ya Bajeti imekuwa ikifanya kila linalowezekana kuinusuru kwa kukutana karibu kila siku na Hazina na wadau wengine wanaochangia fedha katika mfuko wake.
Kwa bajeti ya mwaka 2013/2014 iliyopitishwa na Bunge, Serikali imejikuta ikiwa na upungufu wa Sh1.8 trilioni hali ambayo kamati ya bajeti inatafuta kila njia ikiwamo kushauri vyanzo vipya vya mapato ili kunusuru bajeti ya mwaka huu wa 2014/2015.
Bajeti ambazo zinaelezwa kuiumiza kichwa Serikali ni ya Maji, Miundombinu na Nishati na Madini ambazo zinaelezwa kupata mgawo kidogo mwaka jana na kuzifanya zishindwe kutekeleza miradi mbalimbali.
Mkurugenzi wa Petroli wa Ewura, Godwin Samwel alisema alipata taarifa jana saa 3:00 asubuhi.
Alithibitisha kuwa marehemu alikuwa Dodoma kikazi kwenye vikao na kamati ya Bunge tangu Alhamisi iliyopita.
Baada ya kumaliza kazi ndiyo ndiyo jana (juzi) alichelewa sana kurudi ndipo alipoamua kujipumzisha kwenye nyumba ya wageni (iliyopo karibu na nyumbani kwake) ambako alikutwa amefariki,” alisema Samwel.
Alisema marehemu alikuwa mwadilifu, mchapa kazi na asiye na tatizo lolote kazini na kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni