Social Icons

Jumanne, 20 Mei 2014

Watu 60 wahofiwa kuugua dengue Lindi


Afisa uhusiano wa Manispaa ya Temeke,Joyce Msumba

Zaidi ya wagonjwa 60 kutoka wilaya za mkoa wa Lindi wanahofiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa dengue. 

Kutokana na hali hiyo, wanatarajiwa kuchuliwa vipimo na kufanyiwa uchunguzi kwenye maabara ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na hospitali ya mkoa huo kukosa vifaa vya kutambua ugonjwa huo.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dk. Theophil Malibiche, alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.Dk. Malibiche watachukua wagonjwa wanaoonyesha dalili za dengue. 


Alisema hadi sasa hakuna mtu aliyebainika kuwa na homa hiyo wala aliyefariki na kwamba mkoa umejipanga kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya katika wilaya zote za mkoa huo. 

Aliwaomba wananchi mkoani humo kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo kwa kufanya usafi wa mazingira na kuangamiza maeneo ya mazalia ya mbu wakati utaratibu wa kupata madawa za chanjo na kinga ukisubiriwa.

Wakati huo huo, idadi ya wagonjwa waliogundulika na ugonjwa huo katika Hospitali ya Amana, jijini Dar es Salaam, sasa imefikia 79 tangu ugonjwa huo uibuke.

Akizungumza na NIPASHE, Daktari Kiongozi wa Hospitali hiyo, Andrew Method, alisema kati ya wagonjwa hao 73 waliruhusiwa na sita bado wamelazwa.

Aidha, Dk. Method alisema katika hospitali hiyo hakuna kifo kilichotokana na ugonjwa huo.

Katika Hospitali ya Temeke idadi ya wagonjwa ambao wameugua ugonjwa huo tangu kuibuka mwaka huu ni 72 na kati ya hao, 62 wameruhusiwa.

Afisa uhusiano wa Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba, alisema wagonjwa 10 bado wamelazwa na kuwa kati ya hao, sita ni wanawake na wanne ni wanaume.

Msumba alisema pia hospitali hiyo inachukua tahadhari ya kuendelea kupuliza dawa na wagonjwa kulazwa ndani ya vyandarua kwa ajili ya kuzuia kuambukiza wengine.

Katika Hospitali ya Mwananyamala, idadi ya wagonjwa mpaka imefikia 144, wapya ni wanne na mmoja ndiye amelazwa, kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Faustinias Ngonyani.

Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hadi jana hapakuwapo na mgonjwa wa dengue.

Imeandikwa na Elizabeth Zaya, Jimmy Mfuru, Hussein Ndubikile, Dar na Hamisi Abdelehemani, Lindi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates