Baada ya msemaji wa kambi ya Upinzani Bungeni ambaye ni waziri kivuli wa wizara ya Habari,Michezo, Vijana na utamaduni kumtuhumu Zitto Kabwe kuhusika na kinachoitwa ufisadi katika shirika la TANAPA na NSSF, mashirika haya yameamua kutoa ufafanuzi kuhusiana na tuhuma hizi ili kuweka mambo sawa......
Meneja Uhusiano wa TANAPA, Paschal Shelutete ameliambia gazeti la Mwananchi toleo la leo ( May 30) kuwa shirika hilo linakitambua kiasi hicho kilichotajwa na wapinzani na kwamba fedha hizo zilikuwa ni malipo ya wasanii wa Leka Dutigite ambao walifanya kazi ya kuitangaza Hifadhi ya Saadan...
“Leka Dutigite ilifika Hifadhi ya Saadan na kuitangaza kupitia kazi za sanaa... sikumbuki ni lini lakini walifanya kazi na DvD zake zipo.
“Ifahamike si Leka Dutigite pekee, tunafanya kazi na wasanii mbalimbali kutangaza vivutio, mbuga na hifadhi zetu,” Shelutete ameliambia gazeti la Mwananchi
Naye Meneja Kiongozi wa Idara ya Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa NSSF, Eunice Chiume ameliambia gazeti hilo kuwa pesa walizozitoa kwa kundi hilo zilikuwa malipo ya kutengenezea wimbo maalumu wa shirika hilo na nyingine ni za udhamini wa onyesho lililofanyika mwaka jana mkoani Tanga.
“Kweli mara ya kwanza tuliwalipa Sh25 milioni wasanii wa kundi hilo ili watutengenezee wimbo na Sh56 milioni zilikuwa za udhamini wa onyesho lao, lakini kwa masharti ya kututangaza jambo ambalo lilikuwa na mafanikio kwetu kwani tumefanikiwa kupata wateja wapya 30,000 kutoka sekta isiyo rasmi,” alisema Chiume.
Alisisitiza kuwa wametumia kiwango hicho cha pesa ili kujitangaza kwa kuwa hata mashirika ya kijamii yanapaswa kufanya hivyo ili kuvutia wateja wengi zaidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni