Social Icons

Jumamosi, 10 Mei 2014

PREMIERSHIP KESHO NI VITA YA WATAKA KOMBE NA WASIO NA PRESHA


MANCHESTER CITY


UTAMU upo kesho, hakuna anayeweza kukataa tena kwamba Ligi Kuu England, maarufu kama Premiership imekuwa tamu mpaka basi.

Bingwa wa ligi hiyo atapatikana kesho, ndiyo siku ya mwisho ya ligi hiyo na hili linalonyesha ubora wake na namna mambo yalivyo magumu.
Iwapo utaamua runinga kubwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kualika mashabiki, bila shaka watu watafikia nusu au kuujaza kabisa hasa wakikubali kukusanyika na kuangalia pamoja mechi za mwisho za Premiership ambayo ni maarufu zaidi duniani katika soka.

Majibu ya walioteremka daraja yameishapatikana, Cardiff City, Fulham  na Norwich City wanajua kabisa kuwa msimu ujao watakipiga Ligi Daraja la Kwanza England.
LIVERPOOL
Ukiangalia kwenye msimamo, inaonekana hivi, kama Wes Brom yenye pointi 36 itapoteza mechi ya mwisho itabaki ilipo na kama Norwich atashinda, atafikisha 36 pia lakini tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa inamuangusha kwa kuwa lazima ashinde zaidi ya mabao 15, haitawezekana.
Ukirudi kwenye ubingwa sasa hakuna ubishi tena kwamba Chelsea ilishajiondoa kaika mbio hizo hasa baada ya ile sare ‘tasa’ dhidi ya Norwich na kuifanya ifikishe pointi  79 ambazo hazina faida tena.
Ikishinda ina uwezo wa kufikisha pointi 82 wakati Manchester City imeishafikisha 83. Maana yake haimo na kwenye kuuwania ubingwa kesho, Jose Mourinho analitambua hilo.

Manchester City ndiyo wenye nafasi kubwa zaidi lakini bado nafasi hiyo unaweza kuiweka kwa Liverpool kwa kuwa huu ni mchezo soka.

Man City:
Ndiyo timu yenye nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa kuwa ushindi na hata sare, bado mambo yanaweza kuwa mazuri kwa vijana wa Manuel Pellegrini.
Iwapo itashinda, hata kama ni bao moja tu, basi muhimu pointi tatu na itakuwa na 86 ambazo haziwezi kuguswa na timu yoyote msimu huu.
Hata kama itatoka sare bado ikiwa na pointi 84 ambazo Liverpool atazifikia kama akishinda, lakini bado tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ya City iko juu, imefunga mabao 100 na kufungwa 37 tu.
Ugumu kwa Man City, hata kama ina kiwango kizuri inakutana na West Ham ambayo haina presha hata kidogo na wala si timu ya kuidharau.
West Ham jina la utani kama ‘Wagonga Nyundo’, ina pointi 40 katika nafasi ya 12. Hata ikishinda itabaki hapo ilipo kwa kuwa Crystal Palace kwenye nafasi ya 11 ina pointi 44.
Maana yake, West Ham itacheza mechi hiyo bila ya presha na inachoangalia ni rekodi au kuepuka kuwa daraja la Man City kutwaa ubingwa.
Liverpool:
Baada ya kuteleza na kuruhusu mabao matatu kusawazishwa dhidi ya Crystal Palace na kuzaa sare ya bao 3-3, kuifanya iwe haina ujanja na kwake kikubwa ni ushindi tu katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Newcastle ikiwa nyumbani Anfield, kesh.
Pamoja na kushinda, Liverpool watalazimika kupiga magoti kabla na wakati mechi ikiendelea ili kuwaombea Man City ‘dua mbaya ili wapoteze mechi yao dhidi ya West Ham wakiwa kwao Etihad.
Iwapo wao watashinda na kufikisha pointi 84, halafu City wakapoteza maana yake kombe ni lao, sasa inategemea watazifanyaje kazi hizo mbili za kusaka ushindi na ‘maombi’.
Lakini tatizo kwao linaweza kuwa hivi, pamoja na mashabiki wa Newcastle lakini hata ikipoteza haitashuka au ikishinda haitapata lolote muhimu.
Newcastle ina pointi 49 katika nafasi ya tisa, iwapo itashinda itakuwa na pointi 52, wakati Southampton katika nafasi ya nane ina pointi 55 tayari.
Hivyo Newcastle itakuwa kwenye nafasi nzuri kwa kuwa itacheza mechi hiyo bila ya kuwa na presha hata kidogo.
Unapocheza na kikosi kisichokuwa na presha pia ni tatizo, kwani wao wanakuwa katika nafasi nzuri ya kufanya mambo kwa uhakika kuliko wewe uliyepania zaidi.
Hivyo Liverpool na Man City pia wanapaswa kuwa makini, lasivyo, ndoto zao zinaweza kukwama katika siku ya mwisho kabisa ya ligi.

Mechi za zote za kesho zitakuwa tamu, lakini mbili za mjini Manchester na ile ya jijini Liverpool ndiyo zitakuwa tamu zaidi kwa kuwa zina majibu ya nani mfalme mpya wa England baada ya yule wa msimu uliopita Man United, kujiondoa mapemaaaa!!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates