Miongoni mwa habari kubwa wiki hii ni hii ya bomu kulipuliwa kwenye kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) Mwanza ambapo lilijeruhi mtu mmoja alielazwa hospitali ya Bugando.
Mkuu wa dayosisi Askofu Andrew Gulle anasema: "May 5 2014 bomu limelipuka katika usharika wa kanisa kuu Imani kwenye eneo la rest house saa mbili usiku, ni bomu la kutengenezwa kwa mkono na lilikua limewekwa kwenye karatasi za kufungia zawadi na kuwekwa kwenye mfuko wa plastiki na kuwekwa kwenye varanda ya rest house yetu.
"Kifurushi hicho kimekuwepo kuanzia siku ya Ijumaa ambapo ilipofika Jumatatu saa mbili usiku muhudumu wa rest house Benadertha alianza kujiuliza kifurushi hicho kina nini na kwanini kimekuwepo hapo kwa siku tatu? ambapo mwishowe aliamua kukifungua ili kujua kuna nini ndani lakini ghafla bomu lililipuka kwa kishindo na moshi mwingi huku likisambaza misumari midogomidogo na kumjeruhi miguuni na usoni..
"Alikimbizwa hospitali ya rufaa ya Bugando na kufanyiwa upasuaji na kulazwa kwenye wodi ya mifupa, hatujui lengo la wahusika lilikua kumuumiza yeye au wengi zaidi, au walishindwa kulifikisha walipotaka lifike?
"Vikao vya kanisa vimekaa kutafakari na sasa natamka kama kiongozi wa Dayosisi yale tuliyokubaliana kuyasema kwa Watanzania……
"Tunalaani kitendo hicho kilichofanyika kwenye eneo la Kanisa, tunaomba makanisa yetu kuboresha ulinzi katika maeneo yetu yote maana kwa sababu hatuwezi kujua watu hawa wamekusudia kuweka mabomu wapi na wapi.
"Tunaomba serikali ihakikishe inawashika waliohusika na kutokomeza mtandao huu wa ugaidi kabla haujaota mizizi na kuhatarisha amani tuliyoizoea Tanzania.
"Mwisho tunatoa wito kwa Wakristo wote wawe watulivu, wasiogope wala wasitishwe na mashambulizi yanayotendeka, tunatoa wito kwa Wakristo wote kwamba kusitokee fujo popote wala kulipiza kisasi, silaha yetu kubwa ni maombi na kumtegemea Mungu, wakati huu kanisa linapoteswa ndio wakati wa kumtegemea Mungu zaidi na kuhubiri habari njema"
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni