Washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wamewasili nchini leo asubuhi (Julai 16 mwaka huu) kutoka Tunisia kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Msumbiji itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wachezaji hao wamefikia hoteli ya Courtyard, Seaview Upanga na leo (Julai 16 mwaka huu) watafanya mazoezi kwa programu maalumu waliyopewa na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij wakati wakiwasubiri wenzao.
Naye kiungo Mwinyi Kazimoto anayecheza mpira wa miguu katika klabu ya Almarhiya ya Qatar atawasili nchini kesho (Julai 17 mwaka huu) saa 1.30 asubuhi kwa ndege ya Qatar Airways.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itawasili Dar es Salaam kesho (Julai 17 mwaka huu) saa 3.20 asubuhi kwa ndege ya Fastjet kutoka Mbeya tayari kwa maandalizi ya mwisho kabla ya kuivaa Msumbiji.
RAIS MALINZI KUZUNGUMZA NA WAANDISHI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa na mkutano na waandishi wa habari Ijumaa (Julai 18 mwaka huu).
Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni