Social Icons

Jumanne, 15 Julai 2014

JUMUIYA YA KIKRISTO TANZANIA (CCT) LATOA TAMKO ZITO KWA RAIS JAKAYA KIKWETE.


Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imetoa tamko zito ikieleza kushangazwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kupinga mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya Watanzania na kusema kitendo hicho kimeishusha hadhi Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyoiteua.

Tamko hilo la CCT ni mwendelezo wa lawama ambazo Rais Kikwete amekuwa akitupiwa na taasisi na watu mbalimbali kutokana na mchakato wa kuandika Katiba Mpya kwenda mrama baada ya mkuu huyo wa nchi kueleza maoni yake dhidi ya mapendekezo ya muundo wa Serikali ya Muungano wakati akilihutubia Bunge la Katiba.

Miongoni mwa watu waliojitokeza kuzungumzia kauli hiyo katika siku za karibuni ni aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, maaskofu wa Kanisa Katoliki, katibu mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad.

Jana, CCT iligongomea msumari juu ya lawama hizo ikifananisha kauli ya kiongozi huyo aliyoitoa Machi 21, mwaka huu wakati akifungua Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma na mama anayeamua kubeba mimba na kujifungua kwa uchungu, kisha kumtelekeza mtoto, badala ya kumfurahia.

Pia katika tamko lake, jumuiya hiyo imewataka wajumbe wa Bunge hilo kuheshimu maoni ya Watanzania yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kuacha kujadili maoni ya vyama vyao vya siasa.

“Inashangaza jinsi chama kimoja cha siasa kinavyolazimisha wabunge na wanachama wake kukubaliana na mapendekezo yake ambayo yanapingana wazi na yaliyomo katika rasimu ya Katiba,” linaeleza tamko hilo lililotolewa baada ya Mkutano wa 48 wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya hiyo uliofanyika Julai 2 na 3 mjini Dodoma.

Tamko hilo pia limetaja mambo mengine saba yanayolikabili Taifa.

Kabla ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba kutoa rasimu ya pili ya Katiba Desemba 30, CCM ilisambaza waraka kuwaarifu wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka CCM kuwa msimamo wa chama hicho tawala ni Muungano wa serikali mbili, tofauti na mapendekezo ya wananchi yaliyo kwenye rasimu hiyo ambayo yanataka serikali tatu.

Licha ya mara kadhaa Jaji Warioba kutetea kile kilichopendekezwa na Tume yake, wajumbe hao kutoka CCM wameyapinga maoni hayo na kusisitiza kuwa yanaweza kubadilishwa kadri Bunge la Katiba litakavyoona inafaa.

Kitendo hicho kilisababisha wajumbe kutoka vyama vingine kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao Aprili 16 uliamua kususia vikao vya Bunge hilo ukitoa masharti kuwa utarejea bungeni kama chombo hicho cha kuandika Katiba kitajikita kujadili mapendekezo ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba.

Bunge hilo litaendelea na vikao vyake Agosti 5 na mwenyekiti wake, Samuel Sitta anahaha kushawishi Ukawa walegeze msimamo wao.

Katika hotuba yake ya kufungua Bunge la Katiba, Rais Kikwete aligusia mambo kadhaa yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani kutekelezeka, ikiwa ni pamoja na muundo wa serikali tatu kwa maelezo kuwa idadi ya watu waliotaka muundo huo ni ndogo.

“Tunampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kutoa wazo la kuandikwa kwa Katiba Mpya na kuteua wajumbe wa Bunge la Katiba. Tunaamini kilichoandikwa katika Rasimu hiyo alikikubali na kubariki kutolewa kwa rasimu hiyo kwa sababu alijua ndiyo maoni ya wananchi,” linasema tamko hilo.

“Pia tunaamini kuwa mwenye kutoa hoja (Rais Kikwete) alikuwa na uwezo wa kuzuia rasimu hiyo isitolewe endapo kuna ibara ambayo ina mwelekeo ambao ungekuwa hatari kwa mustakabali wa taifa letu.”

Jumuiya hiyo imesema kitendo cha Rais Kikwete kupingana na kilichomo katika rasimu ya Katiba kimeshusha hadhi ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Hotuba hiyo ilishusha hadhi ya kazi nzuri iliyofanywa na wajumbe wa Tume ambao waliteuliwa na rais mwenyewe kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi,” linasema tamko hilo.

“Jambo hili linaweza kufananishwa na mama anayeamua kubeba mimba, kuilea mimba hiyo kwa gharama na kujifungua kwa uchungu halafu mtoto akishazaliwa, badala ya kufurahi anaamua kumtelekeza.”

Ushauri kwa vyama

Tamko hilo linasema: “Viongozi wa vyama vya siasa na wabunge waheshimu uhuru wa mawazo ya wanachama wao hata kama watatofautiana katika hoja moja au nyingine na wasitumie nafasi zao kulazimisha wanachama wote kukubaliana na mawazo yao.”

Jumuiya hiyo imeifananisha hatua hiyo na udikteta kwa wanachama wa chama husika.

“Katika jambo hili CCT inahimiza wabunge wote waangalie masilahi ya kitaifa kwa upana zaidi na siyo ya vyama vyao.”

Inasema licha ya kuwa wakati wa kutoa maoni CCT ilipendekeza muundo wa serikali moja, inakubaliana na pendekezo la kuwapo serikali tatu kwa sababu ni maoni yaliyotolewa na wananchi walioamini kuwa zitamaliza kero za muungano.

Lugha za kejeli

Katika tamko hilo, CCT imeshangazwa jinsi vikao vya Bunge la Katiba vilivyotawaliwa na mjadala wa muundo wa serikali, huku mambo mengine ya msingi yaliyomo katika rasimu ya Katiba yakiwekwa kando.

“Lugha zisizo za kiungwana zinazotolewa na baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba kwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba zinaonyesha ni jinsi gani wabunge hao wasivyoheshimu uteuzi wa wajumbe wa Tume hiyo,” linasema tamko hilo.

Katika tamko hilo, CCT pia iligusia suala la udini, maadili, kukosekana kwa uvumilivu wa kisiasa nchini, mauaji ya raia, uchaguzi, umasikini na ulipaji wa kodi, hasa kwa mashirika ya dini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates