Social Icons

Ijumaa, 11 Julai 2014

MAAJABU YA MUNGU KATIKA DAMU YA MWANA DAMU MWILINI.

Mwili wa binadamu umesheheni vitu vingi sana, lakini moja ya vitu vinavyoshangaza ni damu. Kiungo hiki ni moja ya ogani ya mwili ya kipekee ambayo ipo katika maumbile ya kimiminika.
Ndiyo maana Shirika la Afya Duniani lilitenga siku ya uchangiaji damu inayoadhimishwa kila tarehe 14 Juni ya kila mwaka. Siku hii ilikuwa juma lililopita.
Ukichunguza kwa makini inavyozunguka mwilini pamoja na kazi zake unaweza kubaini ni ya kipekee na kushangaza.
Damu ndio mfumo pekee wa mwilini wa usafirishaji ambao uko mchakamchaka wakati wote. Kwa kawaida damu huwa haitulilii kusimama sehemu moja.
Wakati wowote husukumwa kwenda sehemu mbali mbali za mwili na baada ya kutumika hurudi kusafishwa katika mapafu.
Miili yetu kila siku za maisha yetu huweza kukumbana na vimelea vya maradhi, ambavyo kama si damu usingeweza kuhimili mashambulizi ya maadui hao.
Damu imebeba mabilioni ya chembe hai, gesi na virutubisho mbalimbali. Chembe hai kuu ambazo zipo katika damu ni nyekundu, nyeupe na sahani.
Damu ni kama vile idara ya maji ya mwili huzunguka katika mishipa maalumu iliyo kama bomba kwa kusukumwa na moyo.
Damu ni aina ya tishu ambayo huwa ni kwa ajili ya kusafirisha bidhaa muhimu mwilini, miongoni vikiwemo virutubisho. Damu hiyohiyo hutumika kukusanya taka sehemu mbalimbali za mwili na kuzisafirisha hadi kutolewa nje. Wale wahenga waliosema kuwa damu ni nzito kuliko maji hawakukosea kwani, ni ukweli wa kisayansi kuwa damu ni nzito mara 5 hadi 6 zaidi ya maji.
Damu nyekundu iliyokolea huwa na mwonekano wa kumtisha mtu yoyote anapoitazama. Yawezekana zipo rangi zinazofanana na damu lakini pale mwanadamu anapoona damu hata ya mnyama aliyegongwa barabarani humpa woga fulani.
Wanasaikolojia wanaeleza sababu ya kinadharia ya kuwa mwanadamu anatambua umuhimu wa damu kama uhai wake. Pale anapoiona inatoka, hofu yake huwa ni kupoteza uhai.
Historia inaonyesha wanadamu wa zamani waliwahi kujaribu kuongezeana damu na hata wakatumia damu za wanyama, na za kwao kuwaongezea majeruhi wa vita, lakini bahati mbaya hawakupona.
Baadaye wanasayansi walitumia historia kama hizi kuja na majibu ya kisayansi kuwa damu huwa na makundi yake maalum pamoja na chembechembe fulani katika nyuso za seli ambazo kama haziko kundi moja hutokea mpambano wa chembe hai na mtu hupoteza maisha.
Mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano mwilini wake huzalisha chembe hai nyekundu katika rojorojo za mifupa yote ya mwili zijulikanazo kama uboho.
Huwa ni rojorojo ya rangi ya njano ya mifupa mirefu lakini baadaye anapofikisha miaka 20 mifupa hii haitengenezi chembe hai nyekundu.
Badala yake hutengenezwa zaidi katika mifupa ya mgongo, kifua, mbavu na kiuno. Damu imebeba mamilioni ya vitu huku asalimia 45 ni chembe nyekundu, sahani na nyeupe.
Damu huwa na sehemu iliyo na maji maji ambayo kitaalam huitwa plasma ambayo ni asilimia 55. Hii imesheheni vitu vingi yakiwemo maji kwa asilimia 91, gesi ya oksijeni, kaboni dayoksaidi, protini, askari mwili, vimeng’enya na madini.
Kazi za damu ni zipi?
Kazi kuu ya damu ni usafirishaji; hubeba virutubisho baada ya kusagwa katika mfumo wa umeng’enywaji chakula.
Hubeba gesi ya oksijeni kutoka katika mfumo wa upumuaji yaani mapafu kwenda tishu mbalimbali za mwili na kwenye ogani hizo hubeba hewa ya kaboni dayoksaidi kurudi katika mapafu ili kupumuliwa nje.
Damu pia hubeba taka mwili au mabaki yasiyotakiwa mwilini baada ya vitu venye tija kwa mwili kuchukuliwa, kisha hupelekwa katika maeneo au ogani zinazohusika na utoaji taka, ufifishaji na kuondoa sumu mwilini.
Damu hubeba mfumo mzima wa kinga kwa ajili ya ulinzi wa mwili, chembe nyeupe ambazo ziko za aina tofauti zaidi ya tano.
Hizi ndizo zinazopambana kama jeshi la mwili dhidi ya maradhi. Zipo chembe zinazokumbatia kimelea na kukiharibu, zipo chembe hai ambazo huwa na muundo katika nyuso zao ambazo huzitumia kama silaha.
Pia zipo kemikali au vitu vinavyoweza kufifisha na kuua vimelea au sumu za vimelea.Chembe sahani hutoa ulinzi kwa kuzuia damu isimwagike. Likitokea jeraha huweza kulifunga na kuigandisha damu sehemu hiyo ili isiendelee kutoka katika mzunguko wa damu.
Damu ina jukumu la kuweka sawia, kurekebisha, kudhibiti mazingira ya ndani ya mwili yasibadilike ili chembe hai na shughuli za mwili zisiathirike.
Kazi kama ya kudhibiti joto la mwili, kudhibiti kiwango cha maji na chumvi ndani na nje ya seli na kudhibiti kiwango cha tindikali na ukakasi wa damu. Damu huwa na viambata maalumu vyenye kusaidia la ubebaji wa vitu kama madini ya chumba, shaba, homoni, tindikali za mafuta, dawa zinazotumiwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates