Social Icons

Ijumaa, 11 Julai 2014

KUELEKEA MECHI YA FAINALI THOMAS MULLER AMPIGA DONGO LIONEL MESSI

430663_heroa

MSHAMBULIAJI wa Ujerumani, Thomas Muller amesema kamwe hajawahi kufungwa na timu ambayo ndani yake yupo Lionel Messi na atapenda kuendeleza hilo wakati watakapokutana na Argentina katika mechi ya fainali ya kombe la dunia siku ya jumapili.
Muller amefurahia michuano ya mwaka huu ya kombe la dunia kwa kufunga magoli matano  katika mechi tano alizocheza mpaka sasa na magoli kama hayo yalimfanya abebe kiatu cha dhahabu nchini Afrika kusini mwaka 2010.
Nyota huyo wa Bayern Munich alisema yeye na wachezaji wenzake watafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanatwaa kombe la dunia kwa mara ya kwanza ikiwa imepita miaka 24.
“Itakuwa muhimu sana kucheza kwa juhudi kubwa, hususani kujilinda. Unatakiwa kuwa makini kumlinda Lionel Messi”.
“Tumecheza dhidi ya Messi  mara kadhaa. Sijawahi kufungwa mchezo wa mashindano na yeye”.
“Hatujawahi kwenda Rio de Janeiro, bado kwangu mimi sababu pekee ya kwenda pale ni kushinda kombe la dunia”.
Ujerumani iliifunga Brazil mabao 7-1 katika mechi ya nusu fainali, lakini Muller anaamini mechi ya jumapili Maracana itakuwa ngumu na kipimo kizuri kwa kikosi cha Joachim Loew.
“Sijui mechi itakuwaje siku ya jumapili, lakini sitarajii kama itakuwa 5-0 kwa kipindi cha kwanza,” alisema.
“Inaweza kuwa nzuri, labda itakuwa ngumu kama ilivyokuwa dhidi ya Algeria au Ufaransa”.
“Tutafanya kila linalowezekana ili kushinda kombe la dunia”.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates