Marekani imefunga ubalozi wake wa Libya kwa muda na wafanyakazi wake
wote wamehamishiwa nchi jirani, Tunisia.
Walipelekwa huko kwa magari huku wakilindwa na ndege za Marekani.
Jengo la ubalozi wa Marekani mjini Tripoli liko katika eneo ambalo limeathirika na mapambano kati ya makundi ya wapiganaji yanayozozana, ambayo yamekuwa yakigombania kudhibiti uwanja wa ndege wa kimataifa wa Libya.Wizara ya mashauri ya nchi za nje ya Marekani piya imewasihi raia wote wa Marekani waondoke nchini humo.
Waziri wa mashauri ya nchi za nje, John Kerry, alisema kulikuwa na hatari hasa ikiwakabili wafanyakazi wa ubalozi huo, lakini alisisitiza kuwa shughuli za ubalozi zinasimamishwa kwa muda tu.
Miaka miwili iliyopita balozi wa Marekani aliuwawa pale ofisi ndogo ya ubalozi wa Marekani katika mji wa Benghazi, mashariki mwa Libya, iliposhambuliwa na wapiganaji Waislamu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni