Dole juu: Luis Suarez amekamilisha uhamisho wake na kujiunga na Barcelona akitokea Liverpool.
Rasmi, Luis Suarez ameondoka Liverpool na kujiunga na FC Barcelona kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 75.
Mazungumzo yalianza wiki iliyopita na yamefikia tamati baada ya Wakalunya kukubali kulipa dau linaloaminika kuwa paundi milioni 75 ili kuinasa saini ya mshambuliaji huyo wa Uruguay.
Awali mazungumzo juu ya namna ya kuilipa Liverpool yalikuwa yanaendelea ambapo majogoo wa jiji walikuwa wanavutiwa na mshambuliaji wa Barcelona, Alexis Sanchez na walitaka kumjumuisha katika dau hilo.
Lakini kitendo cha Sanchez kusaini Asernal hapo jana kunamaanisha sasa Barcelona watalipa pesa taslimu.
Sasa mambo yamewekwa hadharani na dau linafahamika, huku Suarez akitarajiwa kutambulishwa rasmi kama mchezaji wa Barca wiki ijayo.
Suarez alisema siku zote ilikuwa ndoto na nia yake ya kucheza Hispania na amewataka mashabiki kuelewa maamuzi yake,
“Kwa moyo mgumu naondoka Liverpool kwenda kuanza maisha mapya na changamoto mpya Hispania. Mimi na familia yangu tumeipenda klabu hii na mji wake”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni