Social Icons

Jumatano, 25 Juni 2014

Msekwa: Hatuhitaji Katiba Mpya

Spika mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa akikusanya baadhi ya vitabu alivyoviandika alipokuwa akifanya mahojiano na wahariri wa gazeti hili nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha na Mpoki Bukuku

Dar es Salaam.  Spika mstaafu, Pius Msekwa amesema haoni haja wala sababu ya msingi ya Tanzania kuandika Katiba Mpya kwa sasa kwani hakuna matukio makubwa ya kisiasa nchini yanayolazimisha kufanya hivyo.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam jana, Msekwa alisema hata hivyo, anakubaliana na uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kuruhusu kufanyika kwa mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu alikuwa na sababu zake na alikwishazieleza wazi.
Alisema, “Sioni haja ya kuwa na Katiba Mpya. Mnatunga Katiba Mpya kama kuna mabadiliko makubwa ya kisiasa, yaani mabadiliko ya kiutawala,” alisema.
Alifafanua Katiba ya Tanganyika na hata ya Tanzania ilibadilishwa pale palipokuwa na matukio makubwa ya kiutawala, lakini pia kuna matukio mengine ambayo hayakulazimisha kuandikwa upya kwa Katiba.
Msekwa aliyeshiriki michakato yote ya katiba zilizotangulia ikiwamo hii ya sasa, alisema kwa kawaida Katiba Mpya inaweza kuandikwa panapokuwa na mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini kama ilivyotokea mwaka 1962 baada ya Tanganyika kupata uhuru wake, lakini Malkia wa Uingereza akaendelea kuwa mkuu wa nchi.
“Katika mazingira hayo Watanzania hawakujua maana ya uhuru ni nini, ikaleta sintofahamu, ikabidi Mwalimu (Julius Nyerere) na wenzake waamue kufanya mabadiliko makubwa ya kisiasa kutoka kuwa chini ya Malkia kwenda kwa uongozi wa wananchi,’’ alisema.
Pia, alieleza kuwa kuanzishwa kwa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilikuwa tukio jingine kubwa na la msingi lililosababisha kuandikwa kwa Katiba Mpya ya mwaka 1977.
“Mfano wa pili tulipoingia katika Muungano mwaka 1964, hapa kulikuwa na nchi mbili ambazo ni sovereignty (nchi zenye utawala kamili) tukaziunganisha, mazingira kama hayo yalidai Katiba Mpya.
Hata hivyo, Msekwa alisema hata mabadiliko kama ya mwaka 1965 kutoka mfumo wa vyama vingi vya siasa kuingia chama kimoja licha ya kuwa tukio kubwa, hayakulazimisha kuandikwa kwa Katiba Mpya, bali iliyokuwepo ilifanyiwa marekebisho.
Alisema tukio jingine ni la mwaka 1984 ambako mabadiliko mengine yalifanyika katika Katiba kwa kuingiza kipengele cha haki za binadamu na ukomo wa kipindi cha urais kuwa wa vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja ambalo halikuhitaji Katiba Mpya.
Badiliko jingine kubwa ambalo halihitaji katiba mpya, Msekwa alisema ni lile la mwaka 1992 la kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini … “Tuliporejea mfumo wa vyama vingi hatukutunga katiba kwa kuwa haikuwa lazima. Unaondoa vile vifungu vinavyoondoa chama kimoja na vingine vinaendelea kama kawaida.
Kwa hiyo hata sasa hakuna haja ya kuandika Katiba Mpya, kitu chochote kinachotakiwa kingeweza kuingizwa katika Katiba iliyopo.
Mchakato wa Katiba
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea nchini, mwanasiasa huyo ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwamo za ukatibu wa Bunge, Katibu Mkuu wa CCM na Makamu Mwenyekiti wa CCM, alisema tofauti zinazojitokeza nchini wakati huu zina sababu.
“Kwa wengine, mchakato wa Katiba Mpya umekuwa ni ajenda yao. Kwa mfano, Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2010 walishaweka wazi kuwa wangeandika katiba mpya ndani ya siku 100 wakiwa madarakani. Wanaamini Rais Kikwete kakwapua ajenda yao, hivyo hawakufurahishwa kuona ajenda hiyo imechukuliwa na kutekelezwa na CCM.
“Hii ndiyo sababu ya misimamo mikali, ikiwamo ile inayojitokeza kwa sasa kwenye Bunge Maalumu la Katiba,” alisema.
“Ni vyema mjadala uachwe uendelee kwa masilahi ya wananchi, kwanza unawafanya Watanzania wajue maana ya Katiba.
Ni sahihi waachwe wajadili Katiba wanayoitaka, kwani wengi wameweza kuelewa kuwa inahusu maisha yao, zamani nani aliijua?” alihoji.
Mfumo wa Serikali
Akizungumzia mfumo upi wa Serikali unaofaa Tanzania kutokana na mijadala inayokinzana kwenye Bunge Maalumu la Katiba, Msekwa alisema hana chaguo wala hajali iwapo ni Serikali mbili, tatu au moja.
“Sina choice (chaguo) wala sijali kwa sababu uimara wa Muungano unatokana na utashi wa kisiasa wa viongozi wakuu wa nchi, wala si idadi ya Serikali,” alisema.
Katika suala la utashi wa kisiasa, Msekwa alisema umekosekana kwa pande zote mbili za Muungano, jambo ambalo linahatarisha uhai wake.
“Kwa upande wa Zanzibar, utashi wa kisiasa umekosekana, ipo mifano ya kauli kama za Maalim Seif Shariff Hamad anayesema hadharani kwamba tunahitaji Muungano wa mkataba.
“Kukosekana huku kwa utashi wa kisiasa nchini kunaweza kuvunja Muungano,” alisema na kuongeza kuwa ndani ya CCM pia wapo ambao hawana utashi huo.
“Kwa mfano, kuibuka kwa kundi la wabunge 55, maarufu G55 ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1993 ni matokeo ya ukosefu wa utashi huo wa kisiasa.
“Hasira zao (wabunge hao wa G55) ziliamshwa na uamuzi wa Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu ya OIC,” alisema Msekwa na kuongeza kuwa walihisi kuwa ungezuka mgogoro mkubwa wa kikatiba nchini ndipo wao wakaibuka na hoja ya kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika.
MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates