Social Icons

Alhamisi, 5 Juni 2014

Mwenge wapata ajali, polisi watatu wajeruhiwa


Singida. Askari polisi watatu kati ya watano, wameumia vibaya baada ya gari walilokuwa wakisindikizia Mwenge wa Uhuru kupata ajali mkoani Singida huku waandishi wa habari na wapigapicha wakinyang’anywa vitendea kazi na kiongozi wa Mbio za Mwenge, Rachel Steven.
Kitendo hicho kilielezwa kuwa ni kuwazuia waandishi wa habari kutuma taarifa za ajali hiyo kwenye vyombo vyao vya habari. Mzozo mkali uliibuka kwa waandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kituo cha Televisheni cha ITV na Redio One na mwandishi wa Redio Standard waliokuwa kwenye msafara huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, (SACP), Geofrey Kamwela alipotafutwa ili aelezee tukio, alisema hana taarifa kamili na kutaka apewe muda ili afutilie suala hilo aeleze ajali hiyo. Hata hivyo baadaye alipotafutwa jioni alipotafutwa alisema kuwa atatolea taarifa suala hilo leo.
Ajali hiyo iliyohusisha magari matatu ilitokea katika Kijiji cha Kirumbi, Wilaya ya Sikonge, mpakani mwa mikoa ya Tabora na Singida ikiwa ni siku ya kwanza ya mbio za Mwenge huo ulioingia mkoani Singida ukitokea Mkoa wa Mbeya.
Mashuhuda wa ajali hiyo, walisema kuwa ilitokea muda mfupi baada ya Mwenge kupokewa katika Kijiji cha Rungwa kilichopo Kata na Tarafa ya Itigi. Ilielezwa kuwa gari moja la polisi lililokuwa kwenye msafara lilipasuka gurudumu na kusimama pembeni mwa barabara.
Gari jingine la polisi lililokuwa kwenye msafara lilisimama ghafla kutaka kufahamu kilichowapata wenzao, ndipo gari la Ofisi ya Afya ya Mkoa likiwa na wahudumu wa afya, lililigonga kwa nyuma gari hilo.
Kwa kuwa kila gari lilikuwa kwenye mwendo wa kasi ili kuendana na gari la Mwenge lililokuwa limetangulia, gari jingine lililokuwa na askari waliokuwa wamening’inia juu nalo lililigonga gari hilo la afya kwa nyuma na kusababisha askari hao kuumia.
Katika tukio hilo, hakuna hata mmoja kati ya wahudumu wa afya aliyeumia, lakini ajali hiyo ilisababisha askari mmoja kuvunjika mguu, mwingine kuvunjika mkono huku wawili hali zao zikiwa nzuri na mwingine alikuwa mahututi.
Baada ya tukio hilo, waliwahishwa kwenye Hospitali ya Misheni ya St. Gasper iliyopo Itigi kwa matibabu zaidi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates