Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Philip Mangula
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamempuuza Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula, ya kutafuta mwafaka ili warejee katika Bunge Maalum la Katiba.
Juni 10, mwaka huu, Mangula alizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kama Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha cha Demokrasia Tanzania (TCD) na kueleza kuwa kituo hicho kitaandaa mkutano wa faragha kwa viongozi wa vyama vya siasa na kuwaalika watu mashuhuri ili kutafakari hali na mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba na kutafuta suluhu kabla halijaingia awamu ya pili ya majadiliano Agosti 5, mwaka huu.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kauli ya Mangula hawaitambui kwa kuwa ilitakiwa kutolewa na Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo, kusisitiza msimamo wa Ukawa kuwa hawatakuwa tayari kurejea bungeni ikiwa rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Warioba itajadiliwa kama ilivyo bila kubadilishwa.
Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, alisema kauli iliyotolewa na Mangula Ukawa hawaitambui kwa kuwa ameingilia majukumu ambayo hayamhusu na kuongeza kuwa kitakachowashawishi kurudi bungeni ni kujadiliwa maoni yaliyotolewa na wananchi kwa Tume ya Jaji Warioba ambayo yanapendekeza muundo wa serikali tatu.
“Tunashangaa kuona mtu anaingilia jukumu la mwenyekiti, TCD ina kanuni na sheria zinazoiongoza, tutarudi kuendelea na mjadala mpaka wabunge wa CCM watakapoheshimu maoni ya wananchi yaliyopendekezwa kwa Tume ya Warioba,” alisema Profesa Lipumba.
“Wana-Ukawa ni waelewa sana, hawataki kudharau wananchi kwa kile walichokipendeza katika mikoa mbalimbali, tukikubali kurejea tutakuwa tunakiuka haki ya msingi ya kuheshimu maoni ambayo kwa kiasi kikubwa yanalenga kuleta mabadiliko makubwa,” aliongeza Profesa Lipumba.
Aliongeza kuwa kinachotakiwa rasimu iliyowasilishwa na Warioba ijadiliwe bungeni na baada ya wabunge kuchangia na baadaye ipelekwe kwa wananchi waamue ni muundo gani wa Muungano wanaoutaka.
Bunge hilo lilikumbwa na mgawanyiko Aprili 16, mwaka huu baada ya wajumbe wa Ukawa inayoundwa na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kususia kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wake ambao waliulalamikia wakisema kuna ubaguzi na uchakachuaji wa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba.
Bunge hilo lililoanza Aprili 18, mwaka huu hadi Aprili 25 lilipoahirishwa, lilijadili sura mbili tu ya Kwanza na ya sita ambazo zinazungumzia jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wa Muungano.
Ukawa wanataka jina liwe shirikisho na serikali tatu wakati CCM wanataka jina la Jamhuri ya Muungano na serikali mbili.
Hata hivyo, Cheyo alipoulizwa, alisema katiba ya TCD inaruhusu makamu mwenyekiti kuzunguzia jambo lilote pale mwenyekiti anapokuwa na majukumu na kueleza kuwa siku hiyo yeye (Cheyo) alikuwa katika vikao kamati ya Bunge.
LISSU AWAPA ANGALIZO WASULUHISHI
Wakati huo huo; Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema viongozi wa dini na wanasiasa wanaosuluhisha Ukawa kurudi bungeni watambue sababu zilizowatoa bungeni ndipo wajumbe wake watarudi bungeni na kujadili maoni ya wananchi.
Lissu alisema kitakachowakomboa wananchi ni kuunga mkono rasimu ya Jaji Warioba ambayo ndio maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya.
Hata hivyo, amesema CCM hawataki huku na kwamba kutokana na kutokubali kwao, vyama upinzani vimeamua kushirikiana ili kuwaeleza wananchi kuhusu mwenendo wa Bunge hilo.
Lissu aliyasema hayo wakati akiwahutubia wakazi wa Jimbo la Iringa katika soko la Kihesa.
“Sisi vyama vya upinzani tuliamua kuondoka bungeni kwa sababu kungeendelea kukaa kule bungeni na kuendelea kujadili Katiba mpya mwisho wa siku CCM wangepitisha na kusema kuwa haya yote tuliyajadili na vyama vyote vya upinzani vikiwemo, lakini sisi kama Ukawa tuliondoka na kama wanataka turudi bungeni na kuendelea kujadili kuhusu katiba hiyo wakubali maoni ya Jaji Warioba na siyo ya CCM.
Alisema baada ya vyama vya upinzani kuunda Ukawa, kumezuka maneno mengi ya propaganda kutoka chama tawala yanayojaribu kuwakatisha tamaa wananchi, akifafanua kuwa propaganda hizo ni hofu ya CCM kuogopa muungano wa wapinzani.
“Siku zote mtu mkweli huwa anapigwa mawe kwanini, kila kinachosemwa na Ukawa wanapinga na tunayojadili ni ya msingi na yenye tija kwa taifa, lakini jambo la CCM hata kama sio la msingi linapitishwa, sisi Ukawa hatutakubali kabisa,” alisema Lissu. Imeandikwa na Hussein Ndubikile, George Tarimo na Sanula Athanas.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni