Social Icons

Alhamisi, 5 Juni 2014

UDA yavua nguo wabunge wa CCM

Vita ya umiliki wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) iimeendelea kugubika Bunge, safari hii wabunge wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakishambuliana kuhongwa na pande mbili zinazogombea kumilikishwa shirika hilo.


Hali ilikuwa ya kuvuana nguo kati ya Mbunge wa Urambo Magharibi (CCM), Profesa Athuman Kapuya na Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas Mtemvu, kila mmoja akimtuhumu mwenzake kuhongwa ili kufanikisha umilikishwaji wa shirika hilo kongwe, ambalo sasa hivi linaendeshwa na Kampuni ya Simon Group.

Mapambano hayo ya maneno makali yaliibuka wakati wabunge wakijadili hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha na Uchumi ya mwaka 2014/15.

Mtemvu alianza moja kwa moja kutoa mchango wake kwa kuzungumzia sakata la Uda akimtuhumu Profesa Kapuya kuwa ndiye mmoja wapo waliouza shirika hilo bila kuhusisha wadau wa Dar es Salaam.

Alimtaja mwingine aliyehusika na uuzaji huo kuwa ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, ambaye alichukua Uda na kuwapa Simon Group.

“Mimi naanza moja kwa moja kwenye hoja ya Uda, mimi ni mdau wa Uda, ni kijana niliyezaliwa Dar es Salaam, kwa hiyo nimepanda Uda nikiwa mdogo naijua Uda tangu ikiwa DMT (Dar es Salaam Motor Transport). Mimi sikurupuki tu kama wengine wanavyofanya kuhusu suala hilo, ” alisema.

“Mimi niwaombe wabunge waangalie ripoti ya CAG ya mwaka huu ukurasa wa 39, itawasidia taarifa hii. Lakini Dar hatujapinga hata mara moja shirika la Uda kubinafsishwa, lakini humu ndani kuna mjumbe wa bodi ya Uda anayezunguka zunguka humu ndani, hiki siyo kitendo kizuri hata kidogo,” alisema.

Baada ya kauli hiyo, wabunge walisikika wakitaka Mtemvu amtaje mjumbe huyo naye alimtaja kuwa ni Kapuya.

Mtemvu alisema mwekezaji anayetajwa alilipa Shilingi milioni 280 na kuhoji hiyo ndiyo thamani ya Uda? Na kwamba shirika hilo hakukabidhiwa na vikao halali bali na Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

“Tunapoongea tusiangalie sambusa za Dodoma hoteli, tuangalie thamani ya shirika lenyewe, tunauza mali ya serikali bila baraza la mawaziri? Tunaweza kuuza mali ya serikali kutumia kamati ya Tamiseni ambaye mwenyekiti wake anafanya biashara ya pamba,” alihoji.

Alisema utafutwe ukweli na haki badala ya kutafuta dhuluma. Alisema Simon Group uwezo hana, na baada ya kauli hiyo, Profesa Kapuya aliingilia kati kwa kutaka kutoa taarifa ambapo, Naibu Spika, Job Ndugai, alimruhusu.

Katika taarifa yake, Profea Kapuya alisema: “Hakuna dhambi kwa mbunge kufanya biashara, sera inaruhusu na afadhali mimi ninayezunguka kuwaona watu kuliko yeye anayezunguka kwa lengo la kurudisha imprest (masurufu), na anayezungumza ni mmoja wapo.”

Alisema hakuna mali ya serikali iliyouzwa bila Baraza la Mawaziri, bali iliyouzwa ni hisa ya jiji kwa kushirikisha vikao vyote na kuongeza kuwa hisa za serikali zipo salama.

Mjumbe anayelalamika alihusika katika vikao vya kufikia maamuzi ya uuzaji wa Uda na posho alichukua. Profesa Kapuya pia alisema kwa nini Mtemvu hakuzungumza suala hilo Dar es Salaam anakimbilia bungeni.

Hata hivyo, Mtemvu alikataa kupokea taarifa hiyo ya Profesa Kapuya, na kusema alitumia uwaziri wake kupata mali isivyo halali na kwamba Uda imeuzwa kwa mnada Februari 24, mwaka huu kwa kampuni moja ya Al-jazeera na kuhoji hayo yalisemwa bungeni au wanataka yasemwe na mengine.

Alisema Uda imeuzwa kwa dhuluma bila utaratibu wa kuwepo kwa vikao.

Alisema ndiyo maana wanaDar es Salaam hawaoni wakizunguka kwa kuweka vikao Dodoma hoteli kuhonga wajumbe “au unataka ushahidi wa kamera,”alihoji.

“Acheni mmeifanya Dar es Salaam ni ya kuchuma, mbunge usiyekuwa wa Dar, unaijua Dar es Salaam, sisi tunajua mambo yetu wenyewe,” alisema.
Mapema, Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Philikunjombe, alisema sakata la Uda liliibuliwa na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (PAC) na akataka suala hilo liachiwe kamati ishughulikie.

Naye Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, aliitaka serikali itoe maelezo ya kina kuhusu uuzaji na umiliki wa hisa za Uda.

Alisema pendekezo hilo linatokana na utata wa uuzwaji na umiliki wa hisa kati ya serikali na mwekezaji katika shirika hilo na kwamba utata huo bado unaendelea kujitokeza.

“Ni vyema serikali ikaendelea kuheshimu na kutekeleza maazimio yaliyopendekezwa na kamati ya bunge ya Tamisemi, mwaka jana na kuridhiwa na bunge hili tukufu,” alisema.

Akijibu hoja ya Uda, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, alisema chokochoko yote ya Uda aliianzisha yeye alipotoa majibu bungeni juu ya swali kuhusu umiliki wa Uda.

Alisema alijibu kuwa serikali inamiliki hisa asilimia 49 na Jiji la Dar es Salaam lina hisa 51, hicho ndicho anachokijua.
Alisema kama kuna jambo lolote limetokea kwamba serikali haina hisa, alitafuta kama kuna azimio lilitolewa na Baraza la Mawaziri na hakulikuta, kama limeuzwa basi limeuzwa kinyemela.

“Mimi kama Adamu Kigoma Malima, nataka Uda ipate mwekezaji ambaye anaendana na hadhi ya Jiji la Dar es Salaam, lakini huyo mwekezaji afuate utaratibu,” alisema.

Malima aliongeza kuwa Jumatatu wiki hii alimuita mmiliki wa Simon Group na kumtaka aonyeshe uhalali wa hisa za Uda anazomiliki, lakini hakuonyesha karatasi yoyote kuhalalisha umiliki wa shirika hilo.

“Nimetafuta sijaona ridhaa ya baraza la mawaziri…sina taarifa juu ya uuzaji wa Uda. Hisa za serikali hazitolewi kama sambusa,” alisisitiza Malima na kuongeza:

“Kama ana ushahidi alete ofisini…aweke karatasi mezani.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates