Social Icons

Ijumaa, 27 Juni 2014

Mnyika:Waasi Chadema wamehongwa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema watu wanaojiita wanachama wa chama hicho wakiendesha uasi, wanapewa fedha na chama kimoja kikubwa nchini ambacho hakimo ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).


Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika, katika mkutano na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, madai yaå kundi la watu waliojiita kuwa ni wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho hayana ukweli wowote na kuwa watu hao wanatumika kisiasa.

“Tunawajua na tunaelewa njama na mipango yao yote, lakini kwa leo siwezi kuwataja kwa sababu nikiwataja ndio mtakaowafanya habari kubwa na wenyewe watarudi kutushambulia kuwa hatukujibu hoja, lakini katika muda mwafaka ipo siku tutawataja hivyo kwa leo ngoja niishie kujibu hoja za msingi,” alisema Mnyika.

Alisema viongozi na chama hakijavunja katiba yake kwa kujiunga kushirikiana na vyama vingine vya siasa kuanzisha Ukawa.

Aidha, Mnyika alisema kuwa tuhuma zilizotolewa na watu hao kuhusu ubadhirifu wa fedha ndani ya Chadema siyo za kweli kwa kuwa hesabu za fedha za Chadema zimekwisha kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na taarifa yake kupelekwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Akizungumzia tuhuma kuwa viongozi wa Chadema wanavunja katiba kwa kujiunga na Ukawa, Mnyika alisema kuwa Ukawa siyo chama cha siasa bali ni umoja wenye lengo la kuleta mshikamano mzuri na vyama vingine na kwamba katiba ya Chadema inaruhusu chama hicho kuwa na uhusiano mzuri na vyama vingine vya siasa.

“Chama hiki kinaongozwa na katiba na kwa kweli hakuna kifungu chochote kwenye katiba kilichovunjwa kwenye uamuzi wa chama kuanzisha ushirikiano na vyama vingine vya siasa na makundi mbalimbali katika kile kinachoitwa Umoja wa Katiba ya wananchi yaani Ukawa,” alisema Mnyika.

Alisema kuwa katiba ya Chadema imeaninisha utaratibu wa chama kushirikiana na vyama vingine katika nyanja tatu ambazo ni ushirikiano wa kuunganisha vyama ili kuwa na chama kimoja cha siasa, ushirikiano wa kufanya miradi ya pamoja na ushirikiano wa kushirikiana katika shuguli za kisiasa.

Alisema kuwa Ukawa siyo chama cha siasa hivyo kwa kujiunga na Umoja huo Chadema haijavunja katiba yake, bali wanaosema kuwa imekosea kwa mujibu wa katiba yake kujiunga na Ukawa ni kwa sababu tu hawaijui katiba ya chama hicho.

Mnyika alisema kuwa ushirikiano kwenye uchaguzi ambao watu hao wameurejea kwenye mazungumzo yao kwa kutamka kwamba Chadema inakusudia kushirikiana na vyama vingine kwenda kusimamisha mgombea mmoja, wakisema kuwa ni ukikwaji wa katiba pia siyo sahihi.

Alisema kuwa chama kinayo haki ya kikatiba ya kushirikiana na vyama vingine kwa kuweka mipango mbalimbali ya kimaendeleo ikiwamo ushirikiano wakati wa uchaguzi.

Alisema kuwa uamuzi wa chama kuacha kuteua mgombea kupisha chama kingine au chama kuachiwa na chama kingine unakamilika wakati wa uchaguzi na kuwa kabla ya hapo ni maamuzi ya matazamio na mipango tu.

Alisema kuwa jambo hilo siyo geni kwani mwaka 2007 Chadema ilisaini tamko la ushirikiano wa vyama vya siasa vya CUF, TLP, Chadema na NCCR na kuwa kama wanaopinga uamuzi huo wangekuwa ni wanachama hai wa Chadema, wangepinga tangu wakati huo.

Akizungumzia suala la ubadhirifu wa fedha ambalo limeibuliwa na watu hao waliojiita wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema, Mnyika alisema kuwa madai yao hayana ukweli wowote kwa kuwa hesabu zote za fedha za Chadema tayari zimekwishakaguliwa na CAG na taarifa yake kupelekwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Mnyika alimtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kutoa taarifa za fedha za vyama vyote vya siasa ambavyo tayari vimekwishakaguliwa ili ukweli juu ya suala hilo pia ujulikane kwa umma wa Watanzania.

“Mimi kama msemaji wa Chadema nitoe wito kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, kuweka wazi ripoti za vyama vyote vya siasa alivyovikaguka kwa umma ili ukweli ujulikane,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema kuwa Chadema kama taasisi siyo chama cha ufisadi na ubadhirifu na kuwa chama hicho hakiwezi kuvumilia ufisadi wa aina yoyote wa ndani au wa nje ya chama na kwamba chama hicho ndicho kilichotaka sheria ibadilishwe ili CAG aanze kukagua hesabu za vyama vya siasa.

NJAMA ZA HUJUMA
Baada ya kujibu hoja hizo, Mnyika aliwageukia watu walioanzisha madai hayo akisema kuwa wengi wao siyo wanachama wa Chadema, baadhi yao ni wale ambao tayari walishafukuzwa uanachama na wachache ambao ni wanachama halali wa Chadema aliwaita kuwa ni wasaliti.

Alisema kuwa licha ya watu hao kudai kwamba wako 82, lakini waliojiorodhesha kwenye nyaraka alizozipata ni watu 32 pekee na baada ya kuchunguza majina hayo imebainika kuwa zaidi ya watu 10 wamegushiwa saini zao.

Mnyika alisema kuwa uchunguzi uliofanywa na umebaini kuwa watu hao wametumwa na kufadhiliwa na chama kimoja cha upinzani ambacho hakimo kwenye Ukawa kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa juu serikalini.

Alisema kuwa chama hicho pamoja na viongozi wa Serikali waliojihusisha na mpango huo wa kukichafua Chadema wanawafahamu kwa majina pamoja na kiasi cha fedha walichopewa kuwezesha mpango huo.

BARAZA KUU KUKUTANA JULAI
Mbali na kujibu hoja hizo, Mnyika alisema kuwa kati ya Julai 18, mwaka huu chama hicho kitafanya mkutano wake wa Baraza Kuu Taifa kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya chama hicho.

Aidha alisema kuwa chama hicho kinaendelea na uchaguzi wake wa ndani katika ngazi mbalimbali na kwamba kabla ya kuadhimisha siku ya mafisadi, Septemba 15, mwaka huu watakuwa wamekamilisha uchaguzi wa ndani hadi ngazi ya taifa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates