*Geneviveve Nnaji na John Dumelo nao ndani
*Habib Koite, Didier Awadi kuburudisha
*Filamu ya Mandela kufungua pazia
Mkurugenzi Mkuu wa ZIFF, Profesa Martin Mhando (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kuzindua rasmi Tamasha la Filamu la nchi za Majahazi la 17 maarufu kama Zanzibar International Film Festival (ZIFF). Kulia Msaidizi wa Kitengo cha habari ZIFF, Lara Prieston, Kushoto ni Meneja wa Tamasha la ZIFF, Daniel Nyalusi (Dean), Afisa Mawasiliano wa ZIFF, Hassan Musa "Has T" (wa pili kushoto) na Music Coordinator wa ZIFF, Edward Lusala (katikati). Picha na Zainul Mzige wa modewjiblog
Na Andrew Chale
DUNIA inatarajia kushuhudia tukio kubwa na la kihistoria ndani ya viunga vya Ngome Kongwe ndani Mji Mkongwe wa Stone Town, Unguja, kwa watu wa mataifa yote watakapoungana na kushuhudia ‘Hatma ya Pamoja’ (A common Destiny) Juni 14 hadi 22, 2014, katika Tamasha la Kimataifa la filamu la Zanzibar (ZIFF).
Tamasha hilo maarufu kama filamu la nchi za Majahazi ZIFF, kwa mwaka huu linatarajiwa kufanyika kwa mara ya 17, tokea kuanzishwa kwake.
Akizungumza mapema leo jijini Dar es Salaam, kwenye halfa maalum ya uzinduzi wa tamasha hilo la 17, kwa wandishi wa habari iliyofanyika Goethe Institut kituo cha utamaduni, Mkurugenzi Mkuu wa tamasha hilo, Profesa Martin Mhando, alisema tamasha hilo msimu wa mwaka huu linatarajiwa kuwa moto kwani linakuja na mambo mbalimbali yenye kuleta mabadiliko ya hali ya juu.
Ni kutokana na mabadiliko hayo, Profesa Mhando anasema tasnia ya filamu kwa Tanzania inahitaji kubadilika ikiwemo wasanii wenyewe kujituma na hata kuingia darasani ili kufanya kazi zenye uhakika.
Akimaanisha kila msanii wa filamu aweze kufikia malengo yake, hana budi kujifunza na kushirikisha wale waliotangulia katika tasnia hiyo.
Anazungumziaje kaulimbiu ya ‘A Common Destiny’
Prof. Mhando amesema kauli mbiu ya mwaka huu yenye kusema Hatma ya pamoja yenye maana ya ‘A common Destiny’, ina lengo la kuwakutanisha watu wa mataifa mbalimbali kuwa kitu kimoja na kufurahia kwa pamoja ikiwemo kubadilishana mawazo kwa pamoja kwa tasnia ya filamu, muziki, kwa mlengo ya kujenga.
“Tukiwa na haja moja, kuishi kwa amani na kuleta mapinduzi ya kiuchumi, kifikira na maendeleo kwa amani, ZIFF kwa kutumia dira hiyo hasa kupitia filamu zetu za ndani zenye mchanganyiko wa utamaduni na asili yetu.
“Wazanzibari na hata wageni watakaoshuhudia filamu hizi wataweza kuchukua utamaduni huo na kuupeleka nje kwa furaha kubwa katika kufikia hatma ya pamoja” amesema Prof. Mhando.
Music Coordinator wa ZIFF, Edward Lusala akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na wasanii watakaotoa burudani kwenye tamasha hilo.
Lupita Nyong’o, Genevieve ndani ya nyumba
Tukio kubwa ambalo kwa sasa Tanzania hasa kwenye viunga vya Zanzibar
na nchi nyingine duniani katika tamasha hilo la 17, ni ujio wa msanii wa Kenya na Mexico, Lupita Nyong’o, atakayeudhuria utoaji wa tuzo hizo za ZIFF mwaka huu.
Lupita ambaye ametwaa tuzo za Oscar na nyingine nyingi na kupelekea kutikisa Hollywood kwa sasa ni miongoni mwa mastaa watakaokuwa kwenye tamasha hilo huku akitarajiwa kuambatana na wazazi wake wote wawili pamoja na wadogo zake.
Prof. Mhando amesema tayari wazazi wote wawili wa Lupita akiwemo Dorothy na Peter Anyang’ Nyong’o, watakuwapo kwa siku zote 10 kwenye tamasha hilo huku Lupita mwenyewe akiahidi kuangalia uwezekano wa kuhudhuria japo katika utoaji wa tuzo kama ratiba za shughuli zake hazita mbana.
Prof. Mhando alisema Lupita ni zao la ZIFF na ndiyo iliyomfungulia mwanya wa kujulikana na baadaye alienda kusoma zaidi masuala hayo ya filamu, ambapo alishiriki ZIFF 2007 kama Volunteer.
Mara nyingi staa huyo amekua akihudhuria matamasha na halfa mbalimbali za utoaji wa tuzo na zawadi zingine huku akiwa ameambatana na wazazi wake wote wawili.
Lupita mbali na tuzo hiyo ya Oscar, kupitia filamu ya ‘12 Years a Slave’ pia filamu hiyo imempatia tuzo mbalimbali zikiwemo: tuzo ya Steve McQueen kama mwigizaji mwenye mvuto, mwigizaji bora wa kike aliyeshirikishwa, ‘Academy Award’, ‘Screen Actors’ Guild Award’, ‘NAACP Image Award’, ‘Independent Spirit Award’, ‘Broadcast Film Critics Association Award’, na nyingine nyingi.
Genevieve Nnaji.
Mbali na Lupita, katika kuongeza utamu wa tamasha hilo, mastaa wengine nguli wa Afrika kwa mwaka huu wanaotarajiwa kuwapo katika ushuhudiaji wa utoaji wa tuzo hizo ni pamoja na muigizaji na mwanamitindo nyota wa Nigeria, Genevieve Nnaji.
Wengine ni Amr Waked (Misri), Faouzi Bensaidi (Morocco), Nadia Buari, Richard Mote Damijo ‘RMD’, John Dumelo, Desmond Eliot na Florence Masebe.
Afisa Habari wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Fizza Moloo akizungumzia kuhusiana na Filamu iliyopewa jina la "Women with Altitude" iliyoandaliwa na WFP ambapo ndani yake imeshirikisha wanawake wa kitanzania watatu waliofanikiwa kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro wakiwa wameambatana na wenzao nane kutoka Nepal na kuzungumzia changamoto mbalimbali wakati wa kupata elimu na maisha kwa ujumla itakayoonyeshwa kwenye tamasha hilo tarehe 17/6/2014 saa 19:15 jioni ukumbi wa Old Fort visiwani Zanzibar.
Filamu ya Mandela kufungua pazia
Jumla ya filamu 79, kutoka mataifa mbalimbali zinatarajiwa kuonyeshwa huku filamu iliyoingia kwenye tuzo za Oscar, ya Mandela: ‘A Long Walk to Freedom’ ndiyo itakayofungua pazia kwenye tamasha hilo, Juni 14.
“Katika filamu hizo 79 za kimataifa zitaoneshwa ZIFF, nyingi zikiwa zinatoka katika nchi za Kiafrika na filamu ya Mandela imepata bahati ya kuwa ya ufunguzi”, amesema Profesa Mhando.
Pia Profesa Mhando amesema kuwa zitakuwepo filamu zinatoka katika nchi 35 zikiwemo filamu fupi 38, filamu ndefu za kuburudisha 24 na makala 17.
Meneja wa Tamasha la ZIFF, Daniel Nyalusi "Dean" akionyesha kitabu chenye ratiba nzima ya tamasha hilo litakalorindima visiwani Zanzibar kuanzia Juni 14 hadi 22 mwaka huu.
Burudani zitakazopamba
Kwa upande wake, Edward Lusala anayeshughulikia muziki kwenye tamasha hilo la 17, anasema kuwa, wamejiandaa kutoa burudani ya aina yake ambayo itaacha historia kwa mwaka huu.
Lusala amesema jumla ya makundi 18 yanatarajiwa kutumbuiza. Huku kwa wasanii gwiji wakiwemo pia Didier Awadi kutoka nchi ya Senegal na Habib Koite (Mali) wanatarajiwa kuja kuishika Zanzibar na viunga vyake.
“Wasanii Koite na Didier ni miongoni mwa wasanii wakubwa sana na wenye heshima kubwa hasa kwa muziki wao kwani wanapiga kimataifa hasa katika matamasha makubwa na wamekuwa wakipiga miziki ya kipekee. Hivyo watu wote watafurahia” amefafanua Lusala.
Ameongeza kuwa, wasanii wengine ni pamoja na Farid Kubanda ‘Fid Q’, Ambwene Yesaya ‘ Ay’, Sauti Soul, Mzungu Kichaa, Ras Inncent Nganyagwa, Grace Matata na wengine wengi ambao watatoka Tanzania.
Na kuongeza kuwa kwa sasa AY yupo nchini Malawi akijifua na moja bendi maarufu ya muziki wa Live ambapo anatajiwa kukaa jukwaani kwa zaidi ya lisaa limoja na nusu huku akiimbaLIVE.
Pia vikundi vya muziki nguli toka Tanzania, Egypt, Kenya, Uganda, Malawi na Afrika ya Kusini vitatumbuiza kila siku katika tamasha hilo.
Aidha, Lusala amesema kuwa, kwa mwaka huu wanatarajia kufanya ‘surprise’ kwa kumleta msanii mkubwa ambaye bado wapo kwenye mazungumzo na msanii huyo kutoka Afrika kusini.
Kwa upande wake Meneja wa tamasha hilo, Daniel Nyalusi amewataja wadhamini wa tamasha hilo ni pamoja mdhamini mkuu ZUKU Pay tv, huku wengine ni Ethiopian Airlines, Tanzania Media Fund TMF, ComNet, Cello, Air Uganda, Gina Din, FASTJET and United Petroleum. Wengine ni shirika la Rosa Luzemburg Foundation, Arterial Networking, Steps International, Azam marine, Prime Time Promotions, Goethe Institut na wengine wengi.
ZIFF moja kati ya matamasha ya filamu makubwa duniani hukutanisha wadau katika tasnia ya filamu. Wakiwemo waigizaji wa siku nyingi na maarufu, waongozaji, waigizaji wachanga na wanafunzi kutoka ulimwenguni kote
Meneja wa Biashara wa shirika la ndege la Fastjet, Jean Uku akizungumzia udhamini wao kwenye tamasha hilo ambapo wametoa tiketi za safari ya washiriki kutoka Afrika Kusini watakaoshiriki kwenye tamasha hilo.
Msanii wa Hip Hop, Harry Kaale kutoka kundi la One "The Incredible" akielezea namna watakavyotoa burudani na elimu kwa vijana kwenye tamasha hilo.
Msanii Mzungu Kichaa akiwashukuru ZIFF kwa kutoa nafasi kwa wazalendo kuonyesha vipaji vyao kwenye tamasha la ZIFF.
DJ maarufu Kahlil Jacobs-Fantauzzi kutoka Puerto rico akisisitiza kutoa burudani ya aina yake kwenye tamasha hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni