Ugonjwa wa kuanguka na kupiga kelele unaowakumba baadhi ya wasichana katika shule mbalimbali nchini, umetajwa kusababishwa na maambukizi ya hofu inayosababisha mwili kupata dalili za magonjwa yasiyokuwepo.
Mtaalamu wa saikolojia na theolojia, Mchungaji John Rowse kutoka taasisi ya The Uhakika Christian Education Trust Fund kutoka Mbeya, alisema hayo hivi karibuni baada ya kutembelea shule zinazopata tatizo hilo mara kwa mara na kuzungumza na wazazi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo.
Alisema kuna mambo kadhaa yanayochangia kujenga hofu hiyo ambayo mwili hujitayarisha kuambukizwa, ikiwemo vitisho vya maisha kwa wanafunzi vinavyotokana na mambo mbalimbali kama vile ugomvi na mabadiliko ambapo miili yao inahangaika kujihami.
Kwa mujibu wa Mchungaji huyo, upo uwezekano kuwa baadhi ya wanaoanguka, ni wasichana wanaonyanyaswa nyumbani, wengine wanafundishwa kujidharau na wengine wanabaguliwa na kufanyiwa unyanyapaa shuleni.
Sababu nyingine ya kuanguka kwa wasichana shuleni kwa mujibu wa Mchungaji Rowse, ni hofu wanayopewa wasichana hao na waganga wa kienyeji wanaotabiri au kupiga ramli, pamoja na wachungaji au wainjilisti wanaokemea mapepo huku wakiwashika kichwani, begani au kwenye shingo na kuwatetemesha wasichana hao.
Mchungaji Rowse alisisitiza kuwa dawa pekee ya kutibu ugonjwa huo, ni utulivu kwani wanafunzi hao hususani wasichana huambukizana kwa hofu hivyo matibabu yake ni kupunguza hofu na mawazo.
“Hofu hiyo kwa wasichana hao husababishwa kwa imani potofu, waganga wa kienyeji wanaotabiri au kupiga ramli ... waganga hawa wanapenda kujenga hofu ya uchawi, ili baadaye wajidai kwamba ni wao waliondoa laana na kuleta uponyaji.
“Dawa ya kusaidia kuzuia matukio hayo ni kuwa na mipango ya kupunguza msongo wa mawazo shuleni, hasa miongoni mwa wasichana,” alisema.
Mchungaji Rowse alipendekeza machifu na waganga wa jadi wasikaribishwe shuleni kuwaombea wasichana hao kwa kuwa watawaongezea hofu.
Pia alipendekeza wachungaji au wainjilisti wanaopenda kushika mtu kichwani, begani au kwenye shingo na kumtetemesha, wasikaribishwe shuleni kwa kuwa nao pia ni hatari.
“Hata wale wanaokemea mapepo kwa sauti kubwa na wakati wakifanya hivyo hupenda kumwangalia msichana kwa ukali jicho kwa jicho.
”Katika mazingira hayo, watoto watapata tena hofu na wakianguka tena watasema ni pepo, lakini sivyo. Afadhali mchungaji wa amani, amwombee kila mwanafunzi aliyekumbwa na ugonjwa huo kwa sauti ndogo tu na kwa upole na upendo na kumfariji na utulivu. Asitamke wazi neno lo lote juu ya mapepo,” alisisitiza.
Alishauri kuwa kila shule iwe na mwalimu au mshauri wa kike ambaye hatoi adhabu kwa wasichana, atakayepaswa kujenga urafiki nao na kuwa karibu nao, ili wamwamini na kumwelezea mateso yao ya maisha, nyumbani na shuleni.
Alisisitiza kuwa wanafunzi wa kike wapewe nafasi za kukutana katika vikundi, ili wajadiliane pamoja kuhusu mambo yoyote, pia walimu wajitahidi kumpa kila msichana nafasi ya kusikilizwa.
Alitoa mfano wa Shule ya Msingi Inyonga wilayani Mlele katika Mkoa wa Katavi, ambayo aliitembelea na kuzungumza wazazi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo.
Alisema baada ya shule hiyo kuanza kutekeleza ushauri huo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Casto Ismail, alimwambia kuwa kasi ya matukio imepungua.
“Mwalimu Mkuu huyo alinieleza kuwa wamekuwa na mitihani ya darasa ya saba, ambao kwa kawaida husababisha msongo wa mawazo kwa wanafunzi, lakini hakuna mwanafunzi wa darasa ya saba hata mmoja aliyeanguka wakati huo…katika madarasa mengine ni wachache walioanguka.
“Niliwaambia walimu wawe na uvumulivu. Mambo yatatulia kweli baada ya mabadiliko ya imani ya wazazi na jamii… lakini watalaamu bado wanashindwa kuelewa kwa nini hali hiyo inakutwa sana kwa wasichana na wanawake,” alisema Mchungaji Rowse.
Mwandishi alifika katika Shule ya Msingi Inyonga na kuzungumza na Mwalimu Ismail, ambaye alieleza kuwa ugonjwa huo ulidumu kwa zaidi ya miezi sita tangu ulipowakumba wasichana wanaosoma katika shule hiyo Novemba mwaka jana.
Alifafanua kwamba kasi ya kuanguka kwa wasichana hao shuleni hapo imepungua baada ya kuanza kufanyia kazi ushauri wa Mchungaji Rowse, aliyefika shuleni hapo na kuzungumza na wanafunzi. Pia alitoa semina kwa wanafunzi, walimu na wazazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni