1. Utangulizi
Katika
kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 - 22 Novemba 2013,
Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua nafasi
zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya chama
iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe
22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk
Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka
unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba waraka
uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama
ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu
kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo
si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya
chama. Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti
chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi
na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali
vyama.
Ninatambua
kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka
nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha
CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi
nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na
atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na
chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo
na kesho.
2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu
Zipo
tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama
na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. Tuhuma hizi zinalenga
kuonyesha kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili
kukihujumu chama changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama
ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.
- Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
- Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
- Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
- Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.
ii)
Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni
wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi
huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo
ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.
iii)
Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya
majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa
CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni
pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama
nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la
kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi
kwamba nilifanya jambo hili. Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama
na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama
kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila
uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.
iv)
Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama:
Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama
ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni
kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika
mikoa yote tuliyotembelea. Mwaka 2012 baada ya hoja ya mkonge bungeni
nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na operesheni kubwa
moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi. Operesheni hii
sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa
mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.
v) Tuhuma
kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama
hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG):
Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu
nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili
wajiandae. Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi
moja na CCM na nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa
yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na
ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:
- Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha
- Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.
vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao
Mtakumbuka
kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya
kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa
na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa
kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba hivi karibuni
Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni
unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma
ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo
kuhusu jambo hili:
- Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
- Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
- Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.
3. Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe
Hivi
karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi
ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu
chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu
ya CHADEMA. Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa
kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu
haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu
nililalamikia mambo matatu yafuatayo:
- Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
- Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.
4. Hitimisho
Ninatambua
kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na ningewazodoa watu
kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania. Natambua pia
kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa
hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi
magumu'. Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya
kuendelea kutumia suala hili katika harakati zao za kudhoofisha
mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani nchini mwetu.
Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote
nchini watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki
na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu.
Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.
Naomba
wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa.
Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi ili
tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania
wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
Kama
mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi
mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa
niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
Kinachoendelea
ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano
baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji
dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa
majitaka. Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji
uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni