Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye amemtaka Msajili
wa Vyama vya Siasa nchini kukifuta Chadema kwa madai kuwa, kimeshindwa
kusimamia katiba yake kwa kutofanya uchaguzi wa ndani zaidi ya miaka
zaidi ya kumi.
Nape alisema chama hicho kimejaa viongozi waongo,
wapenda vurugu na wanaotaka kuvuruga amani ya nchi kwa kisingizio cha
Katiba Mpya na kwamba, wamesahau katiba iliyopo imedumu kwa miaka 50 na haijawahi kuwagombanisha wananchi wala kuwavuruga.
Hata hivyo, jitihada za kumpata Mkurugenzi wa
Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika kuzungumzia tuhuma hizo jana jioni
kwa simu yake haikufanikiwa.
Akihutubia wakazi wa Manispaa ya Songea jana, Nape
alimtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kukiagiza chama hicho kufanya
mkutano wa uchaguzi haraka kikigoma akifute na kwamba, asipofanya hivyo
wao wataendelea kumsema na kumchukulia hatua.
Aliongeza CCM kilifanya uchaguzi wake 2012 na
kupata viongozi wapya, lakini Chadema imeshindwa kusimamia katiba yake
ambayo ilipeleka kwa msajili wa vyama na kuisajili kwa kuivunja wao
wenyewe kwa kuendesha chama isivyo.
Nape alisema chama hicho hakifai kuongoza nchi, kwani kimeshindwa kusimamia katiba yake na kuifuata hakiwezi kuongoza wananchi.
“Kwa sababu Msajili wa Siasa ni mlezi wa vyama
vyote vya siasa ikiwamo Chadema, namuomba akiagize chama hicho kifanye
uchaguzi kwani wao wanajiita wanademokrasia wakati wanashindwa kufuata
demokrasia kwa vitendo,” alisema Nape.
Kuhusu malalamiko ya wananchi, Nape alisema wananchi wamekuwa wakilalamikia utendaji mbovu wa viongozi wa Serikali na kwamba, yana msingi kwani inasikitisha licha ya Ruvuma kuwa ni mkoa unaolisha nchi, hakuna mawazili wa kilimo ambao wamefika mkoani hapa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni