Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome.
Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania
(Tec), ‘limeuponda’ uamuzi wa serikali wa kushusha viwango vya ufaulu
kwa mitihani ya kidato cha nne na sita, likisisitiza kuwa hatua hiyo ni
upungufu na ishara ya kuporomoka kwa siasa na ni kipimo
kitakachoitumbukiza elimu shimoni.
Kauli hiyo ya Tec, imekuja wakati serikali imetangaza rasmi kuanza
kutumika kwa mfumo mpya wa usahihishaji wa mitihani na upangaji wa
viwango vya madaraja ya ufaulu, uamuzi ambao hata hivyo, umelifuta
daraja sifuri, kuanzia mwakani.
Rais wa baraza hilo, Askofu Tarcius Ngalalekumtwa, akizungumza katika
mahafali ya sita ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu, Mwenge (Mwuce),
kilichopo Wilaya ya Moshi, mkoani
Kilimanjaro, alisema kitendo hicho
kinaishangaza dunia kutokana na wenye dhamana kubadili maneno katika
kushughulikia elimu na kwamba hali siyo nzuri katika sekta hiyo kwa
sababu 'hatutaki kutafuta ni wapi tulipojikwaa na kutufikisha hapo
tulipo.'
Mabadiliko hayo na utaratibu wa kuimarisha mfumo huo wa ufaulu, utaanza
kutumika katika kupanga matokeo ya kidato cha nne na sita kwa mwaka 2013/2014, wakati umma ukiwa bado unahoji kilicho nyuma ya pazia
juu ya matokeo ya aibu ya mwaka jana ya kidato cha nne baada ya asilimia
60 ya watahiniwa wote kupata daraja sifuri.
“Kufuta zero (sifuri), ni sawa na kuongeza zero nyingine kwa kuwa
utazalisha wengi wasio na sifa hata kama utabadili maneno na kuliita
daraja fulani; tunalitumbukiza taifa letu katika balaa. Hali si nzuri na
hatujui hali hiyo ilianza lini ingawa kuna mahali tulipita na
kujikwaa…huu ni upungufu na kuporomoka kwa siasa,” alisema Rais huyo.
Alienda mbali zaidi, akiitaka serikali kutazama upya suala la mikopo kwa
wanafunzi wanaodaihiliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini,
kutokana na vijana wengi kukosa mikopo hiyo kwa kisingizio cha kushindwa
kukidhi vigezo vya bodi ya mikopo ambayo imekuwa ikikabiliwa na
mapungufu kadhaa.
Awali, Mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi,
Awali, Mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi,
Askofu Isack Amani, akitoa nasaha zake katika
mahafali hayo, alisema taifa linapaswa kutafakari upya uamuzi huo kwa
kuwa watu wanaweza kufuta mawazo ya alama sifuri usoni lakini siyo
kichwani.
“Wakati Watanzania wanatafakari uamuzi huu wa serikali, naomba
nikuhakikishe, baba askofu Ngalalekumtwa (Rais wa Tec), kwamba maagizo
ya baraza lako kuhusu chuo hiki (Mwuce) kuwa chuo kikuu kamili,
menejimenti iko katika mchakato huo na tutakuita ukizindue mara baada ya
kupata hati ya ithibati toka Tume ya Vyuo Vikuu nchini yaani TCU,”
alisema Askofu Amani.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino
(Saut), cha Jijini Mwanza, Padri Pius Mgeni, akizungumzia mustakabali wa
elimu nchini kwa sasa, alisema kwamba hali ni mbaya katika baadhi ya
vyuo vya elimu ya juu kutokana na idara nyingi ikiwamo inayoshughulikia
lugha ya Kiswahili kuongozwa na wageni kutoka nje ya nchi kutokana na
wazawa kukosa sifa za kuongoza baadhi ya idara.
“Ukimsikia mtu anakuita wewe ni Mswahili usifikiri anakusifia unajua
Kiswahili, hapana; huyo anamaanisha wewe hujui na ni mtu wa
porojoporojo.
Hali ni mbaya vyuoni na hata pale kwangu idara ya Kiswahili
inaongozwa na Wakenya wakati sisi tunapiga blaa blaa. Tunalo tatizo kwa
sababu wasomi wanakimbizana na fedha badala ya kutoa mchango wao kwa
taifa,” alisema Padre Mgeni.
Hata hivyo, baadhi ya wahitimu wa chuo hicho waliozungumza na NIPASHE
kwa nyakati tofauti, walisema serikali imechukua uamuzi huo kisiasa ili
kuhakikisha inatimiza lengo lao la mpango wa matokeo makubwa sasa,
ambalo ni kuhakikisha matokeo ya ufaulu kwa mtihani wa kidato cha nne
mwaka huu unafikia asilimia 60 kutoka 33 ya mwaka jana.
Jumla ya wahitimu 447 walitunukiwa vyeti vya ngazi mbalimbali kwenye mahafali hayo.
Awali, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilikuwa likitumia alama A, B, C, D na F huku alama A ikianza na maksi wa asilimia 81-100, B=61-80, C=41-60, D=21-40 na F=0-20. Aidha kulikuwapo na madaraja ya I, II, III, IV na 0.
Awali, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilikuwa likitumia alama A, B, C, D na F huku alama A ikianza na maksi wa asilimia 81-100, B=61-80, C=41-60, D=21-40 na F=0-20. Aidha kulikuwapo na madaraja ya I, II, III, IV na 0.
Kwa mujibu ya mabadiliko hayo yaliyotangazwa wiki iliyopita na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome,
alama zitashuka ambapo alama A itakuwa ni (75-100),B+ (60-74), B
(50-59),C (40-49), D (30-39), E (20-29) na F (0-19).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni