MALKIA wa Nyuki ameandika barua ya kujiondoa kwenye Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Simba kutokana na kuchukizwa na migogoro.
Malkia ambaye jina lake halisi ni Rahma Al Kharusi, amethibitisha
hilo na kusema aliamua kufanya hivyo kutokana na kukerwa na migogoro
ndani ya kamati hiyo.
Akizungumza jana kutoka Oman, Malkia wa Nyuki alisema aliamua
kujiondoa kwa mambo mawili makubwa ambayo ni migogoro na kukosa nafasi.
“Baada ya kumueleza Rage kwamba nimefikia uamuzi huo, ameniomba
nibaki kwa kuwa ninahitajika Simba. Kanishauri kwamba niingie katika
upande wa baraza la wadhamini. Kwangu naona si mbaya, maana sitakuwa na
vikao vya mara kwa mara, lakini bado nasisitiza migogoro si sahihi,”
alisema.
“Kwani kama si kuteuliwa katika nafasi hii ya kusimamia mali za
Simba, basi nilikuwa nimeshajiondoa kabisa Simba hadi hapo hali itulie
maana sioni faida ya haya yaliyopo sasa.”
Malkia wa Nyuki, ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya
Udhamini ya Simba, ndiye alitoa zaidi ya Sh milioni 80, Simba ikaweka
kambi ya siku 15 jijini Muscat nchini Oman.
Lakini aliahidi kuanza kushughulikia kujenga uwanja kwa ajili ya
mazoezi, pia alifunga safari kwenda kufanya mazungumzo na Sunderland
kuisaidia Simba, lakini amekuwa akilalama kwamba migogoro na utendaji
mbovu ni tatizo.
Katika mkutano wa jana jijini Dar, Rage alitangaza kumteua Malkia
katika nafasi hiyo na nafasi yake katika kamati ya utendaji akamteua
Michael Richard Wambura aliyewahi kuwa katibu mkuu Simba.