Diwani wa kata ya Issuna wilaya ya Ikungi,Stephano Misai,akizungumza kwenye mahafali ya kwanza ya darasa la saba shule ya msingi Unyahati iliyopo kijiji cha Muungano .Mgeni rasmi huyo amezitaka shule za msingi na sekondari zenye bahati ya kuwa karibu na huduma ya umeme, kuweka nishati hiyo kwa ajili ya wanafunzi kujifunza kompyuta. Wa kwanza kushoto (aliyekaa) ni Chiku Alli raia wa Norway aliyekusanya fedha kutoka kwa raia wa Norway na kugharamia ujenzi wa shule ya Unyahati. Kulia ni mwenyekiti wa kamati ya shule, Alli.
Wazazi/walezi wilayani Ikungi mkoa wa Singida,wamehimizwa kuongeza bidii kuwalea watoto wao katika maadili mema, kama njia mojawapo ya kuwajengea mazingira mazuri ya kujiendeleza kielimu.
Changamoto hiyo imetolewa na raia wa nchini Norway ,Chiku Alli, wakati akizungumza kwenye mahafali ya kwanza ya shule ya msingi ya Unyahati iliyopo katika kijiji cha Muungano wilaya ya Ikungi.
Alisema uzoefu unaonyesha wazi malezi mabaya yanachangia kwa kiasi kikubwa watoto kutokufanya vizuri katika masomo yao na hata shughuli zingine za maendeleo.
“Malezi ya maadili mema kwa mtoto, sio kumpiga fimbo pindi anapofanya makosa au anapokwenda kinyume na maadili mema.Njia sahihi ni kukaa naye karibu na kumweleza madhara ya utovu wa nidhamu. Pia mfahamishe kwa ufasaha faida zitokanazo na maadili mema.Kazi hii mzazi/mlezi aifanye bila kuchoka”,alifafanua Chiku.
Akifafanua zaidi, alisema wazazi/walezi wengi hivi sasa hawapo karibu na watoto wao na mbaya zaidi,wanatoa uhuru mkubwa uliopitiliza.
“Mtoto akipewa uhuru wa kupitiliza ni lazima awe mtovu wa nidhamu na hataheshimu wazazi/walezi wao au mtu mwingine ye yote .Mtoto akifikia hatua hiyo, hatatambua kabisa umuhimu wa elimu ambayo ingemwezesha kumudu maisha yake”, alisema.
Diwani mstaafu wa nchini Norway Chiku Alli (mzaliwa wa Singida), akizungumza kwenye mahafali ya kwanza ya shule ya msingi Unyahati wilaya ya Ikungi.Chiku amefadhili ujenzi wa shule hiyo baada ya kuchangisha raia wa nchini Norway na ameahidi ndoto ya kijiji hicho kuwa na shule ya sekondari, atahakikisha inatimia.
Aidha, Chiku mzaliwa wa Singida mjini, amewataka wazazi/walezi kufuatilia kwa karibu maendeleo ya shule ya watoto wao mara kwa mara ili kama kuna tatizo, aweze kulishughulikia mapema.
“Mtoto wako akipata elimu ya kukidhi mahitaji, elimu hiyo haitamsaidia yeye binafsi,familia yake,kijiji chake, wilaya yake, mkoa wake, taifa lake, mbali itasaidia dunia nzima”, alisisitiza.
Chiku baada ya elimu yake ya sekondari mkoani Singida,mwaka 1984 alihamia Norway na mwaka 1995,alipata uraia wa nchi hiyo baada ya kuolewa na Dk. Bjorn Blomberg.
Baada ya kuwa raia wa Norway,mama yake mzazi Mwagili Saidi Gwau,alimshauri atafute fedha kwa ajili ya kujenga shule ya msingi Unyahati kuwapunguzia adha wanafunzi wa kijiji cha Muungano kutembelea kilometa nne kwenda na kurudi Ikungi shuleni.
Chiku aliufanyika kazi ushauri huo na kujenga shule ya msingi.Pia ameahidi atajitahidi kadri ya uwezo wake kuhamasisha raia wenzake wa Norway kusaidia ndoto ya kijiji hicho kuwa na sekondari inatimia.
Mama mzazi wa Chiku, Mwagili Saidi Gwau, akizungumza kwenye hafla ya mahafali ya kwanza ya shule ya msingi Unyahati kijiji cha Muungano.Mama Mwagili amesema yeye ndiye aliyemshauri mtoto wake kujenga shule ya msingi, ili kuwaondolea adha wanafunzi kutembea umbali wa kilometa nne kwenda na kurudi shuleni Ikungi.
Raia wa Norway aliyefadhili ujenzi wa shule ya msingi Unyahati kijiji cha Muungano wilaya ya Ikungi, Chiku Alli, (wa pili kushoto) akijifuta machozi baada ya kikundi cha uhamasishaji kumpongeza na kumsifu kwa moyo wake wa kukumbuka wakazi wa kijiji alichozaliwa mama yake kwa kuwajengea shule ya msingi.
Baadhi ya wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule ya msingi Unyahati kijiji cha Muungano waliohitimu darasa la saba mwaka huu.
Raia wa Norway mfadhili wa ujenzi wa shule ya msingi ya Unyahati kijiji cha Muungano (wa tatu kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na wahitimu wa kwanza wa darasa la saba katika shule hiyo.Wa nne (waliokaa) ni diwani wa kata ya Issuna, Stephano Misai ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo.
Bendera za taifa la Tanzania na Norway,zikipea kwenye viwanja vya shule ya msingi Unyahati kijiji cha Muungano wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni