RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE AZINDUA RASMI MKOA WA NJOMBE jana.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akibofya kitufe huku wazee wa Njombe wakirusha njiwa kuashiria kuzinduliwa rasmi mkoa wa Njombe jana Oktoba 18, 2013 katika Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Maisha Bora kwa Watanzania hayawezi kuja kwa watu kushinda wanacheza mchezo wa pool badala ya kujihangaisha kwa kufanya kazi na shughuli nyingine za kujiingizia mapato.
Aidha, Rais Kikwete ameahidi kuwa Serikali yake itakomesha haraka iwezekanavyo kero ya wananchi wa sehemu za Mkoa wa Njombe kulazimika kupanda mitini ili kupata mawasiliano ya simu za mkononi.
Rais Kikwete amayesema hayo jana, Ijumaa, Oktoba 18, 2013, wakati alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Wanginyi, Kata ya Lupembe, Wilaya ya Njombe katika Mkoa Mpya wa Njombe kwenye siku yake ya kwanza katika ziara yake ya siku saba kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa huo.
Akizungumza na wakazi wa Kijiji hicho na vijiji vya jirani, Rais Kikwete amezungumzia dhana nzima ya Maisha Bora kwa Watanzania akisisitiza kuwa maendeleo na Maisha Bora kwa Kila Mtanzania hajawezi kupatikana kwa watu kushinda wanacheza mchezo wa pool mchana kucha.
“Ndugu zangu, nimepata kusema huko nyuma na nataka kurudia tena kuwa Maisha Bora kwa Kila Mtanzania yanawezekana kwa watu kujituma na kuchapa kazi na siyo kwa watu kushinda kwenye meza za pool wakipiga kale kampira huko wakiilaumu Serikali na kuulizana ‘Maisha Bora yako wapi?’”
Ameongeza Rais Kikwete: “Inawezekana kweli Maisha Bora yakaja kwa mtu anayeshinda anagonga mpira wa pool kwenye meza? Ni kwa kufanya kazi kwa bidii na shughuli nyingine za kutuingizia kipato ndipo maisha yetu yatakapokuwa bora.”
Kuhusu hali ya mawasiliano ya simu Mkoani Njombe, Rais Kikwete, baada ya kuwa ameambiwa kuwa katika baadhi ya sehemu za Mkoa huo, watu wanalazimika kupanda juu ya miti ili kupata mawasiliano, alisema kuwa Serikali yake itakomesha haraka kero hiyo.
“Ni ajabu na aibu kabisa kwamba watu wanalazimika kupanda miti ili kupata mawasiliano….Hii ni hatari … kwa sababu mtu anaweza kuanguka na kuvunja viungo…mtu anaweza kuvunja kiuno,” alisema Rais Kikwete huko watu wakiangua kicheko.
“Tutahakikisha kuwa watu hawavunjiki viungo kwa sababu ya kupiga ama kupokea simu za ndugu zao,” Rais Kikwete amewahakikishia wana-Njombe.
Katika kufafanua azma hiyo ya Serikali kumaliza kero hiyo, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa Serikali italimaliza tatizo la mawasiliano katika Mkoa wa Njombe kwa awamu mbili.
Alisema kuwa katika awamu ya kwanza, kiasi cha sh milioni 260 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha mawasiliano katika vijiji 25 vya Jimbo la Uchaguzi la Njombe Kaskazini na kuwa kazi hiyo itakuwa imekamilika ifikapo Machi, mwakani, 2014. “Tunataka watu waache kupanda miti kwa kutafuta mawasiliano ya simu tu.”
Amesema kuwa katika awamu ya pili, kiasi cha sh bilioni 1.552 zitatumika kutoka Mfuko wa Mawasiliano Vijijini kwa ajili ya kuboresha mawasiliano ya simu katika Mkoa mzima wa Njombe.
Amesema kuwa kazi ya kuboresha mawasiliano katika awamu hiyo ya pili, itakamilika ifikapo Agosti, mwakani, 2014.
Kuhusu matumizi ya simu zenyewe, Mheshimiwa Mbarawa amewataka Watanzania kuzitumia simu hizo za mkononi vizuri kwa mawasiliano ya maana na yasiyokuwa na ovyo ikiwa ni pamoja na kutukana watu. “Tuzitumie simu zetu vizuri kwa mawasiliano mazuri na ya maana na siyo kutumia simu kujenga na kusambaza fitina na majungu ama kushiriki matusi dhidi ya watu wengine.”
Baadaye jioni, Rais Kikwete alikuwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika sherehe za Uzinduzi Rasmi wa Mkoa wa Njombe kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni