Watiwa Mbaroni dakika 3 baada ya kufnga ndoa
JESHI la polisi nchini limefanikiwa kuisambaratisha ndoa ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mboga iliyopo Chalinze mkoani Pwani, Asha Daru mwenye umri wa miaka 15, aliyeozeshwa kwa Said Ally (29), mkazi wa Pugu jijini Dar, Ijumaa iliyopita.
Ndoa hiyo iliyotawaliwa na usiri mkubwa, ilifungwa nyumbani kwa bibi wa mwanafunzi huyo aitwaye Asha Abdallah maeneo ya Tandale Kwamtogole, Dar.
Kuvuja kwa siri ya ndoa hiyo kulifanikishwa na mmoja wa ndugu wa familia ya mwanafunzi huyo ambaye alidai kitendo hicho kilimkera hivyo kuwaomba mapaparazi wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) iliyo chini ya Global Publishers kumnusuru binti huyo mdogo aliyedaiwa kulazimishwa kuolewa. Baada ya kumsikiliza kwa umakini ndugu huyo mwenye mvi za hekima, mapaparazi wetu walilishirikisha jeshi la polisi na kuanza kuwafanyia mtego wa kuwanasa waliokuwa wakifanikisha tukio hilo.
BWANA HARUSI AWASILI UKWENI
Mishale ya saa 4:00 asubuhi kama ilivyoripotiwa na mtoa habari wetu, tayari bwana harusi ambaye ni fundi seremala alikuwa akiwasili ukweni na kupokelewa na nderemo za chinichini huku mapaparazi wetu wakiwa wamezingira eneo hilo. Mapaparazi wetu walifanya upekepeke na kuingia hadi chumba cha bi harusi mtarajiwa na kumkuta shangazi yake akimpamba fastafasta kwa kile ilichoonekana kama walichelewa kumaliza kazi hiyo hadi ndoa inaanza kufungwa.
USTAADHI AMWAGA MAWAIDHA NA NDOA
Makachero wa jeshi la polisi na OFM, wakiwa kama wageni waalikwa, walisubiri kila kitu kiendelee ili kupata ushahidi wa tukio ambapo ustaadhi aliyekuwa akifungisha ndoa hiyo alionekana akimfungisha Said ambaye alitamka mbele ya waozaji na wageni wengine wakiwemo makachero kuwa anamuoa binti huyo kwa mahari ya shilingi laki tatu na nusu ambapo alilipa laki mbili na kubakiza deni la laki moja na nusu. Baada ya tamko hilo, zilisikika nderemo za chinichini kutoka chumbani kwa bi harusi. Huku nderemo zikiendelea, ustaadhi aliyekuwa akifungisha ndoa hiyo alianza kutoa mawaidha ya ndoa akiwausia maharusi kuishi kwa maadili ya kumpendeza Mungu na kuijaza dunia kama watajaliwa.
POLISI WAVAMIA KATIKATI YA SHEREHE
Mambo yakiwa yamenoga huku polisi wakisubiri wahusika wamalize mambo yao, inspekta wa jeshi la polisi aliyevalia kiraia akiwa na ‘mkwaju kiunoni’ alisimama na kujitambulisha kwa jina la Inspekta Rodger na kuwaweka chini ya ulinzi bwana harusi, ustaadhi, bi harusi, bibi yake na ndugu wengine waliokuwa eneo hilo. Wote wakiwa chini ya ulinzi, Inspekta Rodger aliwatajia tuhuma zao na kuwaita vijana wake waliotanda eneo hilo na kuwaamuru kuwakamata watuhumiwa wote na kuwatia kwenye ‘difenda’ msobemsobe kwa ajili ya safari ya kuelekea Kituo cha Polisi cha Magomeni, Dar kutoa maelezo.
MAHARUSI WATIWA KWENYE DIFENDA
Maharusi waliongozwa na kupandishwa kwenye difenda na kufuatiwa na ustaadhi, bibi wa bi harusi, mshenga aliyefahamika kwa jina la mama Batenga na ndugu wengine.
Maharusi waliongozwa na kupandishwa kwenye difenda na kufuatiwa na ustaadhi, bibi wa bi harusi, mshenga aliyefahamika kwa jina la mama Batenga na ndugu wengine.
BIBI AMWAGA TAMBO KITUONI
Wakiwa kituo cha polisi, bibi wa bi harusi alikuwa akijigamba kuwa ndoa hiyo ya mjukuu wake ni halali na kusema umri wa miaka 15 alionao siyo sababu ya kukosa kuolewa. Akimzungumzia binti huyo mwanafunzi, bibi huyo alisema aliamua kumuoza mjukuu wake huyo kwa kuwa alikuwa hapendi shule na alikuwa amekubuhu kwa utoro hivyo akaona ni bora aende kwa mume. “Kwani mtu kuolewa na miaka 15 ni ajabu gani? Sisi Waluguru kwetu tunaolewa hata chini ya miaka hiyo, mimi mwenyewe huyu babu yake amenioa nikiwa na miaka 15, sasa leo ajabu iko wapi?” alihoji bibi huyo.
BWANA HARUSI ALALA LUPANGO
Ulipofikia wakati wa kutoa maelezo, bwana harusi alisema kwamba yeye aliambiwa mkewe mtarajiwa alikuwa na umri wa miaka 18 na angejua kama ana umri huo asingemuoa. Licha ya utetezi huo, sheria iliendelea kumbana kwa kufanya kosa hilo ambapo alifunguliwa kesi ya jaribio la ubakaji kisha akaswekwa lupango. Wengine waliowekwa rumande kwenye tukio hilo ni baba wa bi harusi, Daru Abdallah, bibi wa bi harusi, Asha Abdallah, mjomba wa bi harusi ambaye jina lake halikuweza kupatikana pamoja na mshenga. Bi harusi huyo yeye alipelekwa ustawi wa jamii kwa ajili ya mchakato wa kuangalia mustakabali wa maisha yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni