Social Icons

Jumanne, 5 Agosti 2014

TUME YA WARIOBA YAIVUA NGUO SERIKALI, YASEMA WANAPOTOSHA KUHUSU KATIBA MPYA

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, 
Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba

JANA taifa lilisimama saa nne kwa Watanzania kuelekeza masikio 
na macho kwenye runinga kusikiliza ufafanuzi wa wajumbe wa iliyokuwa 
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, juu ya upotoshaji wa viongozi waandamizi wa 
serikali kuhusu mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu ya katiba mpya.
Wajumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba, 
waliwataja viongozi hao kuwa ni Stephen Wassira, William Lukuvi, 
Anna Tibaijuka na Mwigulu Nchemba katika mdahalo wa katiba mpya uliofanyika 
Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, uliondaliwa na 
Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kurushwa na runinga ya ITV.
Jaji Warioba, alianza kwa kuweka hadharani namna watu wenye 
propaganda za mfumo wa serikali mbili wanavyopotosha maana nzima ya 
rasimu ya pili ya tume hiyo inayoelekeza mfumo wa serikali tatu.
Alisema watetezi wa serikali mbili, wamejikita kuelezea 
upungufu wa serikali tatu huku wakiacha mazuri ya muundo huo
 pamoja na udhaifu wa serikali mbili za sasa.
Jaji Warioba, alikanusha kauli iliyotolewa na 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, 
William Lukuvi, kuwa kuna maoni mapya yamewasilishwa serikalini.
Alisema hajabadilika katika msimamo wake wa kutetea serikali tatu kama 
wananchi walivyotaka, na kwamba kinachofanywa na wanaoeneza maneno hayo ni 
uzushi wenye malengo maalum.
Alifafanua kuwa kilichofanywa na wao ni kupeleka serikalini yale 
mambo ambayo waliyachuja na ambayo yasingekuwa na nafasi katika 
Serikali ya Muungano zaidi ya kusubiri Katiba ya Tanganyika.
“Sijabadilika, na jambo la msingi ni kwamba yale tuliyoyachuja badala ya kutupa 
tulisema tukakabidhi serikalini kwa ajili ya kusaidia kuwa kumbukumbu kwao pale 
watakapoona wanakwama, lakini muhimu hayo wanayosema tumepeleka kuonyesha 
kuwa tumebadilika ni vema waweke hadharani,” alisema Jaji Warioba.
Alisema bado kuna haja ya viongozi kuendelea kuvumiliana na kutafuta 
maridhiano yatakayozaa katiba bora ya Watanzania, huku akibainisha kuwa 
hata wao walikuwa na tofauti zilizomalizwa kwa kuangalia maslahi ya taifa badala ya
 makundi waliyotoka.
Kwamba kabla ya Bunge la Katiba kuanza, aliwashauri viongozi wa vyama
 vya siasa kukutana na kukubaliana baadhi ya mambo, na kwamba viongozi
 hao hawakuweza kufanya jambo hilo, hali iliyozalisha matokeo ya sasa ya mchakato ulipofikia.
Jaji Warioba alikataa dhana ya wanasiasa na wachambuzi 
mbalimbali wanaotaka Bunge hilo liahirishwe kwa muda 
kuchagua baadhi ya mambo yatakayofanyiwa maboresho 
huku yakitajwa kuwa ni kuboresha Tume ya Uchaguzi na kutoa fursa kwa mgombea binafsi.
Alisema, haafiki mambo hayo kuwa kipaumbele na kuachwa 
kwa mambo muhimu ya wananchi.
Aliyataja baadhi ya mambo muhimu ya kujadiliwa mbali na 
masuala ya uchaguzi, kuwa ni pamoja na suala la uwazi na uwajibikaji, 
kwa madai kwamba huwezi kuwa na utawala bora kama hakuna uwazi na uwajibikaji.
Pia, alisema suala la maadili na tunu ya taifa ni mambo ambayo 
wananchi walizungumzia sana na haki za binadamu ambako walitaka
 kuwekwa kwa utaratibu wa utekelezaji kwa kuwa hata zilizopo hazitekelezeki.
Aidha, Jaji Warioba aliwashangaa wale wanaohangaika na 
takwimu, lakini akasisitiza kuwa itambulike wajumbe wa tume ndio 
waliozunguka mikoani na kuzungumza na wananchi na kuna mengi 
yalisemwa kwa uwazi kabisa ambayo wengi hawayajui.
Paramagamba aonya
Kwa upande wake, Profesa Paramagamba Kabudi akichangia katika mjadala huo, 
aliasa kuzingatia utu na kuheshimu mawazo ya wengine.
Alisema kwa upande wake, hawahofii Wazanzibar kwa kuwa wao wanayo 
mambo yao na yanayojulikana, na kwamba Watanganyika mambo yao 
wameyaficha mioyoni, jambo aliloeleza kuwa ni hatari kama hawatapatiwa 
mahitaji yao mapema.
Alisema kwamba ni wakati muafaka hivi sasa 
Watanganyika wakapewa serikali yao wakiwa wanaidai kwa amani, 
badala ya kusubiri waongezeke na kuidai kwa nguvu.
“Ni busara kuwapa Watanganyika serikali yao wakati wanaiogopa, badala 
ya kusubiri waidai wakati wakiwa wengi na muda wa kuwaongoza ukiwa haupo,
” alisema Profesa Kabudi na 
kutoa mfano wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ambaye wakati wa 
mchakato wa taifa kuingia mfumo 
wa vyama vingi miaka ya 90 mwanzoni, licha wakati ule waliokuwa
 wakitaka vyama vingi walikuwa wachache, 
alivikubali, kwani alijua ni bora kuliko waliokuwa wakiunga
 mkono wangepuuzwa na kuja kuvidai kwa nguvu.
Kuhusu muundo wa rasimu, Profesa Kabudi alisema inatoa 
fursa ya rais wa muungano kushitakiwa kwa uhaini kama atakiuka 
mambo yaliyoamuliwa na mahakama ya muungano.
Alisema tatizo kubwa lililopo, ni kwa watu waliojivika 
upumbavu kushupalia kila jambo hata kama hawana uwezo nalo,
 wakiamini nguvu zitawalinda huku akisisitiza kuwa, hakuna aliye mkubwa juu ya sheria.
Butiku amshangaa rais
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, 
kwa upande wake alieleza kuwa Rais Kikwete alipokubali 
mchakato wa katiba na kuunda tume, hakuwa na mamlaka ya kuiingilia tena.
Alisema jambo la msingi ni wahusika kufuata kile 
kilichokusanywa kwa wananchi na kuheshimu, 
badala ya yale wanayoyakwaza kwenda kupata ushauri ndani ya chama.
“Ninyi simamieni kile mnachoamini kilichokusanywa na tume,
 hapa hakuna nani wala nani, hata Wassira hayupo, watu 
wanasema tume imesema uongo, lakini tunajua namna 
umri wetu ulivyo, tutasema uongo kwa ajili ya nini, 
huu mchakato ni wa wananchi,” alisema Butiku.
Alisema katika mazingira ya sasa wanapoamua 
kusema wanaitwa wachochezi, na kwamba wananchi 
wanapaswa watafakari kwanini baadhi ya vitabu walivyokusanyia
 maoni vimefichwa na tovuti ya tume imefungwa.
Aliongeza kuwa Jaji Warioba anaficha baadhi ya 
mambo, ikiwamo kueleza wazi kuwa kutungwa kwa 
katiba ya Zanzibar ya 2010 kulivunja uwepo wa muungano.
Alipoulizwa kama hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa 
bungeni iliharibu mchakato mzima wa Katiba Butiku, 
alisema nchi ina Rais na anaheshimiwa sana na kwamba
 heshima ina pande mbili huku akizitaja kuwa njia mojawapo
 ya kumheshimu rais ni kutokuficha ukweli na kwamba upande wa
 pili ni heshima ya kuficha ukweli.
Alisema mtu atakayeficha ukweli atakuwa hamuheshimu rais, 
na kwamba kitendo cha kusema hakushauriana na tume 
kinapaswa kifikiriwe kwa makini kwa kuwa wao walishauriana nae vya kutosha.
Butiku alisema rais anapaswa kuheshimiwa na 
hata eneo alilotolea kauli hiyo linapaswa kuheshimiwa, na 
kwamba muhimu Watanzania wajue kuwa walishauriana kwa kina.
Polepole afichua siri
Aliyekuwa mjumbe wa tume hiyo, Humphery Polepole, alisema 
wakati wakikusanya maoni, viongozi mbalimbali wa kiserikali waliojitokeza 
mbele yao walitaka muundo wa serikali tatu na hata tasisi wanazozisimamia
 zilibainisha umuhimu wake.
Alizitaja taasisi hizo kuwa ni Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, 
Tume ya Makatibu na Viongozi wa Serikali ya Zanzibar, 
pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Alisema anapowaona baadhi ya viongozi waliotoa maoni ya
 serikali tatu wanavyotumia nguvu ya kutaka serikali mbili wakiwa
 hadharani, anashindwa kuwaelewa wana dhamira gani kwa Watanzania.
Kuhusu gharama za Serikali ya Muungano, 
Polepole alisema hakuna gharama kubwa zaidi ya
 kupunguza matumizi na kubainisha kuwa haziwezi kuzidi sh trilioni 2.
Awadh Said ashangaa madai ya gharama
Mwanasheria Awadh Said ambaye naye alikuwa 
mjumbe wa tume hiyo, alisema anashangazwa na watu 
wanaokimbilia takwimu na gharama katika suala zima
 la rasimu huku wakishindwa kuainisha idadi ya wabunge 
watakaopungua kwa kupatikana serikali tatu.
Alisema muundo mzima wa wabunge wote wa muungano 
kwa sasa una watu 434 na kwamba katika Serikali ya 
Muungano iliyopendekezwa idadi hiyo itapungua kwa wabunge 100.
Kwamba tume haikuelekezwa ichukue takwimu bali uzito wa 
hoja, na kwamba hoja zilizotolewa ndizo zimezaa rasimu iliyopo.
“Nashangaa wengine wanajiita wachumi huku wakishindwa kuona 
namna gharama zitakavyopungua katika muundo wa serikali tatu, lakini 
katika hali ya sasa wanapaswa watuambie ni wizara gani inayofanya 
kazi yake Zanzibar ukiacha zile za muungano na sana sana ile ya 
Mambo ya Ndani,” alisema huku akihoji kama Wizira ya 
Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewahi kwenda kusimamia maendeleo ya ardhi Zanzibar.
Aliongeza kuwa kwa sasa Zanzibar inajisimamia kwa masuala mbalimbali,
 ikiwamo ardhi, hivyo kusema uwepo wa serikali tatu ni gharama ni kuudanganya umma.
Awadh alisema suala la muungano kwa bahati mbaya linazungumziwa na watu wasiolielewa au  
hawapendi kufuatilia mambo, zaidi ya kutengeneza propaganda na vitisho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates