Nasikitika kwamba washauri wake hawakumshauri vizuri, kauli yake imekuwa ni kama kujidhalilisha mbele ya jamii.” Dk Helen Kijo-Bisimba
Dar es Salaam/mikoani. Siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa hotuba yake mwisho wa mwezi, watu mbalimbali wamesema Rais hawezi kukwepa lawama za kuvuruga mchakato wa katiba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dk Helen Kijo-Bisimba amewakosoa washauri wa Rais Jakaya Kikwete, akidai kwamba wamemshauri vibaya kuikana Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akitoa maoni kuhusu hotuba ya mwisho wa mwezi ya Rais Kikwete aliyoitoa juzi, Dk Kijo-Bisimba aliliambia gazeti hili kuwa Rais Kikwete hana cha kujitetea kuhusu rasimu hiyo kwa sababu aliiunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, James Mapalala amesisitiza hotuba aliyoitoa Rais Kikwete wakati akilifungua Bunge hilo kuwa ilikuwa na vitisho vya wazi vilivyolenga kuwatishia wanaounga mkono muundo wa serikali tatu kwamba serikali ya muungano itapinduliwa kijeshi.
“Amerudia yaleyale tofauti na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba alivyowasilisha rasimu akionyesha vielelezo jinsi serikali tatu zinavyoweza kujiendesha, Rais Kikwete yeye hakuwa na vielelezo bali vitisho,” alisema Mapalala.
Akizungumza katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi, Alhamisi wiki hii, Rais Kikwete alisema licha ya kuwa alikuwa akielezwa kila hatua ya mchakato huo na tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba, hayakuwa mazungumzo ya kina kuhusu nini kiwe vipi katika maudhui na mapendekezo ya Tume.
Rais Kikwete alitoa ufafanuzi huo baada ya kupita miezi takribani mitatu tangu alipoanza kurushiwa lawama na viongozi wa dini, wanasiasa, wanaharakati na wananchi wa kawaida kuwa ndiye aliyevuruga mchakato huo.
“Kuna lawama kwamba eti kuwa mambo yalikuwa yanaenda vizuri mpaka pale nilipotoa hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalumu ndipo yalipoharibika. Pili nalaumiwa kwamba nawezaje kuikana Rasimu ya Katiba ambayo na mimi ni mmoja wa watu waliotia sahihi katika Rasimu hiyo?” alihoji.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk Benson Bana aliipongeza hatua ya utetezi ya Rais Kikwete, akisisitiza kwamba ameliweka taifa sawa na kuonyesha nia yake ya dhati ya kutaka Katiba Mpya ipatikane.
“Yeye kama mdau namba moja alistahili kuweka mambo sawa kwa sababu kulikuwa na upotoshaji mkubwa uliokuwa unaelezwa kuhusu hotuba yake. Ni vyema Ukawa na CCM wakaitumia fursa hiyo vyema kwa kumaliza tofauti zao ili mchakato uendelee,” alisema.
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Profesa Gaudence Mpangala, alisema hakubaliani na utetezi wa Rais Kikwete akidai kwamba ukweli wa mambo ni kuwa hotuba yake ndiyo ilivuruga mwelekeo wa Bunge hilo.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia (DP) Mchungaji Christopher Mtikila, alizungumza kwa kifupi akieleza kwamba ni vyema Rais Kikwete akubali kwamba ndiye aliyevuruga Bunge kwa hotuba yake, kisha aombe msamaha, hatua ambayo inaweza kusaidia mchakato huo kuendelea kwa usahihi.
Mkoa wa Arusha
Dk Frank Urio alisema Rais Jakaya Kikwete hawezi tu kutoa maagizo ya kuwa Ukawa warejee bungeni bila kwanza kufikiwa mwafaka kuhusu malalamiko ambayo Ukawa yaliwaondoa bungeni.
Mkoa wa Mwanza
Makamu Mkuu wa Chuo cha Biashara (CBE) tawi la Mwanza, Kimambo Geofrey alisema Rais hapaswi kulalamikiwa kwa kile alichodai kuwa hakuwalazimisha wabunge hao wapitishe muundo wa serikali mbili kama baadhi wanavyodai.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni