Social Icons

Jumamosi, 2 Agosti 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI-SERIKALI HAIJAWATELEKEZA WATANZANIA UKRAINE

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mkumbwa Ally akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu hatua zilizochukuliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi katika kuhakikisha Wanafunzi kutoka Tanzania wanaondoka katika Jimbo lenye machafuko la Lugansk huko Ukraine. Mwingine katika picha ni Bw. Ally Kondo, Afisa Habari.
Sehemu ya Waandishi kutoka Vyombo mbalimbali vya habari vya hapa nchini
Mkutano ukiendelea (Picha na Reginald Philip)

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kukanusha vikali taarifa iliyotangazwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), tarehe 30 Julai, 2014, iliyodaikuwa Serikali ya Tanzania imetelekeza wananchi wake wanaosoma Ukraine Mashariki, ambako kunarindima vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Taarifa hiyo ya upande mmoja, iliyomnukuu mtu anayeitwa Shamila, aliyedai ni mmoja wa wanafunzi Watanzania nchini Ukraine, ilisema eti wananchi hao wameachwa bila msaada wowote.

Wizara imesikitishwa na taarifa hiyo iliyotolewa bila kufanyiwa uchunguzi wa kutosha. Ukweli ni kwamba Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi, ambao unatuwakilisha pia Ukraine, umechukua hatua za haraka tangu mwezi Juni, 2014, kuhakikisha wanafunzi Watanzania wote wanaondoka katika jimbo la Lugansk lililoko vitani.

Ubalozi ulishirikiana na Rais wa wanafunzi wa Tanzania katika mji wa Lugansk, Bwana Ahmad Juma, kufanikisha kuondoka kwa Watanzania wote 32 waliokuwepo huko kurudi nyumbani au kuhamia mji wa Kharkov, ambao ni salama zaidi.

Serikali kupitia Ubalozi wake Moscow iliwaombea wanafunzi hao malazi kwenye Chuo cha Kharkov Technical University ambacho kilikubali kutoa hosteli kwa wanafunzi hao. Hata hivyo, wengi wa wanafunzi hao waliondokea Lugansk kurudi nyumbani isipokuwa wanafunzi saba ambao walihamia Kharkov. Mpaka tarehe 31 Julai, 2014, ni wanafunzi watatu tu waliokuwa wamebaki mjini Kharkov. Wanafunzi 20 wamedhaminiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Bodi ya Mikopo.

Orodha ya wanafunzi iliyopo Ubalozini haijumuishi jina la Shamila anayedaiwa kuhojiwa na BBC. Inasemeka na mtu huyo alikwishamaliza masomo yake ya shahada ya kwanza na ya pili lakini akaamua kubakia Ukraine akifanya udalali wa kuleta wanafunzi kutoka Tanzania kwa kushirikiana na vijana wa Nigeria.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kuuhakikishia Umma kuwa inasimamia kikamilifu usalama na ustawi wa Watanzania walioko Ukraine na popote ulimwenguni, na inasikitishwa na taarifa ya uzushi, upotoshaji na uzandiki iliyomnukuu mtu anayeitwa Shamila.

IMETOLEWA NA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA DAR ES SALAAM
02 AGOSTI, 2014

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates