Social Icons

Alhamisi, 14 Agosti 2014

Gaza :vita kukomeshwa kwa siku 5 zijazo.


Israel na Palestina zimekubaliana kusitisha mapigano kwa siku 5 zijazo.

Kufuatia tangazo hilo la kusitishwa kwa mapigano, Israel ilitekeleza shambulizi la angani na kudai ilikuwa inajibu shambulizi la roketi kutoka Gaza.
Hakukuwepo na ripoti nyinginezo za ukatili usiku kucha, huku pande zote mbili zikitarajiwa kuendelea na mazungumzo mjini Cairo, chini ya mpango uliotolewa na Egypt.
Wa-Israel walizindua operesheni ya kijeshi ndani ya Gaza tarehe 8, Julai 2014, ili kukomesha mashambulizi ya roketi kutoka Gaza.
Hamas, inayotawala Gaza na inayohusika kwenye mazungumzo mjini Cairo, imekana kuwa wapiganaji wake walifanya shambulizi la roketi dhidi ya Israel, usiku wa Jumatano.
Msemaji wa majeshi ya Israel Peter Lerner amesema kwenye mtandao wa Twitter: “Hakuna haja ya kurukia hitimisho.
Sifahamu aliyetekeleza shambulizi la roketi dhidi ya Israel, saa nne usiku.”
Punde tu baada ya shambulizi hilo, hakukuwepo na ripoti zozote kutoka pande zote mbili kuhusiana na majeruhi au vifo.
Maeneo yaliyoharibiwa Gaza
Lakini mwanahabari wa BBC aliyeko Gaza Kevin Connolly anatuarifu kuwa kulingana na makadirio yake huenda mazungumzo ya siku za usoni yakawa magumu zaidi.
Maafisa kutoka pande hizo mbili wamekuwa wakitoa hoja zao na matakwa yao kupitia wasuluhishi walioko mjini Cairo.
Mazungumzo hayo yanaazimiwa kuleta mwafaka wa kudumu na kusuluhisha migogoro iliyoko Gaza.
Wapalestina wanataka vizuizi vilivyowekwa dhidi ya Gaza kuondolewa, huku Israel ikitaka Gaza kupokonywa silaha zote.
Kulingana na ripoti kutoka Misri na Palestina, Israel imeonyesha kuwa huenda ikakubali kulegeza sehemu kadhaa za vizuizi hivyo .
Mapendekezo mengine chini ya majadiliano hayo ni, kupunguza maeneo yaliyokatazwa kupitiwa ndani mwa Gaza, na kuongeza maeneo ya kando ya bahari yanayotumika na wavuvi wa Gaza kuendeleza shughuli zao.
Wapatanishi wa Misri wamependekeza kuahirishwa kwa majadiliano ya matakwa mengine, yakiwemo: kufunguliwa kwa bandari ndani mwa Gaza, na kurejeshwa kwa miili ya wanajeshi wawili wa Israel waliouwawa.
Wapalestina na Waisrali wameafikiana kusitisha mapigano kwa siku 5 zaidi.
Takriban watu 2,000 wamefariki kufuatia mapigano yaliyoanza tarehe 8, Julai, ndani mwa Gaza.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, kati ya waliouwawa kuna zaidi ya wapelestina 1,900, wengi wao wakiwa raia.
Wanajeshi 64 wa Israel, na raia watatu wa ki-Israel pia waliuwawa kufuatia mapigano hayo.
Mvutano kati ya Gaza na Israel uliongezeka baada ya kutekwa nyara na kuuwawa kwa vijana watatu wa ki-Israel mwezi Juni.
Israel ilinyosha kidole cha lawama kwa Hamas, japo kundi la Hamas lilikana kuhusika kwake.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates