FAHAMU KWA UFUPI KUHUSUASKOFU MOSES KULOLA
Askofu Kulola alizaliwa Juni 2, 1928 katika Kijiji cha Nyahonge
wilayani Kwimba mkoani Mwanza. Ameacha mjane, watoto 10, wajukuu 44 na
vitukuu 16. Alifungua makanisa zaidi ya 4,600 ya EAGT ndani na nje ya
Tanzania, ikiwemo Zambia, Malawi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia
Kongo (DRC). Lakini ana nyumba moja tu aliyojengewa na waumini
Ni vigumu kuzungumzia historia ya vuguvugu la uanzishaji makanisa nchini, pasipo kumtaja Askofu Moses Kulola.
Askofu Kulola anajulikana na wengi kama mtu aliye na nia ya dhati
kutangaza neno la Mungu, kutokana na kile kinachoonekana wazi kwamba
hakujilimbikizia mali kama ambavyo tunaona baadhi ya watumishi wa Mungu
siku hizi wanavyomiliki majumba, benki na hata magari ya milioni ya
shilingi.
Kwa namna inavyoonekana nchini, ni kama kuna kundi kubwa la watumishi
wanaohubiri kwa lengo la kushibisha matumbo yao zaidi; Hawana mpango
thabiti wa kusaidia yatima wala maskini, badala yake waumini ndio
wanaonyonywa kwa kutoa zaka na sadaka ambazo baadhi yake hata matumizi
yake yamekuwa yakizua maswali.
Utumishi wa Mungu na mali
“Hakuna shaka kwamba kama kila nyumba ya ibada Tanzania ingekuwa na
mpango thabiti wa kusaidia watu maskini, yatima na watu wengine wenye
hali ngumu, hali ya maisha ingekuwa nzuri zaidi kwa wengi. Lakini wapi,
baadhi ya watumishi wako ‘bize’ kujaza matumbo, wanaendesha magari ya
kifahari yenye thamani ya mamilioni ya shilingi badala ya kutumia fedha
hizo kutangaza neno la Mungu au kusaidia wasiojiweza,” anasema Charles
Mtanga, mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam.
Mtanga anawashauri viongozi wa nyumba za ibada kuwa na mkakati wa
kusaidia yatima na watu wengine wasio na uwezo, huku wakiendelea
kutangaza neno la Mungu, ili wote waweze kuufurahia ulimwengu.
Utanuzi wa huduma
Kwa mujibu wa Askofu wa EAGT Sengerema, Joshua Wawa, Askofu Kulola
alizaliwa Juni 2, 1928 katika Kijiji cha Nyahonge wilayani Kwimba mkoani
Mwanza. Ameacha mjane, watoto 10, wajukuu 44 na vitukuu 16.
Katika uhai wake, Askofu Kulola alifungua makanisa 4,600 ya EAGT ndani
na nje ya Tanzania, ikiwemo Zambia, Malawi, Rwanda na Jamhuri ya
Kidemokrasia Kongo (DRC) na ameacha wosia kwamba makanisa yafunguliwe
kadiri inavyowezekana.
Hata hivyo, licha ya kuwa na wingi wote huo wa makanisa, Askofu Kulola
anamiliki nyumba moja iliyoko mkoani Mwanza aliyojengewa na waumini.
Askofu Moses Kulola
“Yoooh! Unapenda niseme?” hicho ndicho kilikuwa ‘kibwagizo’ cha Askofu
Moses Kulola wakati wa uhai wake hasa alipokuwa akihubiri mikutano ya
injili.
Askofu Kulola alifariki Agosti, 29 mwaka huu katika Hospitali ya AMI
(African Medical Investments) iliyopo Slipway jijini Dar es Salaam.
Mikakati mingine
Askofu huyo mkuu wa EAGT, ameelezewa kuwa amewahi kwenda Ikulu mara kadhaa kuombea nchi kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete alishuhudia hayo wakati wa maziko yake yaliyofanyika
Bugando, jijini Mwanza kwamba kwa namna inavyoonekana Askofu Kulola
alikuwa ana maanisha kuifanya kazi ya Mungu.
Kufungwa na kunusurika kuuawa
Askofu Kulola amewahi kufungwa gerezani kwa ajili ya kuhubiri injili,
pia amewahi kunusurika kifo katika ajali. Rais Kikwete anamzungumzia
kama mchungaji aliyekuwa mkweli na aliyeutumia muda wake kusaidia wote
bila kujali imani zao za dini.
Maisha yake
Katika maisha yake, Kulola alisoma Shule ya Msingi ya Ligsha Sukuma,
mwaka 1939 baadaye akajiunga na taasisi ya usanifu mwaka 1949.
Alibatizwa mwaka 1950 katika Kanisa la AIC Makongoro. Alimwoa Elizabeth.
Mwaka 1959 alianza kufanya kazi serikalini, wakati huo huo akihubiri
injili katika miji na vijiji. Utumishi wake serikalini ulifika mwisho
mwaka 1962, aliamua kujitolea moja kwa moja katika kazi ya kutangaza
neno la Mungu.
Mwaka 1964 alijiunga na chuo cha theolojia na kuhitimu 1966. Aliendelea na masomo ya theolojia ndani na nje ya nchi.
Alihudumu kama mchungaji katika Kanisa la AIC kabla ya kuhamia madhehebu
ya Pentekoste mwaka 1961-1962 na alifanya kazi katika Kanisa la TAG
1966 mpaka 1991 alipoamua kuanzisha Kanisa la Evangelistic Assemblies
God (EAGT) baada ya kutokea mgogoro wa kiuongozi.
Kisa cha Askofu Kulola kuanzisha kanisa lake
Katika kitabu cha Historia ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God,
mwandishi Dk Jotham Mwakimage anasimulia kiini cha mtafuruku uliolikumba
kanisa hilo miaka ya 1980 kiasi cha kusababisha mgawanyiko mkubwa.
Anasema kulikuwa na mikutano mikuu ya kanisa hilo kati ya mwaka 1980 na
1982.
“Mkutano mkuu wa mwaka 1980 ulikuwa wa kipekee kwa wale waliohudhuria,
kwani ulitawaliwa na ujumbe wa kinabii zaidi, ulifanyika kwenye jengo la
udongo lililoko Chuo cha Biblia Dodoma,” kinasema kitabu hicho na
kuongeza:
“Kwa mtazamo wangu, mkutano huu haukuonekana kama mkutano wa shughuli za
kikanisa, bali kama kusanyiko la uamsho wa kiroho katika kuwatia nguvu
wachungaji wa TAG kwa ajili ya huduma za kichungaji.”
Dk Mwakimage anaendelea kusema kuwa kulikuwa pia na mkutano wa aina hiyo
pia mwaka 1982. Lengo la mkutano huo uliofanyika pia Dodoma lilikuwa ni
kuchagua viongozi wakuu wa kanisa hilo na hapo ndipo kanisa
lilipopasuka.
“Sababu ya mgawanyiko ilitokana na ule mtafaruku uliokuwa kati ya
wainjilisti wawili mashuhuri waliokuwa na mvuto ambao ni Emmanuel Lazaro
aliyekuwa Askofu Mkuu wa TAG na Moses Kulola. Ushawishi wa viongozi hao
kiroho ulikuwa mkubwa na uligusa watu wengi,” anasimulia.
Anasema ushawishi huo uliwagusa siyo waumini tu wa kanisa hilo, bali hata wamisionari waliolisaidia kanisa hilo.
“Viongozi hawa hawakukubaliana katika mambo ya msingi na mgongano wao
ukawagusa watu wengi na matokeo yake hayakuweza kuepukika.”
“Kabla ya mwaka 1982, sheria ndogo ya uhamisho iliongezwa katika Katiba
“Uhamisho huo haukueleweka vizuri… hasa uhamisho wa Mchungaji Calist
Masalu wa Kanisa la Temeke ambalo lilikuwa ndiyo kituo kikuu cha Dar es
Salaam kwa ajili ya shughuli za Moses Kulola.”
“Wachungaji, washirika na hata wamisionari hawakuelewa sababu za
kuwahamisha wachungaji hao, hivyo wakatafsiri kwamba kumhamisha
Mchungaji Masalu kulilenga kuharibu huduma ya uinjilisti za Kulola. Kwa
sababu hiyo Mchungaji Masalu akagoma kuhama, akisubiri uamuzi wa mkutano
mkuu”. Dk Mwakimage aliyekuwa mjumbe katika mkutano huo uliotawaliwa na
minong’ono ya uhamisho wa wachungaji anasema uchaguzi ulifanyika na
Lazaro kuchaguliwa kuwa askofu mkuu na Kulola kuwa msaidizi wake. Hata
hivyo mambo yakazuka tena.
“Siku iliyofuata wakati wa kipindi cha shughuli, suala la uhamisho wa
Mchungaji Masalu likajitokeza tena na hoja kama sharti la Kulola
kuikubali nafasi yake hiyo ikaibuka. Kulola alinukuliwa akisema, “Kama
uhamisho wa Mchungaji Calist Masalu kwenda Bugando Mwanza hautatangazwa,
kuondolewa au kufutwa, basi siko tayari kupokea wadhifa mlionichagua.”
“Huo ndiyo ulikuwa msimamo wa Kulola,” anasema Dk Mwakimage na kuongeza:
“Baada ya hapo Askofu Mkuu Lazaro akasimama kujibu hoja akimpinga Kulola
akisema; “Uhamisho wa Mchungaji Masalu utabakia na kamwe hautafutwa
wala kubadilishwa”.
Ni kutokana na kauli hizi mbili zilizosigana ikawa ndiyo sababu ya
mgawanyiko kutokea. Mgawanyiko huo kwanza ulizaa chuki na kashfa
endelevu kati ya makundi hayo mawili hadi leo. Lakini kwa upande
mwingine umeyaimarisha makundi hayo, kwani hadi sasa ni madhehebu
yaliyokua.
TAG bado yaidai EAGT
Akizungumzia uhusiano kati ya TAG na EAGT hivi karibuni Askofu Mkuu wa
TAG, Dk Barnabas Mtokambali, licha ya kusema kuwa makanisa hayo yana
uhusiano mzuri, anaongeza kuwa bado kanisa lake linaidai mali zake EAGT.
Anaongeza kuwa mwaka 1991 kabla Askofu Kulola hajasajili kanisa lake,
Serikali ilimpa sharti la kurejesha mali za TAG ili apate usajili, ndipo
alipoweka ahadi ya kurudisha jambo ambalo hakulifanya hadi anafariki.
EAGT haidaiwi
Hata hivyo madai hayo yamekanushwa na Katibu Mkuu wa EAGT, Brown Mwakipesile akisema mgogoro uliopo ni wa kikatiba:
“Hakuna mali yoyote tunayodaiwa na TAG, tatizo letu lilikuwa ni la
kikatiba tu,” anasema Mwakipesile. Kanisa la EAGT chini ya Askofu Kulola
limeendelea kukua kwa kasi. Tofauti ya uongozi kati ya makanisa hayo
mawili ni kwamba, EAGT imekuwa chini ya Askofu Kulola hadi mauti
yanamkuta huku TAG ikibadilisha uongozi, kutoka Askofu Lazaro kuja kwa
Ranwel Mwenisongole hadi askofu wa sasa Dk Barnabas Mtokambali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni