Upinzani ‘wawasha moto’ Zanzibar,wataka Chikawe ajiuzulu kwa taarifa za uongo.
Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe ametakiwa ajiuzulu kwa kutoa taarifa za uongo kwamba Zanzibar ilishirikishwa kabla ya Muswada wa Mabadiliko ya Katiba kuwasilishwa bungeni na kupitishwa na Bunge Septemba mwaka huu.
Msimamo huo ulitolewa na Waziri wa Sheria na Katiba Zanzibar, Aboubakary Khamis Bakari wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliovishirikishwa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi uliofanyika Uwanja wa Kibandamaiti mjini Unguja jana.
Aboubakari alisema kwamba Zanzibar ilipokea taarifa ya awali ya mabadiliko kuhusu vifungu vinne vya Muswada wa Mabadiliko ya Katiba na kutakiwa Zanzibar itoe maoni na mapendekezo yake, jambo ambalo alisema lilifanyika kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hata hivyo, alisema vifungu vya mabadiliko ghafla viliongezwa kutoka vinne hadi 12 bila ya Zanzibar kupewa nafasi ya kujadili vifungu vinane ambavyo vina umuhimu mkubwa katika kupata katiba bora.
“Waziri nimesoma naye Chuo Kikuu mwaka 1972, Chikawe kwa hili amesema uongo vinginevyo ajiuzulu, hafai,” alisema Aboubakari.
Alisema kabla ya kufanyika Waziri akifuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge, William Lukuvi walifika Zanzibar na kutaka wajadili vifungu hivyo kwa siku moja jambo ambalo alipinga kulitekeleza.
“Baada ya kuanza kupiga kelele, wenzetu walikuja Zanzibar wakitaka tujadili mabadiliko ya mswada,nikawaambia siwezi kujadili masilahi ya nchi kijuujuu, huko ni kuiuza nchi, siko tayari kufanya hilo,” alisema.
Aboubakari alisema marekebisho yaliyofanyika katika muswada huo na kutoa nafasi kujadili na kupitisha mabadiliko ya Katiba kwa kutumia wingi wa kura ni sawa na wazimu.
Alisema mabadiliko yoyote ya Katiba yanapaswa kutumia theluthi mbili toka pande mbili za Muungano, utaratibu ambao ndiyo umekuwa ukitumika na nchi mbalimbali zenye mfumo kama wa Tanzania. Mwananchi ilipomtafuta Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kujibu tuhuma hizo alisema Aboubakari ameudanganya umma mchana kweupe kwa vile yeye na Waziri Lukuvi walifika Zanzibar kupeleka rasimu ya muswada na si kujadili na kupokea mapendekezo papo kwa hapo.
Chikawe alisema kwamba walipokabidhi muswada pia walimtaarifu siku ya kuwasilishwa muswada huo katika kikao cha Bunge na kuwataka kutoa maoni na mapendekezo kwa wakati mwafaka kabla ya kujadiliwa na kamati ya Katiba ya Sheria ya Bunge.
Alisema kwamba nyongeza ya marekebisho ya vifungu vinane yalitokana na mapendekezo ya wabunge katika kamati na michango ya wabunge ndani ya Bunge katika utaratibu unaoruhusiwa kisheria.
“Baada ya kamati ya Bunge kukaa, Mbunge Halima Mdee wa Chadema ndiye aliyependekeza kutumika kwa utaratibu wa wingi wa kura katika kupitisha mabadiliko hayo ya Katiba kama hatua ya theluthi mbili itashindwa kufikia mwafaka,” alisema Chikawe.Pia alisema mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashim Jaku yeye alitetea kwa nguvu ya hoja kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba imalize kazi yake baada ya kuwasilisha ripoti yake kwa Rais na kwamba haikuwa ni uamuzi na matakwa ya Serikali kama inavyodaiwa na vyama vya upinzani kuhusu nyongeza hiyo.
“Nyongeza ya vifungu ilitokana na wabunge katika kamati na ndani ya Bunge lenyewe, Serikali haiwezi kupuuzia ushauri wa wawakilishi wa wananchi na wabunge ambao wanaisimamia Serikali,” alisema Waziri Chikawe.
Aidha, Aboubakari alimshutumu Naibu Spika wa Bunge,Job Ndugai kwa kulidanganya Bunge kwa kitendo chake cha kutoa barua ikithibitisha Zanzibar imeshiriki wakati kuna vifungu vya ziada vimefanyiwa marekebisho bila ya kupata baraka ya Zanzibar.
Alisema kwa msingi huo amevunja na kukiuka kanuni za Bunge na wabunge wana haki ya kumshtaki kwa kutumia kanuni zao kwa kupotosha Bunge na umma.
Hata hivyo, taarifa hizo za Aboubakari kutokana na maelezo aliyotoa awali Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwenye mkutano wa hadhara, alisema Zanzibar ilishirikishwa katika kuvifanyia vifungu sita na SMZ ilitoa mapendekezo katika vifungu vitatu na baadae vikaongezwa vinane kinyemela bila ya Zanzibar kushirikishwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kwa muda mrefu viongozi wa Zanzibar walikuwa wakijitolea kupigania mabadiliko ya taifa lao na kukutwa na vizingiti ikiwemo kuwekwa vizuizini na kupewa hongo ya madaraka.
Mbatia alisema miongoni mwa viongozi waliojitoa muhanga kutaka mabadiliko ya mfumo wa Muungano ni pamoja na Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi ambaye aliondolewa kibabe madarakani chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere.
Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alimtaka Rais Jakaya Kikwete kumfuta kazi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kwa madai kuwa hawana nia njema wakikusudia kuharibu nia njema ya Rais ya kupata Katiba mpya.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema Katiba iliyopo sasa nchini haifai kwa kuwa imejaa upungufu unaokwenda kinyume na misingi ya haki za raia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni