Dar es Salaam.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema wanasiasa wanaomtuhumu kwa kumsaliti Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuhusu Muungano, ndiyo wasaliti kwa kuwa waliingiza kwenye Katiba, mambo yanayokinzana na makubaliano ya Muungano huo.
Jaji Warioba amesema usaliti huo ni pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuondoa mamlaka ya Bunge la Muungano katika utungaji wa sheria, kuitambua Zanzibar kuwa nchi inayojitegemea na kuongeza mambo ya Muungano bila kufuata Katiba.
Ametoa kauli hiyo kujibu mwendelezo wa lugha za kejeli na matusi anazorushiwa na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wengi kutoka CCM na baadhi ya viongozi wa Serikali baada ya Tume aliyoiongoza kupendekeza muundo wa serikali tatu.
Akizungumza juzi usiku katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV, Jaji Warioba alisema viongozi wa pande mbili za Muungano wanaomtuhumu, ndiyo waliouvuruga Muungano huo
“Mwalimu aliacha Bunge likiwa na mamlaka kamili, aliacha nchi ni moja, aliacha mambo ya Muungano 11 sasa yamekuwa ni 22, kwa bahati nzuri Rais Jakaya Kikwete alieleza bungeni hilo kwamba mambo hayo yaliongezekaje,” alisema na kuongeza:
“Katika kubaini kuongezeka kwa mambo ya Muungano ndivyo ilikuwa inapunguza mamlaka kwa Zanzibar, mambo 11 yaliyoachwa na mwalimu yaliingizwa kikatiba lakini haya yaliyoongezeka yalipatikana kienyeji.”
Jaji Warioba alisema enzi za uhai wake, Mwalimu Nyerere aliheshimu na kuilinda Katiba hivyo, walioivunja ndiyo wasaliti wa Muungano.
“Sasa kati ya mimi na wao ni nani msaliti kwa Mwalimu, angekuwapo (Mwalimu) ni yupi angeonekana msaliti wa Serikali ya Muungano? Wao ndiyo wameuvuruga, alichokiacha Mwalimu ni tofauti na kinachoonekana kwa sasa,” alisema Jaji Warioba.
Kuhusu Bunge
Jaji Warioba alisema mipango mingi ya maendeleo inayopangwa ndani ya Bunge la Muungano inatekelezwa upande wa Bara pekee.
“Si hivyo tu, Bunge hilo linajadili mambo ya Bara tu na halihusishi upande wa Zanzibar. Zanzibar nayo inajadili mambo yake na kujiamulia lakini jina la Bunge hilo ni Muungano,” alisema Jaji Warioba.
Kutokana na mazingira hayo, Jaji Warioba alisema Zanzibar iliamua kuondoa mamlaka ya Bunge hilo katika utungaji wa sheria kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema sheria zinazotungwa katika Bunge hilo zitatumika ndani ya pande zote za Muungano, lakini Zanzibar wakabadilisha hilo kupitia Katiba yao wakasema sheria zote zitakazotungwa ndani ya Bunge hilo, lazima zipitiwe tena na Baraza la Wawakilishi,” na kuongeza: “(Zanzibar) Hawakuishia hapo, wakafanya mabadiliko ya Katiba mwaka 2010 iliyovunja Katiba ikiitambua Zanzibar kama nchi kamili, ikaondoa mamlaka ya Rais wa Jamhuri kugawa wilaya na mikoa kwa Zanzibar tofauti na Katiba ya Muungano, kwa maana hiyo Zanzibar ikavunja nguvu ya Bunge la Muungano.”
Aidha, alisema hatua hiyo ilionekana kuuvunja Muungano kwa vitendo baada ya kuvunja mamlaka ya Rais na kutambua marais kamili katika nchi mbili tofauti.
“Kwa kawaida nchi inakuwa na amri jeshi mkuu mmoja ambaye anapigiwa mizinga 21, Jeshi la Muungano linapiga mizinga kwa marais wawili kitu ambacho hakiwezekani,” alisema.
Malalamiko ya Watanganyika
Jaji Warioba alisema Kwa upande wa Tanzania Bara, walibaini malalamiko ya Watanganyika kuwa ni pamoja na kukosa fursa mbalimbali ndani ya Zanzibar. “Watu wa bara nao wanasema Zanzibar inashiriki Bunge la Muungano, inakagua miradi ya bara na kuihoji lakini wao hawana nguvu ya kushiriki mambo hayo kwa upande wa Zanzibar,” alisema.
Aliongeza: “Mbaya zaidi wanasema Wazanzibari wanaweza kumiliki ardhi na kupata uraia kwa upande wa bara lakini haki hizo haziwezi kupatikana kwa Mtanganyika, njia pekee tukaona ni vyema Zanzibar nayo ilete mambo yake ndani ya Muungano lakini ikashindikana.”
Hoja ya takwimu
Jaji Warioba aliwataka wajumbe wa Bunge wasihangaike na takwimu badala yake wajibu maswali yaliyojitokeza kutoka kwa washirika wa Muungano.
“Takwimu siyo tatizo, sisi hatukufanya jambo jipya, ila ilikuwa ni kama marudio tu ya Tume ya Nyalali, wanahoji takwimu hizo je, hawakuona dosari kwa takwimu za maoni ya asilimia 20 kwa jaji Nyalali?
Alisema Tume yake ilizunguka nchi nzima ikiwa na waandishi waliorekodi kwa tepu, video na maandishi kwa ajili ya kuweka kumbukumbu katika mtandao wa Tume.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni