Social Icons

Jumatano, 30 Aprili 2014

BAYERN WAVULIWA UBINGWA UEFA, BALE ASEMA......


BAYERN Munich wamevuliwa ubingwa wa UEFA kwa kipigo cha mbwa mwizi baada ya 
kufungwa mabao 5-0 na Real Madrid katika mechi mbili za nusu fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Mechi ya kwanza katika dimba la Santiago Bernabeu, Real Madrid walishinda bao 1-0 na leo hii katika
 nusu fainali ya pili kwenye uwanja wa Allianz Arena mjini Munich, kikosi cha Carlo Ancelotti kimeibuka
 na ushindi wa mabao 4-0.
Real Madrid walitumia dakika 16 tu kufunga goli ambapo Luca Modric alichonga kona kutoka winga ya kulia na Sergio Ramos kujitwishwa mpira huo na kuuzamisha kimiani.
Dakika nne baadaye, beki huyo wa kati aliwamaliza Bayern baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ndogo uliochongwa na Gareth Bale.

Baadaye Real Madrid walifanya shambulizi la kushitukiza ambapo Cristiano Ronaldo alifunga bao safi
 baada ya Bale kumpatia pasi murua.
Bao hilo liliwafanya Real wahitimishe dakika 45 za kipindi cha kwanza kwa mabao 3-0.
Bao la dakika ya 90 la Cristiano Ronaldo kwa njia ya adhabu ndogo lilitia chumvi katika kidonda cha
 Bayern na kuvuliwa ubingwa kwa wastani wa mabao 5-0.
Kabla ya mechi hii, nyota wa zamani wa soka la Ujerumani, Stefan Effenberg alionesha wasiwasi 
wake kama falsafa ya Pep Guardiola itaisaidia Bayern Munich kutwaa ubingwa wa UEFA, 
wakati huu ambapo mchezaji muhimu Frank Ribery yupo katika kiwango cha chini.
Effenberg anaamini falsafa ya sasa ya Bayern ya kupiga pasi nyingi haikuweza kuwasaidia
 Bernabeu na alikuwa na wasiwasi katika mechi ya leo. 
Kipigo cha mabao 4-0 kimethibitisha mawazo ya gwiji huyo wa soka la Ujerumani.
Tangu enzi za Zinedine Zidane, Luis Figo, Roberto Carlos na Raul, Real Madrid hawajacheza fainali 
na sasa wamefanikiwa kuelekea La Decima mjini Lisbon mwezi ujao.
Kabla ya mechi, watu walikuwa wanasema Real Madrid wanahitaji bao 1 zaidi au suluhu ili kuwashinda 
Bayern, 
lakini wameweza kushusha mvua kubwa ugenini. 
Baada ya mechi hiyo, Gareth Bale amesema kipigo walichotoa leo hii ni sababu mojawapo ya yeye kujiunga na 
klabu kubwa duniani majira ya kiangazi mwaka jana.
“Ni matokoe mazuri mno kwetu. Nadhani tumejituma, tulitumia vizuri mbinu zetu na kucheza vizuri usiku huu, 
hivyo tulistahili ushindi”. Bale amezungumza na ITV.
“Walicheza mpira sana, waliacha nafasi za kushambuliwa kwa kushitukiza, nasisi tunapenda hivyo”.
“Tuna wachezaji wenye kasi na tunatumia nafasi kama hizo. Tulikuwa katika kiwango bora na tumefurahi kufika fainali”.
“Lakini kuna hatua nyingine mbele”.
“Kiukweli hii ndio sababu ya kwanini nilijiunga na Madrid. Ndio maana niliamua kuja kujiunga na klabu kubwa zaidi duniani”
“Lengo ni kushinda makombe na mechi kubwa. Tunatakiwa kushinda taji, tutakuwa na fainali ngumu 
kwa timu yoyote itakayopita kesho”.
Ronaldo baada ya kufunga mabao mawili usiku huu amevunja rekodi ya Lionel Messi kwa kufikisha 
mabao 16 katika msimu mmoja wa UEFA.
Real Madrid wamefuzu kwa mara ya kwanza fainali tangu walipofanya hivyo mwaka 2002 
na kutwaa kombe na sasa wanatarajia kukutana na 
 Chelsea au Atletico Madrid ambazo zitapambana kesho katika uwanja wa Stamford Bridge.
Mechi ya kwanza katika dimba la Vicente Calderon mjini Madrid, 
Chelsea walilazimisha suluhu ya bila kufungana, hivyo wanahitaji bao 1-0 ili kufuzu fainali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates