Social Icons

Jumatano, 30 Aprili 2014

KAMA WEW NI MSHABIKI WA WANA JANGWANI:-KAVUMBAGU ASAINI AZAM MWAKA MMOJA

Didier Kavumbagu akiwa na Viongozi wa timu ya Azam Fc. 
Hans Mloli na Sweetbert Lukonge
UKISUSA sisi twala! Hivyo ndiyo Azam wanavyoweza kusema baada ya kumsainisha mkataba wa mwaka mmoja mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu.
Kavumbagu alimaliza mkataba na Yanga baada ya msimu uliomalizika hivi karibuni na Yanga hawakufanya naye mazungumzo yoyote, hali iliyoonekana kuwa walikuwa wakisita kumpa mkataba mpya.
Mshambuliaji wa Azam, Didier Kavumbagu akikamilisha kusaini mkataba wa mwaka mmoja.
Straika huyo ambaye alimaliza msimu akiwa ameifungia Yanga mabao 11, yakiwa ni nane pungufu ya aliyekuwa kinara, Mrundi mwenzake Amissi Tambwe wa Simba, alikuwa hajui hatima yake baada ya ligi kumalizika.
Azam wameamua kutumia mwanya huo kwa kumsainisha mkataba wa mwaka mmoja jana alasiri, kisha wakatulia kama vile hawajui kinachoendelea.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha kuaminika ndani ya Azam, mshambuliaji huyo baada ya kusaini mkataba, atarudi kwao kwa ajili ya mapumziko kabla ya kurejea kuanza maandalizi ya msimu mpya na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, mwezi mmoja baadaye.
“Kweli Kavumbagu amesaini mkataba wa mwaka mmoja na timu yetu, ni jambo ambalo uongozi hautaki kulitangaza kwa sasa kuepuka kuvuruga mambo, lakini ukweli ndiyo huo,” kilisema chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa jina.
Chanzo kingine kilicho ndani ya timu hiyo, nacho kililithibitishia Championi Jumatano kuwa, mshambuliaji huyo amesaini mkataba wa mwaka mmoja.

Paparazi ilimtafuta Katibu Mkuu wa Azam, Nassor Idrissa lakini simu yake haikuwa ikipatikana. Naye mwenyekiti wa klabu hiyo, Said Mohammed hakuwa tayari kuzungumza kwa undani kuhusiana na ishu hiyo.
“Kawaida yetu tukisajili mchezaji yeyote huwa tunaita waandishi wa habari, kwa hiyo subirini, kama ni kweli tutawaita tulizungumzie suala hilo,” alisema Mohammed kisha akakata simu bila kuhitaji kufafanua zaidi.
Usajili huo, unamaanisha kwamba, ushindani wa namba katika safu ya ushambuliaji ya Azam utaongezeka na huenda timu hiyo ikawa na moja ya safu za ushambuliaji kali zaidi kwenye Ligi Kuu Bara.

Tayari Azam ina mastraika wengine hatari wakiongozwa na Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast, John Bocco, Gaudence Mwaikimba na Mganda, Brian Umony. Azam FC wanajiandaa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates