Mara nyingi katika maisha yetu tuliwahi kukutana au kukumbana na masaibu, vimbwanga, vioja na mambo mengine mengi ya kukatisha tamaa ya kusonga mbele. Nina uhakika kama kuna baadhi yetu tungepewa fursa ya kuandika mahali kuhusu masaibu yaliyotukuta, basi tungejaza maelfu ya kurasa, kwa sababu ni dhahiri kuna mambo mengi tuliyopitia.
Huenda pengine vingekuwa ni vitabu vingi sana ambavyo vingeweza kuuzika sana. Baadhi wange vitumia kwa ajili ya kujifunza mambo mengi na kuwasahihisha wengine ambao walikatishwa tamaa au wamekatishwa tamaa au na mambo kama hayo.
Lakini kwa bahati mbaya au nzuri kuna wengine hawajapata nafasi hiyo au na wengine imewadondokea na wameipata kwa kutumia vyema nafasi hiyo. Kwa wale waliopata nafasi ya kuandika vitabu ambavyo vimesomwa sana duniani na kuhamasisha watu wengine na hata kubadili maisha yao, wamekuwa na mchango mkubwa sana na wanakumbukwa daima.
Mfano ni daktari na mtaalamu wa nyurolojia wa Marekani, Ben Carson, ambaye alipitia maisha magumu sana kabla ya kufikia mafanikio hayo. Kutokana na yale aliyokuwa amepitia hadi kufikia kuwa mtu mwenye jina kubwa duniani, aliamua kuandika kitabu ili awahamasishe watu wengine ambao wamepitia masaibu kama aliyoweza kupitia yeye.
Moja ya vitabu vyake vinavyopendwa na vilivyopata kuuzwa sana hapa duniani kile cha “ Gifted Hands” (Mikono iliyobarikiwa). Kitabu kilichoelezea maisha yake kwa ujumla mpaka alipofika kwenye ngazi ya mafanikio aliyopo sasa. Mwanzoni Ben Carson alikuwa na maisha magumu shuleni. Hali iliyosababisha kuwa wa mwisho darasani mara kadhaa.
Alikuwa akiitwa majina mbalimbali kutokana na hali hiyo, hivyo ikasababisha kuwa mtu wa hasira sana karibu na kila mtu. Akiwa amedhamiria kubadili maisha ya mtoto wake, mama yake alimnyima kuangalia televisheni wala kutoka nje na kucheza na wenzake hadi pale atakapokuwa amemaliza kazi zake za shule kila siku.
Muda huo aliweza kuutumia kusoma vitabu viwili na kuandika taarifa juu ya kile lichokisoma. Baada ya muda fulani wa kuishi maisha hayo tofauti alianza kuona mabadiliko hata shuleni walimu na wanafunzi wenzake walianza kumshangaa.
Aliwahi kusema : “Ni wakati ule ndipo nilipogundua kuwa sikuwa mpumbavu”. Huo ni ulikuwa mwanzo wa kihistoria uliobadilsha maisha yake ambayo yalikuwa magumu kupita kiasi.
Huo ni mfano mmoja tu lakini nafahamu kuwa wapo baadhi ya watu walioandika vitabu kama hivyo kwa ajili ya kuhamasisha watu wengine kuwa imara katika mafanikio na kile wanachokifanya katika maisha yao, ili baadae mbele kuwe kweupe.
Japokuwa siyo rahisi kwa sababu wakati mwingine utafanya hivi, halafu utaambiwa siyo vile. Basi tu watu wengine hulka yaoni kuona unapiga hatua moja mbele halafu unarudi hatua mbili nyuma. Jambo la muhimu ni kutokukata tamaa na kuongeza juhududi zaidi na zaidi kwa kile tunachokifanya. Kumbuka hakuna marefu yasiyo na ncha, hivyo huwezi kubaki kwenye umaskini milele ikiwa utaamua, ni lazima UFANIKIWE hakuna wa kukuzuia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni