Rwanda imeshutumu uamuzi wa mamlaka za Uingereza kumkamata kiongozi wake wa ujasusi wa Rwanda, Karenzi Karake, ambaye anatakiwa Uhispania kwa madai ya uhalifu wa kivita.
Waziri wa maswala ya kigeni Louis Mushikwabo ameelezea hatua hiyo kama wazimu na lengo lake ni kukandamiza waafrika akiongezea kwamba inatokana na madai ya watu wanaotaka kuwanyima haki waathiriwa wa mauaji ya kimbari nchini humo mwaka 1994.
Mamlaka ya Uhispania inataka kumhoji bwana Karake kuhusu kuhusika kwake katika mauaji ya raia wakiwemo wafanyikazi wa msaada kutoka Uhispania baada ya mauaji hayo.
Kesi ya Uhispania ilianzishwa mwaka 2008,lakini waandishi wanasema kuna wasiwasi kuhusu ushahidi wa mashtaka.
Makumi ya maelfu ya raia wa Rwanda wanadaiwa kufariki baada ya mauaji hayo ya kimbari aidha kupitia mauaji ya kulipiza kisasi nchini Rwanda ama katika kile waandishi wanataja kama wimbi la mauaji ya kikabila katika taifa jirani la jamhuri ya kidemokrasia ya Congo baada ya wapiganaji wanaoungwa mkono na serikali ya Rwanda kuwalazimisha raia wa kabila la Hutu kutoka katika kambi za wakimbizi karibu na mpaka.
Takriban watu laki nane hususan wale wa kabila la Tutsi waliuawa na wenzao wa kabila la Hutu katika mauaji ya kimbari yaliochukua miezi mitatu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni