Kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Charles Boniface Mkwasa leo ametangaza kikosi kipya cha timu hiyo ambacho kitaingia kambini hivi karibuni kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa marudiano wa kufuzu kucheza fainali za michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) utakaopigwa kwenye uwanja wa Namboole, Kampala Uganda. Mbali na kutangaza kikosi cha wachezaji 26, Mkwasa ametaja vipaombele vyake kwenye timu hiyo ambavyo amezingatia katika kuteua majina hayo. Amesema kitu pekee ambacho wameangalia ni uwezo wa mchezaji na nidhamu ndani na nje ya uwanja ili kuweza kujenga timu imara ambayo itakuwa na uwezo wa kupambana kwa kuwawakilisha watanzania. Ametaja pia benchi la ufundi ambalo atashirikiana nalo katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu ya kuinoa Stars mpya,
Waliotajwa kwenye benchi la ufundi ni pamoja na kocha msaidizi Hemed Morocco, kocha wa makipa Peter Manyika, madaktari wa timu watakuwa wawili watatangazwa baada ya kuwasiliana na idara ya tiba, mtunza vifaa Hussein Sued ‘Gaga’ Mshauri wa timu Abdallah Kibadeni ‘King Kibadeni Mputa’, mratibu wa timu Alhaj Ahmed Idd Mgoyi na meneja wa timu ni Juma Mgunda. Mkwasa pia ameomba ushirikiano kutoka kwenye vilabu vyote vya
Tanzania na pindi watakapoliona benchi la ufundi la Stars kwenye vilabu vyao watoe ushirikiano kwani watakuwa wakitembelea vilabuni ili kufuatilia kwa karibu maendeleo ya wachezaji ili kuendelea kukiimarisha kikosi chao. Ameishukuru kamati ya utendaji ya TFF kwa kumuamini na kumpa majukumu ya kuifundisha timu ya Taifa huku akikiri kuwa kazi hiyo siyo nyepesi kwasababu timu imeshapoteza mchezo wake wa nyumbani kwa idadi kubwa ya magoli lakini akakiri kuwa kwenye mpira chochote kinaweza kikatokea. Mbali na kuishukuru TFF, ameushukuru pia uongozi wa klabu yake ya Yanga kwa kumruhusu kwenda kuifundisha timu ya Taifa. Lakini Mkwasa ameonya kuwa, wachezaji ambao wameitwa kwenye kikosi cha Taifa wanatakiwa kuendelea kufanya vizuri kwenye kikosi cha Stars na vilabu vyao. Mchezaji yeyote ambaye hatopata nafasi ya kucheza kwenye klabu yake hatoitwa kwenye kikosi cha Taifa hata kama anacheza nje ya nchi kama mchezaji nwa kulipwa.
Kikosi kipya cha Stars ni; Mudathir Khamis (KMKM), Mwadini Ali (Azam FC) na Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga). Mabeki ni Shomary Kapombe (Azam), Michael Aidan (Ruvu Shooting), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba SC), Mwinyi Hajji Mngwali (KMKM), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga SC), Kevin Yondan (Yanga SC), Hassan Isihaka (Simba SC), Aggrey Morris (Azam FC). Viungo ni Jonas Mkude (Simba SC), Abdi Banda (Simba SC), Salum Telelea (Yanga SC), Frank Domayo (Azam FC), Simon Msuva (Yanga SC), Said Ndemla (Simba SC), John Bocco (Azam FC), Ramadhani Singano ‘Messi’ Simba SC na Deus Kaseke (Mbeya City). Washambuliaji ni Atupele Green (Kagera Sugar), Rashid Mandawa (Kagera Sugar), Ame Ali (Mtibwa Sugar), wakati wengine ambao wamewekwa akiba ni Juma Abdul wa Yanga SC, Mudathir Yahya wa Azam FC na Samuel Kamuntu wa JKT Ruvu. Kesho benchi la Ufundi la Stars litakutana na wachezaji wote walioteuliwa katika hoteli ya Tansoma, eneo la Gerezani, Dar es Salaam ili kuzungumza nao juu ya uzalendo na Mkwasa amesema Jumamosi timu itaenda kuweka kambi nje ya mji. Mwisho, amewaomba wapenzi na mashabiki wa Stars wasahau yote yaliyopita kwasababu timu ipo mikononi mwao nao wanaamini watafanya vizuri. Amewaomba watanzania kuiunga mkono timu yao kama ilivyokuwa zamani na kuacha vitendo vya kuwadhihaki wachezaji ikiwa ni pamoja na kuwapiga mawe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni