Ripoti kadhaa ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa kocha wa timu ya Mbeya City Juma Mwambusi amejiuzulu .
Hatua hiyo imekuja baada ya kuishuhudia timu yake ikipata mfululizo wa matokeo mabaya kwenye ligi ambapo katika michezo saba imeweza kushinda mchezo mmoja pekee huku ikitoka sare kwenye michezo miwili na kufungwa jumla ya michezo minne .
Taarifa mbalimbali toka jijini Mbeya zinasema kuwa kwa muda mrefu wachezaji wa Mbeya City walikuwa wamepoteza Imani na kocha wao hali ambayo mashabiki wanaamini kuwa imechangiwa na pengo la aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo Maka Mwalusi .
Mwalusi ambaye alihama Mbeya City na kwenda kuifundisha timu ya ligi daraja la kwanza ya Panoni Fc ya mjini Moshi anadaiwa kutoridhishwa na kitendo cha kupewa ‘mgao kiduchu’ wa zawadi ya kocha bora ambaye bosi wake Mwambusi aliipata hali ambayo ilionyesha kutothaminiwa kwa mchango wake .
Hali ya Juma Mwambusi ilikuwa inaonekana kuwa mbaya kadri Mbeya City ilivyozidi kupata matokeo mabaya hasa baada ya kujikuta ikipoteza michezo minne mfululizo mbele ya timu za Azam Fc , Mtibwa Sugar , Mgambo Jkt na Stand United.
Endapo taarifa hii itathibitika kuwa Kweli Mwambusi ambaye msimu uliopita alitwaa tuzo ya kocha bora wa msimu kabla ya kutwaa tuzo nyingine ya kocha bora wa mwezi septemba wakati ligi ilipoanza atakuwa kocha wa pili kupoteza kibarua chake baada ya Denis Kitambi ambaye alifukuzwa kazi na Ndanda Fc baada ya matokeo mabaya .
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni