Social Icons

Jumamosi, 11 Julai 2015

UKAWA NAKO KWA WAKA MOTO...

 Hatimaye leo wabunge wote wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanakutana na viongozi wao wa jijini hapa kumchagua mgombea urais atakayeviwakilisha vyama hivyo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Mkutano huo wa wabunge umekuja baada ya vikao kufanyika mfululizo wiki hii, huku kukiwa na mvutano kuhusu nani au chama gani kisimamishe mgombea urais.
Jana gazeti hili liliripoti kwa uhakika habari zilizotoka ndani ya vikao hivyo na kuthibitishwa na Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi, kuwa vyama hivyo vitaweka wazi mgombea wake wa urais leo.
“Tumeshakubaliana namna ya kugawana kata na majimbo 13 yaliyobaki na Jumamosi tutaweka wazi kwa wananchi. Pamoja na hilo pia tutamtangaza mgombea urais na chama anachotoka,” alisema Dk Makaidi.
Umoja huo umekuwa ukiongezeka nguvu tangu wakati wa mchakato wa Katiba mwaka jana, hali inayosababisha wafuasi wake kuamini kuwa yeyote atakayesimamishwa na umoja huo na kupigiwa kampeni kwa pamoja anaweza kujikuta anakuwa rais, mbunge au diwani.
Mvutano
Vikao vya umoja huo vilitawaliwa na mvutano baina ya wajumbe ndani ya umoja huo hasa katika nafasi ya mgombea urais baada ya kuwapo kwa watia nia zaidi ya mmoja.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya umoja huo kilisema kuwa isingekuwa rahisi vikao vya namna hiyo vikakosa mvutano huo, kutokana na baadhi ya wajumbe kushindwa kukubaliana na vigezo vilivyowekwa tangu mikutano ya awali.
Iliilazimu Kamati Kuu ya Ukawa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha kuwa maridhiano yanafikiwa ili kumpata mgombea, ndipo ikaamuliwa waalikwe wabunge wote wapige kura kupata mgombea.
Taarifa zaidi zilisema kuwa wajumbe walio wengi walikuwa wanaipa nguvu Chadema kutoa mgombea urais kutokana na nguvu yake hasa katika mikoa ya Bara, na ukweli kwamba tayari CUF imekwishapewa fursa hiyo Zanzibar.
Jana gazeti hili likinukuu vyanzo vya ndani ya kikao hicho, liliripoti kuwa licha ya kutangaza kugawana kata na majimbo yaliyobaki, jina la mgombea urais lingetangazwa leo endapo wajumbe wa Kamati Kuu ya Ukawa iliyokutana jana wangeafikiana.
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam jana, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema leo vyama hivyo vitalitangazia dunia chama kipi kitatoa mgombea wa Ukawa.
Siku chache baada ya baadhi ya wabunge kupewa adhabu ya kutohudhuria vikao vya Bunge na Spika Anne Makinda, Jumanne ya wiki hii Chadema ilifanya mkutano wa dharura kujadili mambo kadhaa ya kitaifa.
Siku moja baada ya kikao hicho, viongozi wa waandamizi wa Ukawa walikutana na kujadili mambo yanayohusu umoja huo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Baada ya vikao hivyo, mpaka jana Chadema iliendelea na vikao vyake vya ndani kujadili mambo kadhaa kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Ukawa kinachotarajiwa kufanyika leo kupitisha mgombea urais.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika licha ya kuthibitisha kuendelea kwa vikao vya ndani juzi, hakuwa tayari kusema chochote kwa sababu ajenda bado zinajadiliwa na kwamba kesho taarifa za uhakika zitatolewa kwa vyombo vya habari.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates