Shirikisho la Soka Marekani limetangaza mpango wa kupiga marufuku watoto wa chini ya umri wa miaka 10 kupiga mpira kwa kichwa.
Mpango huo utatatua kesi iliyowasilishwa mahakamani na wazazi dhidi ya shirikisho hilo. Hata hivyo, shirikisho hilo limejitetea na kusema lilikuwa limepanga hilo awali.
Shirikisho hilo pia linapanga kuweka kizuizi kwenye upigaji mipira kwa kichwa miongoni mwa watoto wa umri wa miaka 11 hadi 13 wakati wa mazoezi.
“Ingawa haya ni mapendekezo, yanatokana na ushauri wa kamati ya matibabu ya shirikisho la soka la Marekani,” shirikisho hilo limesema.
"Kwa hivyo, shirikisho la soka la US linahimiza sana ushauri huu ufuatwe.”
Kupiga mipira kwa kichwa miongoni mwa watoto huwa hatari kwa afya ya watoto ambao miili yao bado haijakomaa.
Dkt Michael Grey wa chuo kikuu cha Birmingham anasema kupiga mipira sana kwa kichwa huathiri misuli ya shingo pamoja na ubongo miongoni mwa watoto.
Kundi moja la wazazi na wachezaji watoto liliwasilisha kesi Agosti 2014 likituhumu mashirikisho yanayosimamia soka duniani, ikiwemo Fifa na shirikisho la soka la California kwa kuhatarisha maisha ya wachezaji wachanga.
Shirikisho la soka la Marekani limesema mabadiliko hayo mapya pia yatabadilisha kanuni kuhusu kuondolewa uwanjani kwa mchezaji anayepata majeraha kichwani na kupoteza fahamu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni