Rais wa Rwanda Paul Kagame ameshutumu vikali viongozi wa Burundi kutokana na mauaji yanayoendelea nchini humo nakuonya kuwa huenda kukatokea mauaji ya halaiki
Bw Kagame ameshangaa ni vipi viongozi wa taifa hilo jirani "wanaweza kuruhusu wananchi wao kuuwawa kiholela".
Rais Kagame alisema hayo Ijumaa, lakini matamshi yake hayakutangazwa hadi mwishoni mwa wiki, akionekana sana kumlenga Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
Akizungumza kwa Kinyarwanda Rais Kagame alisema: ''Tazama nchi jirani kama Burundi, maisha yao yamesimama kabisa. Lakini sababu ni ipi? Wana historia inayofanana na yetu.
Ila viongozi wao wapo kwa ajili ya kuua wananchi kuanzia asubuhi hadi jioni."
''Rais akajifungia sehemu isiyojulikana, hakuna anayejua sehemu alikojificha, hakuna anayezungumza naye, huyo anaongoza watu vipi?" alisema Bw Kagame, akihutubu katika hafla ya kuwatunuku Wanyarwanda waliosaidia kuwaficha na kuwaokoa Watutsi wakati wa mauaji ya kimbari 1994 pamoja na wanaharakati wanaotetea umoja na maridhiano miongoni mwa Wanyarwanda.
''Watu wanakufa kila siku, maiti zinabururwa barabarani. La kusikitisha ni kuwa bara la Afrika lina ugonjwa wake lenyewe kiasi kwamba hata nitalaumiwa eti nimekosea kuitaja nchi nyingine, eti ningecheza diplomasia au siasa. Siyo haki mimi nitasema wazi. Viongozi wanashinda wakiua watu, maiti zinatapakaa sehemu zote; wakimbizi wanarandaranda sehemu zote watoto, wanawake ....kisha unasema ni siasa. Hiyo ni siasa gani?"
Uhusiano kati ya Rwanda na Burundi umedorora sana tangu Bw Nkurunziza atangaze kuwa atawania urais kwa muhula wa tatu, hatua iliyopingwa na wapinzani.
"Utasema kuwa ni nani aliyesababisha matatizo ya Burundi? hata kukiwa na mtu anayekutakia mabaya atavutiwa na ubaya wako unaotenda...Hata kama ni mtu kutoka Rwanda anayesababisha machafuko nchini Burundi, bila shaka atavutiwa na maovu ya viongozi wa Burundi wanayotendea wananchi wao. Shida ni ya Warundi wenyewe," alisema Bw Kagame.
"Tatizo ni kwamba hawakupata somo kutoka kwetu (Rwanda), kutokana na yaliyosibu taifa letu wangepata somo hasa kutokana na baadhi ya Warundi wenyewe kuhusika katika yale yaliyolisibu taifa letu.
Afrika sijui tunaugua ugonjwa upi?"
Hayo yamejiri siku moja baaya watu 9 kuawa usiku na watu wenye silaha, ndani ya baa moja katika mji mkuu wa Bujumbura.
Askari wa usalama wanafanya msako katika kila nyumba, kwenye mitaa inayoonekana kuwa ni ngome za upinzani, baada ya muda uliowekwa na serikali kwa watu kusalimisha silaha zao kumalizika.
Watu takriban 20 wameuwawa nchini Burundi katika juma lilopita, huku maelfu ya watu wakitoroka makwao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni