DEREVA teksi Hamis Seleman (18), mkazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam, amekufa baada ya kuchomwa kisu kifuani na Ali Kimodo, aliyemfumania akiwa na mpenzi wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema tukio hilo lilitokea usiku wa saa 9:00 wa kuamkia mwaka mpya, katika eneo la Vingunguti mtaa wa Magenge, ambapo Seleman alifumaniwa na msichana mmoja (jina tunalihifadhi), mwenye umri wa miaka 15, mkazi wa Tabata.
Nzuki alisema kuwa baada ya tukio hilo kutokea, Kimodo pamoja na binti huyo walitoroka, hivyo polisi inaendelea na upelelezi kwa ajili ya kuwapata watu hao.
Aliongeza kuwa katika maeneo mengine ya mkoa huo, hali ilikuwa shwari katika sherehe hizo za sikukuu ya Mwaka Mpya.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya Kihenya alisema hali ilikuwa shwari katika eneo lake, kuanzia Krismasi na Mwaka Mpya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura alisema katika eneo lake, pia hakukuwa na tukio lolote kubwa la uhalifu na hali ilikuwa shwari.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni