Polisi katika jimbo la California wametaja majina ya washukiwa wawili ambao wameuawa na polisi baada ya watu 14 kuuawa kwa kupigwa risasi katika mji wa San Bernardino.
Mwanamume Syed Rizwan Farook, 28, na mwanamke Tashfeen Malik, 27, wameuawa kwenye ufyatulianaji wa risasi na polisi.
Farook alikuwa ameajiriwa na baraza la mji kwa miaka mitano, mkuu wa polisi wa San Bernardino Jarrod Burguan amesema.
Shambulio hilo lilitokea wakati wa hafla katika afisi moja Jumatano. Maelezo kuhusu waliofariki bado hayajatolewa.
Kisa hicho ndicho kibaya zaidi cha ufyatuaji wa risasi dhidi ya umma Marekani tangu watu 26 wauawe katika shule moja mjini Newtown, Connecticut mwaka 2012.
Bw Burguan, amesema watu 17 walijeruhiwa na kwamba polisi wana kila sababu ya kuamini kwamba wawili hao pekee ndio waliohusika kwenye shambulio hilo.
Shambulio lilo lilitekelezwa katika kituo cha Inland Regional Center ambacho huwasaidia walemavu na watu wenye matatizo ya kiakili. Hata hivyo, ufyauaji risasi huo hauonekani kuwa na uhusiano na wagonjwa hao.
Limetokea siku chache tu baada ya watu watatu kuuawa katika kliniki ya Colorado Planned Parenthood.
Rais wa Marekani Barack Obama ameshutumu shambulio hilo.
“Jambo moja tunalojua ni kwamba visa hivi vya ufyatuaji wa risasi humu nchini haviwezi kulinganishwa na kwingine duniani.”
Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la kijasusi la FBI David Bowdich anasema sababu kubwa ya mauaji hadi sasa haijafahamika.
"Kwa wakati huu ninaelewa moja ya maswali yenu ni kuhusu tukio hili la kigaidi. Ninawaeleza sasa kuwa hatujui kama hili ni tukio la kigaidi kwa hiyo tunaanzia mwanzo kufanya kazi na wenzetu waliopo katika eneo hili. Tunadhani inaweza kuwa, pia inaweza isiwe lakini tunafanya kazi bega kwa bega nao kuanzia mwanzo. Kama mambo yatabadilika tupo hapa na hakuna hatua yoyote itakayopotea wakati uchunguzi utakapokuwa unaendelea."
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni