Umoja wa Mataifa unasema mashambulizi yaliyofanywa Jumapili usiku na waasi wa Uganda huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) yamesababisha vifo vya takriban watu 24 akiwemo mlinzi mmoja wa amani wa Umoja wa Mataifa.
Taarifa iliyotolewa Jumatatu na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa, Maman Sidikou imelaani mashambulizi hayo na kusema kuwa ni kitendo cha kihuni na mashambulizi ya kihalifu katika mkoa wa Beni ambayo yamefanywa na kundi la kiislamu lijulikanalo kama Allied Democratic Forces (ADF).
Taarifa imesema waasi walishambulia malengo mawili, hospitali moja iliyopo eneo la Eringeti na kuua walinzi wa amani waliokuwa karibu na hapo. Taarifa imeongeza kuwa waasi pia walifanya wizi wa ngawira na kuchoma nyumba na maduka, na kwamba waasi 12 walikuwa miongoni mwa waliofariki.
Afisa mwingine wa juu wa Umoja wa Mataifa katika eneo hilo, Jose maria Aranaz, amesema mashambulizi yaliyowalenga raia na vifaa vya afya ni sawa na uhalifu wa vita. Pia ameapa kwamba waasi wa ADF watawajibishwa.
DRC mara kadhaa imefanya operesheni za kijeshi dhidi ya waasi wa ADF katika jimbo lenye utajiri wa madini la Kivu Kaskazini, ambalo linajumuisha mkoa wa Beni. Eneo hilo kwa muda mrefu nchini Congo limegubikwa na ghasia na ni eneo tete, huku makundi kadhaa ya waasi na wanamgambo yakipambana kuwania madaraka, ikiwemo kundi la uasi la Rwanda linalojulikana kama FDLR.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni