1. Malezi ni jukumu zito na linalohitaji kujitoa kwa hali ya juu sana, (labda tofauti na majukumu mengine mengi) bahati mbaya wazazi wengi hawayajui mapana na marefu ya jukumu hili. Kuzaa ni kazi ambayo wengi twaijua na twaiweza lakini malezi ni wachache wetu tunayajua, na wapo wengine hudhani wanajua kwa vile wanavyolea watoto wao kumbe wanachofanya sicho.
2. Kuwa mlezi inaenda mbali zaidi ya uwezo wako wa via vyako vya uzazi kuweza kutengeneza kiumbe kinachoitwa mtoto.
3. Matatizo mengi leo tunayokutana nayo katika mahusiano yetu, ndoa zetu, familia zetu na jamii zetu nikutokana na malezi mabovu wakati wa utoto. Wengi wetu tumekosa mapenzi ya wazazi wote au mzazi mmoja, tumekosa usalama na hali ya kujihisi kutosheka tukiwa na wazazi wetu, hali hizi zote huweza kuleta matokeo mabaya wakati wa makuzi yetu na hata tunapokuwa katika mahusiano yetu.
4. Kuwa mzazi au mlezi bora haimaanishi uwezo wa kuwapa watoto wako kila wanachohitaji na mara wanapokihitaji (hili ni wazo potofu). Haimaanishi kuhakikisha nyumbani kuna kilakitu wanachokifurahia watoto wakati wewe haupo kwa ajili yao, bali uwezo wa kuwepo nao, kuwajua na kuwafahamu vema hisia zao na kuwezakuingia katika maisha yao kila mara. Ni uwezo wakuwafanya watoto wako wafahamu kwamba sio tu kwamba unawapa vitu bali unajitoa kwa ajili yao ili tu kwamba wao na wewe mfurahi.
5. Wakati wote wazazi ndio vioo au mifano ya kuigwa (models) kwa watoto wao. Wengi wetu tumeharibika sio kwa jinsi ulimwengu ulivyotuathiri bali kwa jinsi ambavyo tulijifunza toka kwa walezi wetu. Baadhi ya misimamo yao na imani zao na namna ya utendaji wa mambo vimetuathiri vibaya katika maisha yetu leo. Kama mzazi jiulize leo wewe kama kioo unaakisi nini katika maisha ya watoto wako? Je wanachojifunza toka kwako au kwenu leo kitawafanya kujisifia au kuona aibu hapo baadae?
Mambo ya kuzingatia ili kumlea mtoto akue akiwa mwenye furaha
1. Mpe mototo wako muda na uhuru wa kucheza
Usipende kumpa mtoto wako ratiba ngumu iliyo jaa shuhuli za kufanya na majukumu ya kumfanya awebize wakati wote ukidhani ndo jinsi bora ya kumlea mtoto anayewajibika, Hapana!! Mtoto anayepewa ratiba chache na inayoruhusu muda wa uhuru binafsi huweza kuonyesha vitu anavyovipendelea na vile asivyovipenda, wazazi wengi hupata ugumu kujua vipaji vya watoto wao kwasababu ratiba zao kuanzia wakitoka shule zimejaa vitu ambavyo wazazi wamewapangia sio vitu ambavyo watoto wanavibuni wenyewe huku wakipewa msaada pale wanapohitaji. Sio kitu chema wazazi kulaazimisha watoto wao kufanya au kujua vile vitu ambavyo vi vipaji vya wazazi, kama mtoto atajua mwenyewe na kutamani basi haina shida lakini sio kulazimishwa au kushawishiwa.
2. Jali sana usingizi, mazoezi na chakula
Wakati wote wazazitukumbuke kuwa watoto wanapo lala ndio mchakato wa makuzi bora kiakili, kihisia na kimwili unapofanyika. Watoto pia wanatakiwa kufundishwa kutoona mazoezi kama jambo la anasa, hamu na kupenda kushiriki mazoezi ya viungo kuwe kitu cha kawaida kwao, hii itawasaidia sana katika makuzi ya kimwili na kuwaepusha na magonjwa yasiyoyalazima. Mazoezi huwapa ujasiri watoto wakiwa bado wadogo, kwahiyo kama mzazi unapenda kufanya mazoezi basi penda kumshirikisha mwanao hatakama sio kushiriki kiutendaji basi hata kuangalia na kumuelewesha kinachojiri. Kumbuka kumruhusu mtoto kuwa na muda wa kucheza kwasababu katika kucheza ndiko mazoezi ya viungo kwa watoto hufanyika. Hapa nazungumzia kucheza na sio kucheza kucheza.
3. Usiyachukue matatizo yao
Baadhi ya wazazi hupenda kuwasaidia watoto wao katika kilakitu, hata katika vile ambavyo watoto hao wangeweza kuvifanya wenyewe. Hata kama maranyingine inaonekana ni kitu kigumu basi waache wajaribu kwanza kwa njia zao wakipata shida taratibu watajifunza kuomba msaada (huku nako ni kujifunza), maranyingine utashangaa wanabuni njia ta kutatua tatizo hilo wao wenyewe na jambo linafanikiwa, mbinu hizi ni vema zianze watoto wakiwa wadogo kwasababu zinawasaidia sana hata katika maisha yao ya baadae. Pale unapokutana na watu wazima ambao hawawezi kuvumilia mara wanapokutana na matatizo madogo tu ujue hawakufunzwa jinsi ya kukabiliana na matatizo yao wenyewe, walitegemea msaada hata katika kitu kidogo. Kumbuka kuwa uwezo wa kuyashuhulikia matatizo na kuyatatua huanza tukiwa bado wadogo.
Jifunze kuziangalia changamoto za mtoto wako kama zawadi itakayomfanya ajifunze zaidi mbinu na ujuzi mpya. Changamoto hizi zitamfundisha kuwa mvumilivu na mstahimilivu. Zinamfundisha pia jinsi ya kuchukuliana na mazingira.
4. Check in “Jifunze kuingia kwenye maisha yao mara kwa mara”
Kama mzazi jifunze na jitahidi kuingia mara kwa mara kwenye maisha ya watoto wako. Usiwe mbali nao kihisia, lugha yako iwe inayoruhusu wao kujiachia kwako katika yote yanayowahusu. Tafuta sana kujua toka kwao, kwa mfano; uliza, “naonakama una huzuni leo vipi?” “hembu niambie shule yako ya jumapili ilikuwaje, ,lifundishwa nini?” Ikiwa atakukataa au kutokukubali katika jitiada zako zakuingia katika maisha yake basi jaribu tena baadae, usichoke haraka kumweka karibu.
5. Ruhusu hisia zao
Sio tu kwamba tunataka watoto wetu wawe na furaha bali pia tunatamani wafanye mambo kwa furaha pia, inasikitisha sana kuona mtoto wako analia na kugaragara sehemu wakati wenzake wote wana furaha, sasa famu kwamba suala hapa sio kumwambia acheke bali ni kushuhulikia kile kinachomfanya asionyeshe furaha. Mfundishe mtoto wako kuzigundua hisia zake na kuzielezea kwa maneno, kwa mfano; “Sijafurahi kwa sababu sijabembea mara ya pili kama wenzangu”. Mfundishe mtoto wako kufahamu kuwa ni sawa na nihaki yake kukasirika na sio dhambi wala kosa kwahiyo asiogope mradi tu hasira hizo ziwe zina maelezo bayana na yenye mantiki. Mtoto anapoweza kuzishuhulikia hisia ngumu itamsaidia kuwa na furaha ya kudumu katika maisha yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni