Social Icons

Alhamisi, 3 Desemba 2015

BAADA YA AGIZO LA ELIMU BURE, ADA ELEKEZI KWA SHULE BINAFSI KUJULIKANA DEC 15

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imewataka wazazi na walezi wenye wanafunzi wanaotegemea kuanza masomo au kuendelea na masomo katika shule binafsi mapema Januari mwezi ujao, kuvuta subira hadi Desemba 15, mwaka huu serikali itakapotoa maelekezo mbalimbali ikiwemo suala la ada elekezi.

Akizungumzia hatua zinazofanywa hivi sasa na serikali kuhusu ada elekezi kwa shule binafsi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome, alisema timu mbili hivi sasa zinafanya kazi ya uchambuzi wa michanganuo ya ada kwenye shule hizo, na baada ya muda mfupi uamuzi utatolewa.

“Hili sasa tumeliundia timu mbili za kufanya uchambuzi wa masuala ya ada katika shule za msingi na sekondari binafsi, ili kuwa na ada ekelezi kwenye utozaji wa ada kuanzia Januari mwakani,” alisema Profesa Mchome.

Aidha, alisisitiza kuwa katika mchakato huo, na kwa muda uliopo hivi sasa hadi Januari ni kipindi kifupi, hivyo inawezekana ada elekezi zikaanza kutumika kwa baadhi ya shule za msingi binafsi, kama eneo la majaribio.

Aliongeza kuwa Tanzania ina shule za msingi 17,000, zikiwamo za binafsi karibu 1,000 na zile za serikali 16,000 na kwamba iwapo wataanza na ada elekezi kwa shule hizo binafsi, wanaweza kuona utekelezaji wake.

Kwa upande wa shule za sekondari, Profesa Mchome alisema ziko zaidi ya shule 4,700 na kati ya hizo shule binafsi ni karibu 1,400 huku za serikali zikiwa 3,300 na kwamba mchakato wa ada elekezi kwa shule hizo binafsi unaendelea pia.

“Timu yetu inaendelea kufanya kazi kwenye mchakato katika shule za sekondari binafsi, zina wadau wengi kwa vile ni nyingi pia, hivyo hatuwezi kutoa maekelezo ya harakaharaka bila kuangalia utekelezaji wake kwa kina,” alifafanua Katibu Mkuu.

Alisisitiza kuwa kwa kuanzia, serikali ilifuta michango yote kwa shule zote nchini na kwamba hatua hiyo inazihusu pia shule binafsi na kuzitaka kutotumia ujanja wa kuingiza michango hiyo kwenye ada kwa madai ya kupandisha ada kwa mwaka ujao wa masomo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates