Social Icons

Ijumaa, 27 Desemba 2013

Siwataji walioficha mabilioni Uswisi ng’o, Zitto


Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amevunja ukimya na kusema hayuko tayari kwa sasa kuwataja Watanzania wenye mabilioni huko Uswisi na kuitaka Serikali ifanye uchunguzi.
Zitto ndiye aliyeibua hoja bungeni kuwa kuna Watanzania walioficha Sh315 bilioni katika taasisi za fedha nchini Uswisi.
Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Zitto alisema anasita kutaja majina hayo sasa ili kuepusha kile alichosema majina hayo kutumiwa vibaya bila kujali kama Watanzania walizipata fedha hizo kihalali au la na kuzihifadhi nje ya nchi.
Alisema ameshauri mchunguzi wa kimataifa anafaa kufanya kazi hiyo.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), amesema wastani wa Sh729.3 bilioni hutoroshwa kila mwaka kwenda nje ya nchi.
Alisema kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema kwamba yeye (Zitto) hakutoa ushirikiano wa kamati inayochunguza sakata hilo si ya kweli.
“Nataka niwahakikishie, nimekutana mara nne na kamati hii. Nimewapa mpaka jina la mchunguzi wa kimataifa atakayeweza kuwasaidia katika uchunguzi huu, leo naambiwa sitoi ushirikiano,” alisema Zitto.
Alisema mchunguzi huyo wa kimataifa ana uzoefu katika uchunguzi wa suala kama hilo na angeweza kuwatambua kwa majina na kiasi cha fedha na pia uhalali na uharamu wa fedha hizo.
Alisema ameshangazwa na hatua ya Serikali kumbeza pale alipopendekeza suala la kutafutwa mchunguzi wa kimataifa lakini siku chache baadaye ikatangaza magazetini nafasi ya kazi hiyo.
Tangazo hilo lilichapwa Desemba 17, mwaka huu siku ambayo Zitto alisema kwamba angesoma maelezo binafsi kujibu kauli ya Jaji Werema. Hata hivyo, alisema alikosa nafasi. Zitto amesema hashurutishwi na azimio la Bunge kutaja majina hayo kwa sababu yeye siyo chombo cha uchunguzi ambacho kinapaswa kuwa na mkono mrefu.
Alisema wakati akikabidhi majina ya Watanzania hao, angependa ushahidi huo uwe umefanyiwa uhakiki na vyanzo vyake vya kimataifa na vyombo vya usalama vya Serikali nchini.
“Siko tayari kutaja kwa sasa. Narudia tena kwa sasa hayo majina maana naweza kusababisha wahukumiwe na umma bila kupitia utaratibu uliowekwa na sheria zetu hapa nchini,” alisema Zitto.
Alisema inawezekana pengine shinikizo hili linatoka kwa watuhumiwa wenyewe baada ya kuona watu wengine waliokumbwa na kashfa nyingine walitajwa majina na hakuna hatua zilizochukuliwa.
“Mimi kama kiongozi makini na kama wasiwasi huu nilionao utakuwa wa kweli basi siko tayari kurudia makosa yaleyale ya kutaja majina halafu ikaishia hapo bila wahusika kushughulikiwa,” alisema.
Alisema suala la utoroshaji wa fedha nje ya nchi ni kubwa kuliko Watanzania wa kawaida wanavyolifahamu na kusema hilo ni janga la kitaifa na kimataifa na si la Zitto pekee.
Akitoa mfano, Zitto alisema uchunguzi unaonyesha mwaka 2010 pekee, kiasi cha Sh2.1 trilioni kilitoroshwa hapahapa nchini na mwaka 2011 kiasi cha Sh1.3 trilioni kilitoroshwa kwenda nje.
Alisema taarifa za mashirika ya kimataifa zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kiasi cha fedha kilichotoroshwa hapa nchini na kupelekwa nje ya nchi ni Sh7.3 trilioni.
Zitto alisema hali hiyo si nzuri hata kidogo kwani inatokea wakati kuna Watanzania wanaoishi katika lindi kubwa la umaskini na kutahadharisha kuwa ipo siku kundi hilo linaweza kuchukua hatua.
“Nawaomba wenzangu waifanye vita hii kama ya Watanzania wote, wafahamu wale wenye masilahi na fedha hizi hawataacha kufanya kila njia kubeza vita hiyo. Mimi ni mpuliza filimbi tu katika vita hii na Watanzania wajue sina uwezo wa kuishinda vita hii peke yangu bila kuungwa mkono na wabunge, wananchi na hata Serikali.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates