Social Icons

Jumatano, 12 Februari 2014

RAGE -NIMEPOKEA BARUA TATU KUTOKA FIFA, IMO INAYOMHUSU OKWI



Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), limetuma barua tatu tofauti kwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, moja ikiwa ni ile inayomhusu Emmanuel Okwi ambaye sasa yuko Yanga.
Moja ya barua ambazo Rage amepewa kopi na Fifa ni ile ambayo Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa), limemuomba Okwi kurejea Uganda na kuitumikia timu ya taifa katika michuano ya kimataifa.

Pamoja na barua hiyo, Rage amethibitisha kupokea barua hizo tatu kutoka Fifa ikiwemo ile ya Etoile du Sahel ya Tunisia kuomba kuongezewa muda wa kulipa deni la dola 300,000 wanazodaiwa na Simba kutokana na mauzo ya Okwi.

“Kweli nimepokea barua hizo, moja ni ile ambayo Etoile ambao mwezi huu ndiyo ulikuwa mwisho kulipa dola 300,000, sasa wameomba waongezewe muda hadi Septemba, mwaka huu ili waweze kulipa.
“Fifa wao wamenitumia kopi lakini barua hiyo ni kutoka kwao Etoile kwenda Fifa na wamethibitisha kwamba ni kweli Simba inawadai,” alisema Rage.
Barua ya tatu kati ya hizo kwa mujibu wa Rage ni ile ambayo inaonyesha namna klabu hiyo ya Tunisia ilivyomshitaki Okwi kwa Fifa kutokana na kuonyesha kukiuka mambo kadhaa wakati akijua mkataba wake nao unamalizika mwaka 2016.
“Katika ile barua ya kuhusiana na suala la kulipa, Fifa wametaka tusaini na kukubali kwamba sasa mwisho utakuwa Septemba 30 na tayari barua hiyo nimeikabidhi kwa Hans Pope,” aliongeza Rage.
Tayari Okwi yuko nchini na Yanga imemsajili ingawa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeamua kusimamisha usajili wake hadi litakapopata ufafanuzi kuhusiana na usajili wake.
Wakati Fifa ilitoa kibali kwa Okwi kucheza SC Villa ya Uganda kwa miezi sita, lakini Yanga ikamnunua na kuingia naye mkataba wa miaka miwili, suala ambalo limezua mzozo mkubwa huku Simba wakiendelea kusisitiza kulipwa fedha zao ambazo mwanzo walimuuza na hawakulipwa. 
Okwi amekuwa akisisitiza kwamba anataka kuichezea Yanga ambayo imemsajili, huku akieleza amekuwa akiumia moyoni kuona wenzake wakicheza naye akiwa jukwaani kama mtazamaji. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates