Social Icons

Jumatano, 5 Februari 2014

ICC:NINI HATMA YA KESI YA KENYATTA?


Rais Kenyatta na wakili wa Naibu Rais William Ruto Karim Khan
Hatma ya kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta katika mahakama ya kimataifa ya jinai ICC, inatarajiwa kuamuliwa leo Jumatano, wakati ambapo viongozi wa mashitaka katika mahakama hiyo wataoomba muda wa ziada kujiandaa kwa kesi.
Mawakili wa Kenyatta wanatumai kuwa kesi hiyo ambayo imezua mgawanyiko kati ya mataifa ya Afrika itatupiliwa mbali.
Mataifa ya Afrika yamekuwa yakikosoa ICC kwa kulenga tu viongozi wa Afrika.
Kesi dhidi ya Kenyatta ni muhimu kwa ICC ambayo imefanikiwa tu kumhukumu mtu mmoja huku nyingi ya kesi zinazofikishwa katika mahakama hiyo zikitupiliwa mbali kutokana na sababu nyingi tu tangu kubuniwa miaka 11 iliyopita.
Wadadisi wanasema kuwa huenda kesi hiyo ikaleta msukosuko katika kanda ya Afrika Mashariki ikiwa viongozi wa mashitaka watasisitiza iendelee.
Rais Kenyatta alifikishwa ICC kutokana na tuhuma kuwa alikuwa mmoja wa washukiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya mwaka 2007/2008. Anakabiliwa na makosa ya mauaji na uhalifu mwingine dhidi ya binadamu.
Kadhalika Kenyatta alishitakiwa pamoja na makamu wake wa Rais William Ruto kwa tuhuma sawa. Kesi dhidi ya Ruto inaendelea katika mahakama hiyo.
Mataifa ya Magharibi ambayo yanajitolea katika kuunga mkono ICC, pia yana wasiwasi kuhusu uhusiano wao na Kenya ambayo inaonekana kama mshirika mkubwa katika vita dhidi ya kundi la wanamgambo la Al Shabaab nchini Somalia.
Watu 1,200 walipoteza maisha yao katika ghasia za uchaguzi mkuu mwaka 2007/08 huku maelfu wakilazimika kutoroka makwao. Wote wamekanusha mashitaka.
Viongozi wa mashitaka ICC wanasema kuwa Kenyatta aliongoza ghasia hizo lakini kesi dhidi yake imefanywa dhaifu kutokana na baadhi ya mashahidi kujiondoa katika kesi hiyo tangu kesi hiyo kuwasilishwa katika mahakama hiyo miaka minne iliyopita.
Kesi yenyewe ilitarajiwa kuanza Jumatano, lakini ikaahirishwa kwa mara ya nne mwezi jana wakati ambapo wendesha mashitaka waliposema kuwa shahidi mwingine alijiondoa kwenye kesi huku wakiomba mahakama kuwapa muda zaidi kutafuta ushahidi.
Viongozi wa mashitaka wanasema kuwa mashahidi wengi wamehongwa au kutishwa kiasi cha kujiondoa katika kesi hiyo.Chanzo BBC Swahili

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

 
 
Blogger Templates